Tuesday, April 18, 2017

Tatizo ni wabunge, kiti cha Spika au kanuni?

 

By Matern Kayera

Uchaguzi wa wabunge watakaoliwakilisha taifa kwenye Bunge la Afrika Mashariki hatimaye umefikia tamati, licha ya kutawaliwa na mvutano mkali wa kikanuni.

Kwa mujibu wa katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, walioshinda uchaguzi huo kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ni Adam Kimbisa, Happiness Lugiko, Dk Ngwaru Maghembe, Fancy Nkuhi; kutoka Zanzibar ni Dk Abdullah Makame na Maryam Yahya.

Kwa upande wa upinzani aliyechaguliwa ni Habib Mnyaa kutoka Chama cha Wananchi (CUF), huku wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao ni aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha na aliyewahi kuwa Mbunge wa Nyamagana Ezekiah Wenje, wakipigiwa kura za hapana.

Pamoja na kumalizika kwa uchaguzi huo, tumeshuhudia mabishano makali bungeni kuhusu kanuni zilizotumika kusimamia mchakato mzima wa kuwapata wawakilishi hao.

Mvutano huo wa kanuni ulitokana na hoja iliyotolewa na upande wa upinzani wakitaka wagombea wa Chadema wapitishwe bila kupingwa, jambo ambalo wabunge wa CCM pamoja na Spika walilipinga na kutaka kura zipigwe kuamua hatima ya wagombea hao.

Kwa kuwa mara nyingi tunashuhudia mivutano mikali ya kikanuni bungeni, swali hapa ni kwamba, je tatizo ni wabunge hawazielewi kanuni zao vizuri au kiti cha spika au kanuni zenyewe zina upungufu kiasi kwamba zinasababisha mivutano yote hiyo?

Ni vigumu kuelewa jinsi wabunge na kiti cha spika wanapotumia muda mrefu kubishana juu ya jambo moja tu, huku mbele yao kukiwa na mambo mengine muhimu ya kujadili kwa faida ya Taifa.

Hali hii inaleta taswira kwamba ama kanuni hazieleweki vizuri kwa wawakilishi wetu au zina upungufu. Kama kanuni ziko wazi juu ya jambo fulani na wabunge wanazifahamu kanuni hizo vizuri, kwa nini mivutano isiyo na ulazima itokee na kuchukua muda mrefu ambao ungetumika kwa mambo mengine muhimu?

Utofauti wa kiitikadi wa kivyama hauwezi kuwa sababu ya msingi kwa wawakilishi hao wa wananchi kulumbana juu ya kanuni zao.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi) James Mbatia mara nyingi huwataka wabunge na wananchi kuweka mbele masilahi ya Mama Tanzania bila kujali tofauti zozote walizonazo.

Aidha, Rais John Magufuli mara kwa mara amekuwa akihimiza wananchi kujali masilahi ya Taifa kwanza kabla ya kitu kingine chochote.

Uwakilishi kwenye Bunge la Afrika Mashariki ni jambo kubwa kwa taifa ambalo hatupaswi kucheza nalo kwa sababu tu ya weledi ama wa kupindisha kanuni au kukataa tu matakwa ya kanuni.

Ni wazi kwamba uwakilishi wetu huko unapaswa kuwa mzuri kwa kupeleka watu wenye sifa na uwezo mkubwa wa kutetea masilahi ya taifa bila kujali vyama vyao wanavyotoka.

Kubishana juu ya kanuni siyo jambo baya, ila mantiki iliyokaa kwenye mvutano huo ina faida gani kwetu wananchi na Taifa?

Mara nyingine ukiangalia mivutano hiyo kuhusu kanuni kati ya wabunge wa CCM na upinzani utadhani ni wawakilishi wa mataifa mawili tofauti wanaobishana juu ya masilahi ya mataifa yao; kumbe wote ni Watanzania waliochaguliwa na Watanzania wenzao ili wawakilishe mawazo yao bungeni.

Wabunge wetu watambue kwamba wananchi hawahitaji maneno mengi kwenye kufikisha hoja zao, bali utendaji wao wenye tija na wenye kuleta majibu kwa changamoto mbalimbali wananchi wanazokabiliana nazo kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kubishana kupita kiwango juu ya kanuni wakati wananchi hawana ajira, maji safi na salama, barabara nzuri, makazi bora na mahitaji mengine ya msingi, ni sawa na kutowatendea haki.

Kanuni zimo kwenye uwezo wenu wabunge; kama zina upungufu na ikiwa udhaifu huo ndiyo unaowafanya mtumie muda mwingi kuvutana bila sababu ya msingi, zibadilisheni ili zikidhi mahitaji na matarajio ya wananchi.

Au kama tatizo ni ninyi wenyewe kutokana na tofauti zenu za kivyama, tambueni kwamba Mama Tanzania hafaidiki lolote na hiyo mivutano yenu.

Nyinyi wote ni Watanzania, mmetumwa na wananchi kuwawakilisha kitaifa na kimataifa, wekeni taifa mbele kwanza kisha vyama vyenu vifuate, ndipo kanuni mlizojitungia zitawasaidia kufikia malengo ya uwakilishi wenu.

Maten Kayera ni mwandishi wa Mwananchi. 0754574248

-->