Tufuate ushauri wa madaktari kuepuka kujifungua watoto walemavu

Muktasari:

  • Pamoja na wengi wetu kuamini kuwa mtu kupatwa matatizo ni kudra za Mwenyezi Mungu, lakini madaktari wanaamini kuwa maradhi mengi yanaweza kuzuilika kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

Tatizo la watoto kuzaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi limekuwa changamoto kwa wazazi na kwa Taifa kwani limejikuta likitumia fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia matibabu yao.

Pamoja na wengi wetu kuamini kuwa mtu kupatwa matatizo ni kudra za Mwenyezi Mungu, lakini madaktari wanaamini kuwa maradhi mengi yanaweza kuzuilika kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

Wanasema chanzo cha watoto kuzaliwa na vichwa vikubwa ni ukosefu wa virutubisho muhimu mwilini ambavyo mama anatakiwa avipate kabla hajabeba ujauzito.

Inakadiriwa kuwa hapa nchini watoto 4,000 huzaliwa na matatizo hayo kila mwaka japo wanaofikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ni takriban 600 tu, huku wengine ikiwa haijulikani wanakwenda wapi.

Serikali katika kupambana na changamoto hiyo, imeamua kugawa bure vidonge vya folic acid kwa wajawazito ili kuhakikisha kuwa watoto wanazaliwa wakiwa na afya njema.

Hata hivyo, mbali na kumeza vidonge hivyo, virutubisho hivyo vinaweza kupatikana kwenye matunda, mboga za majani, mayai na vyakula vyote vyenye protini.

Wanawake ambao bado wapo kwenye umri wa kuzaa wanashauriwa kula vyakula vyenye virutubisho hivyo ili kuwaepusha na matatizo ya kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Kwa hapa nchini, takwimu zinaonyesha watoto wengi wanaozaliwa na matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wanatokea katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Mwanza.

Hospitali ya Taifa Muhimbili inapokea takriban watoto watano kwa wiki wenye matatizo ya vichwa vikubwa wanaofika kwa matibabu ambayo matibabu hugharimu kuanzia Sh200,000 hadi milioni moja.

Madaktari wanasisitiza kuwa ugonjwa huu unaepukika, kinachotakiwa ni kupatikana kwa virutubisho vya kutosha kwa mama kabla hajabeba ujauzito na wakati wa ujauzito. Hapa naomba niweke wazi kuwa Watanzania wengi bado hatuoni umuhimu wa kujiandaa kwa ujauzito kwani wapo wanaojigundua ni wajawazito wakati mimba ikiwa na miezi mitatu. Ujauzito ni jambo la msingi na linalohitaji ufuatiliaji na umakini mkubwa katika malezi yake hadi kuhakikisha mtoto anazaliwa, lakini ukweli ni kwamba, wengi wetu bado hatutilii maanani suala hilo.

Kadhalika, suala la matumizi ya vidonge vya folic acid miezi mitatu kabla na baada ya ujauzito, wanawake pia wanakosa taarifa hizo maana wengi wao wanasubiri mimba ifikie miezi mitatu waanze kwenda kliniki huko ndiko wanakokutana na taarifa hizo.

Wakati mwingine hata baada ya kuanza kuhudhuria kliniki na kupatiwa vidonge hivyo, wapo baadhi ya wajawazito hupuuzia kuvimeza tena bila sababu yoyote.

Baadhi ya wajawazito wanaona ni kero kuvimeza vidonge hivyo wakidai eti hawajaelezwa kwa kina madhara ya kuacha kuvitumia.

Nishauri tu mamlaka zinazohusika kupeleka elimu hiyo katika shule zetu za sekondari kusudi vijana walio shuleni watambue umuhimu wa virutubishi hivi wakati wa ujauzito ili kuepusha jamii na changamoto ya gharama za matibabu kwa watoto hawa.

Shuleni ndiyo sehemu pekee ambayo watu wanaweza kupata nafasi ya kujifunza mambo tofauti ambayo baadaye yanawawezesha kuishi vyema, kwani baada ya shule watu wengi hujikuta wakiwa bize na harakati za maisha na kusahau masuala mengine ya msingi.

Najua wapo baadhi ya watu watakaolipinga hili kwa kudhani kwamba shuleni hapafai kuzungumzia masuala ya ujauzito, lakini niwaambie tu kwamba, kuna baadhi ya vitu tukiendelea kuviogopa, madhara yake ni makubwa kwa jamii.

Katika somo la baiolojia, wanafunzi tangu wakiwa kidato cha pili hufundishwa masuala ya mifumo yote ya uzazi na jinsi inavyoweza kufanya kazi.

Huu sasa ni wakati kwa somo hilo kwenda mbali zaidi ili kuelimisha namna ya kutunza pia ujauzito. Watanzania tunahitaji kuunganisha nguvu ili kukabiliana na changamoto hii ambayo inasababisha gharama kwa Taifa na kupoteza nguvu kazi kubwa ya uzalishaji. Tusaidiane kuiokoa jamii na tatizo hili ambalo linaepukika kwa njia tu ya kutoa elimu iliyo sahihi.

Nashauri tuelekeze nguvu katika shule zetu za sekondari kwa kuwandaa vijana wetu kuwa kina mama na kina baba wanaoelewa vizuri elimu ya afya hasa afya ya msingi ambayo inajumuisha utunzaji wa ujauzito.

Lilian Timbuka ni Mhariri wa Jarida la Afya la gazeti la Mwananchi. Anapatikana kwa simu namba: 0713-235309, email - [email protected]