Tuiwezeshe Sido kutupeleka Tanzania ya viwanda

Muktasari:

  • Kama mojawapo ya mkakati wa kutekeleza dhamira hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano imeanzisha mkakati wa ujenzi wa viwanda.

Dira ya Maendeleo ya Taifa inaelekeza Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kama mojawapo ya mkakati wa kutekeleza dhamira hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano imeanzisha mkakati wa ujenzi wa viwanda.

Ni mkakati ambao aghalabu umekuwa ukitajwa na viongozi katika majukwaa mbalimbali na hilo ni kwa sababu viwanda ndio mwelekeo wa Serikali yetu kiuchumi.

Nasi tunaunga mkono mkakati huu kwa kuwa ni mwelekeo sahihi kuelekea kuwa na Tanzania ya uchumi wa kati na baadaye uchumi mkubwa.

Katika safari hii ya Tanzania ya viwanda, pamoja na ukweli kuwa kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa namna yake, kwetu sisi msisitizo mkubwa tunauweka katika uwekezaji na uimarishaji wa vyombo ambavyo tayari vimeshajipambanua kama waendelezaji wa viwanda nchini.

Mojawapo ya vyombo hivyo ni Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).

Kwa muda mrefu sasa, Sido imekuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo na kubuni mashine rahisi zinazotumiwa na wajasiriamali wengi nchini walioanzisha viwanda vidogo na vile vya kati.

Kwa kufanya hivyo, chombo hiki kimekuwa kikichochea ajira kwa wananchi na kuwa msingi wa kukuza uchumi, maendeleo ya nchi na ustawi wa raia. Tunapohamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda kutoka kwa wawekezaji wa nje na wa ndani, chombo kama Sido hakina budi kutazamwa kwa jicho la karibu, kwa kuwa ndio mkombozi wa wananchi.

Kwa kukitumia chombo hiki, wananchi wanaweza kuanzisha viwanda vingi vidogo, vya kati na hatimaye viwanda vikubwa.

Inatia moyo kusikia kuwa mwaka huu, Serikali imeitengea Sido jumla ya Sh5.5 bilioni, fedha ambazo pamoja na mambo mengine, uongozi wa shirika hilo unasema utazitumia kujenga ofisi mpya na kuziboresha zile za zamani.

Tunaamini ikiwa Sido itajengewa uwezo kama huu, bila shaka itajikita katika kazi ya kutoa mafunzo ya utengenezaji wa zana rahisi za uzalishaji na uchakataji wa mazao, jambo litakalofanya safari ya kuiendea Tanzania ya viwanda kuwa na mafanikio makubwa.

Katika kilimo kwa mfano, tumekuwa tukiona mashine nyingi rahisi zikitumika katika nchi nyingine. Hizi zikizalishwa kwa wingi nchini sio tu zitavutia wengi kuingia katika shughuli za kilimo, lakini uzalishaji wa mazao mbalimbali utaongezeka.

Kukua kwa uzalishaji wa kilimo unaotokana na Watanzania kulima kwa teknolojia na mashine za kisasa, kunamaanisha viwanda vitakavyoanzishwa vitakuwa na uhakika wa kupata malighafi.

Tunasisitiza kuwa ili ajenda ya kuelekea Tanzania ya viwanda iwe na mashiko, vyombo kama Sido havipaswi kupewa kisogo. Huko ndiko kwenye chimbuko la viwanda vidogo ambavyo kwa uzoefu Watanzania wanaweza kuvimudu.

Tanzania ya uchumi wa kati haitojengwa na viwanda hasa vya wawekezaji wenye mitaji mikubwa kutoka nje pekee. Tunahitaji ushiriki wa wananchi kupitia viwanda vidogo, vya kati na hatimaye viwanda vikubwa.

Ili ushiriki huo uwe na tija, tuanze sasa kuviwezesha vyombo kama vile Sido ili vitusaidie katika safari hii ya matumaini ya Tanzania ya viwanda.