Tujipange kudhibiti madhara ya radi shuleni

Muktasari:

  • Wanafunzi hao 14 kati yao na mwalimu mmoja waliruhusiwa jana kurudi nyumbani.

Juzi wanafunzi sita wa Shule ya Msingi ya Emaco Vision mkoani Geita walifariki dunia baada ya kupigwa na radi. Wenzao 21 na walimu wawili walijeruhiwa na kulazwa hospitali.

Wanafunzi hao 14 kati yao na mwalimu mmoja waliruhusiwa jana kurudi nyumbani.

Kutokana na tukio hilo wanafunzi wengi wamepata majeraha ya miguuni na shingoni. Mwalimu mmoja amejeruhiwa zaidi baada ya kuungua sehemu kubwa ya mwili wake na bado anaendelea kupatiwa matibabu.

Shule hiyo imesitisha kufundisha kwa muda na masomo yataendelea Jumatatu, Oktoba 22.

Hili si tukio la kwanza kwa radi kupiga wanafunzi na hata kusababisha vifo. Matukio kama haya ni ya kawaida katika mikoa mingi hasa ya Kanda ya Ziwa inayohusisha Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Kigoma na hata Rukwa. Pia mikoa mingine huyapata mara chache.

Katika matukio mengi ya namna hiyo, si wanafunzi tu ambao hupata madhara, bali hata watu wengine, mifugo, nyumba na mazao pia hukumbwa na kadhia hiyo.

Pamoja na madhara hayo si watu wote wenye uwezo wa kufahamu radi ni kitu gani na hutokeaje, na ndiyo maana wengine huihusisha na masuala ya ushirikina, wakati ni tukio la kisayansi ambalo linaweza kufanyiwa kazi na kupunguza madhara.

Kisayansi radi ni mwanga mkali kutoka angani ambao hutokana na msuguano ndani ya mawingu ya kati na kusababisha cheche za umeme na sauti za vishindo, na hatimaye moto ambao husababisha madhara au hata vifo.

Katika msuguano wa mawingu hayo nguvu za umeme huzalishwa kuanza kutafuta njia rahisi ya kuzifikisha ardhini. Hapo ndipo kitu chochote ambacho hukutwa ardhini na chenye uwezo wa kupitisha nguvu hizo kama mtu, mti, jengo, mnara au nyaya za umeme hutumika. Hilo ndilo tukio la kupigwa na radi. Pamoja na ushauri wa wataalamu kwamba radi zinapoanza ingia ndani katika nyumba imara kujihifadhi au unapokuwa ndani epuka maji ya bomba au kutumia simu za mezani na redio kwa kuwa umeme unaweza kusafiri kupitia mabomba au nyaya za simu na mawimbi, bado kuna njia nyingine za kisayansi zinazoshauriwa.

Zaidi wanashauri kwamba wakati wa mvua hizo chomoa vitu vya umeme, ukiwa kwenye boti au unaogelea nenda nchi kavu na tafuta hifadhi au ingia kwenye gari, usiguse kitu chochote cha chuma na epuka barabara zenye madimbwi.

Pamoja na hayo, ipo mitego ya radi ambayo huwekwa juu ya majengo hasa maghorofa na mengine ya umma kama makanisa na misikiti.

Mitego hii ambayo ni kipande cha chuma au waya, huwekwa juu ya majengo ili ‘kudaka’ wingu la radi na kusafirisha umeme wake bila madhara hadi ardhini.

Shule zote za msingi na sekondari na hata vyuo ni muhimu kuwa na mitego hii kwa kuwa mbali na kuwa na idadi kubwa ya watu, pia nyingi hujengwa mahali pa wazi ambapo huwa rahisi kwa wingu la radi kuzifikia moja kwa moja bila kizuizi.

Hivyo, ni vyema utaratibu ukafanyika ili kuweka mitego hii kwenye shule kuwezesha kuepuka madhara zaidi kwa watoto.

Hata hivyo, lazima pia liwepo angalizo kwa kuwa hata katika majengo ilipowekwa mitego hiyo watu wenye nia mbaya huing’oa na kutoweka nayo.