Tujifunze uandishi wa makala-maoni

Muktasari:

  • Makala haya ya tatu na ya mwisho, inakushirikisha moja kwa moja katika kufanya uchaguzi wa kipi hasa ung’ang’anie na kuandika.
  • Makala ya pili ilikuwa juu ya mfano wa ajali ya meli MV Nyerere. Kulikuwa na maeneo manane yenye jumla ya vipengele 106.

Mpaka sasa safu hii imejadili katika makala mbili, mifumo, taratibu na mbinu za kuandika makala-maoni.

Makala haya ya tatu na ya mwisho, inakushirikisha moja kwa moja katika kufanya uchaguzi wa kipi hasa ung’ang’anie na kuandika.

Makala ya pili ilikuwa juu ya mfano wa ajali ya meli MV Nyerere. Kulikuwa na maeneo manane yenye jumla ya vipengele 106.

Nieleze hapa kuwa kipengele kimoja katika eneo moja, kinaweza kutotolewa na hatimaye kuwa makala kamili inayojenga kiu au inayokata kiu.

Labda tuanze kwa onyo. Maeneo yote manane yakiwekwa katika makala moja, utakuwa na zaidi ya maneno 10,000. Hii ni makala ndefu yenye vitu vingi na huenda isiyoeleweka.

Au, itabidi utoe makala 16 za maneno 650 kila moja. Kwa makala moja kila siku utachukua zaidi ya wiki mbili kuchapisha zote, kwa mfano, katika gazeti la Mwananchi.

Kwahiyo, njia bora na nyepesi ni kuchagua kile ambacho unaona kinagusa wahusika na jamii kwa jumla; kinachoweza kufafanua mazingira, kueleza tatizo na kuleta ufumbuzi; au kuchukua kile ambacho mhariri wako amekuelekeza uzingatie.

Utaona kuwa unaweza kuelekezwa na chombo chako au kujielekeza mwenyewe.

Lakini hata baada ya kuelekezwa na chombo chako, bado una nafasi ya kutafiti na kuandika zaidi ya ulichoambiwa kuzingatia hasa kama uko kwenye eneo la tukio.

Chukua mfano uleule wa ajali ya MV Nyerere. Wakati chombo chako kinaweza kukutuma kuandika juu ya tukio; wewe unaweza baadaye kujituma kuandika juu ya mazingira na mfumo wa usafiri katika eneo hilo.

Wakati chombo chako cha habari kinakutaka uandike juu ya uokoaji na uopoaji maiti; wewe waweza kujituma pia kulinganisha uokoaji unaouona na ule uliowahi kuona au kusoma au kusikia; na mifano yake katika sehemu mbalimbali duniani.

Hapa mwandishi hafungwi tu kwenye maelekezo ya mhariri kutoka chombo chake.

Ukitaka unaweza kusema, kwa kuelekezwa kufanya jambo moja, anakuwa ameachwa huru kuona kipi anachoweza kuripoti au kujadili.

Rejea kwenye maeneo manane yenye vipengele 106 tuliyojadili katika makala ya pili. Eneo la kwanza linasema: “Iwapo kivuko kimeelezwa na kufafanuliwa – jina lake na kiini, umri, uwezo (kilitoka wapi, kiliundwa na nani na utumikaji wake); matengenezo na ukarabati; hali yake hadi kinazama na sura yake (picha).”

Katika eneo hili kuna vipengele 12. Mwandishi anaweza kuvigusa vyote katika makala moja.

Lakini aweza pia kugusa vichache anavyoona vinakidhi matakwa yake au yale ya mhariri au chombo chake cha habari.

Tumeona kuwa mbali na kutumwa, mwandishi ana utashi binafsi wa kipi kingine anaweza kukiandika.

Kwa mfano huu, ina maana kuwa mwandishi amezama katika kisima cha taarifa na kazi yake ni kuchukua hili na kuacha lile.

Kwa kila moja analoamua kuandika juu yake, mwandishi atalazimika kufanya uchunguzi.

Chukua sehemu ya mwanzo ya eneo la kwanza lililonukuliwa hapo juu: jina lake (kivuko) na kiini, umri, uwezo, (kilitoka wapi, kiliundwa na nani na utumikaji wake).

Mwandishi mtotozi na anayejua kuumba, ataanza kwa kujiuliza iwapo kulikuwa na haja ya kivuko.

Kama ilikuwepo, wasomaji, wasikilizaji na watazamaji televisheni wanatarajia kuona haja hiyo ikifafanuliwa.

Njia bora ya kuifafanua ni kueleza ukubwa wa idadi ya wasafiri (kutoka huku kwenda kule na kurudi); ulazima wa safari, wingi wa safari, ongezeko la ulazima na wingi wa wasafiri na umuhimu wa chombo kikubwa cha usafiri.

Hapa lazima hadhira yako ielezwe mfumo wa usafiri uliokuwepo kabla ya mahitaji mapya na makubwa.

Mwandishi aipe hadhira yake wingi wa watu waliokuwa wakisafiri, safari (ngapi) zilizokuwa zikifanywa, mizigo iliyokuwa ikisombwa, biashara (ukubwa – takwimu kama zipo) iliyokuwa ikifanywa kati na baina ya vituo ambako kivuko kilitiananga.

Maelezo haya yaliyosukwa katika lugha hai ya mwandishi anayetambua uzito wa kilichotokea, yanatosha kutoa mwanga juu ya wakazi, uchumi wa eneo husika, umuhimu wa kivuko, janga lililowakumba wakazi maeneo hayo na uhalali wa kilio chao.

Katika muktadha huu na katika andishi moja, mwandishi ataleta kiu ya hadhira yake ya kujua maisha kabla ya kivuko, wakati wa kivuko, umuhimu wa kivuko, matarajio ya wadau na msiba uliowakumba.

Mwandishi atakata kiu ya wadau wake kwa kuonyesha umuhimu wa chombo kipya katika mazingira ya wingi wa abiria, wingi wa safari, ukubwa wa biashara visiwani na furaha ya jamii.