UCHAMBUZI: Timu za Ligi Kuu zilazimishwe sasa kujenga viwanja

Muktasari:

  • Wiki iliyopita Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kupitia kwa mkurugenzi mtendaji wake, Boniface Wambura ilitangaza mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/2019, ikiwa ni wiki na nusu kabla hata haijaanza.

Kwa mara nyingine tumeshuhudia changamoto ya miaka nenda rudi, inayolikumba soka letu, ya viwanja hivyo kusababisha kuahirishwa kwa mechi au ratiba kupanguliwa.

Wiki iliyopita Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kupitia kwa mkurugenzi mtendaji wake, Boniface Wambura ilitangaza mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/2019, ikiwa ni wiki na nusu kabla hata haijaanza.

Wambura alisema kwa kiasi kikubwa upanguaji huo wa ratiba umeihusu zaidi Simba ambayo inautumia Uwanja wa Taifa kwa mechi zake za nyumbani ambao kwa sasa unatumika kwa mechi za mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Bodi iliweka wazi kuwa sababu pekee ya kupanguliwa kwa ratiba ni uwanja huo unaotumiwa na Simba na Yanga kutokana na klabu hizo kutokuwa na viwanja vyao. Mmiliki wa Uwanja wa Taifa ni Serikali na mara nyingi unakuwa na matumizi mengine nje ya soka.

Kwa sasa matumizi ya uwanja huo yameelekezwa katika mechi ya michuano hiyo ya vijana chini ya miaka 17.

Mbali na Uwanja wa Taifa Wambura, alisema pia Uwanja wa Jamhuri Morogoro, ambao ulikuwa utumike kwa mechi ya Ligi Kuu kati ya Mtibwa Sugar na Yanga, umekodiwa kwa ajili ya shughuli za kijamii kuanzia Agosti 23 hadi 30, hivyo mechi ya Ligi Kuuhaziwezi kuchezwa ndani ya kipindi hicho.

Kutokana na uamuzi huo wa wamiliki wa viwanja hivyo, Bodi ya Ligi imelazimika kupangua ratiba ya ligi inayozihusisha mechi ambazo zimeingiliana na ratiba hiyo ya wamiliki.

Bila shala mabadiliko haya yameleta athari ambayo haiishii kwenye timu hizo pekee, bali imekwenda hadi kwa wadau wa soka nchini, kwa kuwa mechi za Simba kwa mfano zilizokuwa zichezwe uwanja wa Taifa sasa zitachezwa kwenye Uwanja wa Uhuru.

Sote tunafahamu tofauti iliyopo kubwa iliyopo tangu miundombinu hadi ubora wa viwanja vyenyewe ni tofauti wakati Uwanja wa Taifa ukichukua mashabiki wanaofikia 60,000 Uwanja wa Uhuru, unachukua mashabiki wasiozidi 25,000 hivyo mashabiki waliopania kuuona mchezo huo kama watajitokeza wote bila shaka hawataenea.

Upanguaji huu wa ratiba uliojitokeza kabla ya Ligi kuanza ni sehemu ndogo tu na inayoonyesha athari ambayo hupatikana karibu kila msimu kutokana na timu nyingi za ligi kuu kutokuwa na viwanja vyao ninafsi.

Athari ya timu kutokuwa na kiwanja ni kubwa sana, mbali ya kukosa fedha nyingi ambazo zingetokana na viingilio vya milangoni lakini pia timu kukosa uwanja wake binafsi utakaochukua walau watazamaji 15,000 ni tatizo kubwa kwa klabu zetu.

Nadhani muda umefika sasa timu hizi zibanwe na kuweka utaratibu a kupata uwanja utakaoingiza watazamani walioketi hata wasiopungua 10,000.

Mpango wetu unaweza kuanzia chini kidogo, tunaweza kushinikiza kwa timu za kuanzia daraja la chini angalau kuanzia zile zinazotinga Ligi Daraja la Pili ambazo kimsingi zinabakiza daraja moja kufikia kucheza Ligi Kuu.

Hizi tunaweza kuzilazimisha kupata uwanja utakaokuwa na ukubwa wa eneo la anagalau lisiwe chini ya ekari 15 ambazo kwa kujibana panaweza kujengwa uwanja utakaotosha kuwa na mambo yote muhimu kama vyumba vya kupumzikia timu na kubadilishia mavazi, vyumba vya waamuzi, huduma ya kwanza ukumbi wa mikutano, vyoo na kadhalika.

Timu zikipata uwanja unafanyika upembuzi yakinifu na makandarasi wanatafutwa wenye masharti nafuu ambao wako tayari kujenga na kulipwa kidogokidogo kupitia mapato ya milangoni.

Bila shaka timu ya daraja la pili ikijengewea uwanja hata kama itachelewa kujikatia tiketi ya kupanda daraja lakini ikiwa na uwanja haitashindwa kumlipa mkandarasi aliyeujenga kutokana na mapato ya viingilio au hata kwa mikopo kutoka serikalini au katika taasisi za kibenki.

Hili linawezekana iwapo itapitishwa sharia mahsusi, sidhani kama Baraza litashindwa kuisukuma TFF kusimamia hili, iweze kuzidhamini klabu kuingia mikataba.

Ukiangalia taasisi kama ile ya mifuko ya jamii ya akiba za uzeeni mfano NSSF au taasisi za kifedha kama benki za kibiashara zinaweza kuwajengea viwanja na kuanza kulipwa baada ya ujenzi kukamilika.

Ninajiuliza hivi kweli tungekuwa tupo makini na tuna malengo ya kufika mbali kwenye soka letu tungeendelea kukwazwa na tatizo la viwanja hadi leo.

Sioni sababu za msingi za Mtibwa Sugar kutokuwa na uwanja mkubwa na wa kisasa utakaowezesha angalau kuingiza watazamaji 15,000 walioketi, wakati mkoa wa Morogoro bado una maeneo makubwa ya wazi nje kidogo tu ya mji.