MAONI: Tunataka kuona nidhamu ikianzia kwenye usajili

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa mchakato wa usajili huo ambao msimu huu umeelezwa kutumia mfumo mpya wa usajili uitwao TFF FIFA Connect, baada ya Dirisha kufungwa kutakuwa na wiki moja ya pingamizi kuanzia Julai 27 na baada ya hapo kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji itakutana kwa ajili ya kupitisha majina ya wachezaji waliosajiliwa.

Siku chache zilizopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilituma ujumbe kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na bila shaka, kwenye vyombo vya habari likizikumbusha klabu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili kuwa dirisha la usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa 2018/2019 lililofunguliwa Juni 15 litafungwa Julai 26.

Kwa mujibu wa mchakato wa usajili huo ambao msimu huu umeelezwa kutumia mfumo mpya wa usajili uitwao TFF FIFA Connect, baada ya Dirisha kufungwa kutakuwa na wiki moja ya pingamizi kuanzia Julai 27 na baada ya hapo kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji itakutana kwa ajili ya kupitisha majina ya wachezaji waliosajiliwa.

Ili kuhakikisha kuwa hakuna timu inayoachwa ikishangaa kuhusu mfumo huo, Shirikisho hilo lilitangaza utoaji wa mafunzo ya jinsi ya kutumia mfumo huo mpya wa usajili kwa klabu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili.

Msimu huu utakuwa tofauti na ule uliopita kwani idadi ya timu zinazoshiriki zimeongezeka kutoka 16 hadi 20 na kwa maana hiyo upya wa mfumo na wingi wa klabu shiriki ni changamoto zinazotarajiwa kujitokeza kuelekea msimu ujao.

Kwa sababu hiyo na kwa kurejea matukio kadhaa katika kipindi kama hiki cha usajili, tunaungana na TFF kuzikumbusha timu zote zenye wajibu wa kufanya usajili kuhakikisha zinafuata sio tu sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, bali na muda uliotajwa ambao ni Julai 26 na si vinginevyo.

Yapo matukio mengi yaliyojitokeza katika kipindi kama hiki kwa timu kushindwa kuendana na tarehe iliyopangwa na kusababisha aibu na usumbufu mkubwa.

Licha ya kuwapo kwa taratibu zilizo wazi na zinazoeleweka kwa wahusika wote, tumeshuhudia baadhi ya wachezaji wakisajiliwa na klabu zaidi ya moja lakini pia muda wa kukamilisha ukimalizika bila matakwa hayo ya kisheria za soka yakitekelezwa.

Ushauri wetu wetu kwa TFF ni kuwa wakali katika msimu huu na kutokubali kuyumbishwa na baadhi ya klabu ambazo zitafanya uzembe wa kukamilisha wajibu wake wa kufanya usajili.

Hatutaki kusikia TFF ikiomba muda kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (TFF) kwamba liongezewe hata saa moja kukamilisha kazi hiyo. Wahenga walinena, kutenda kosa si kosa ila kurudia kosa. Tusirejee makosa kama haya tena.

Soka ni mchezo wa nidhamu, unahitaji watu wanaofuata maadili ndani nan je ya uwanja. Kwa maana hiyo, kutokuwa na nidhamu katika masuala ya msingi kama haya ni mwanzo wa klabu zetu na hata timu zetu za Taifa kushindwa kufanya vizuri.

Tunataka kusikia hatua zikichukuliwa bila kuangalia sura kwa klabu au mchezaji atakayebainika kujisajili katika zaidi ya klabu moja ilhali anafahamu.

Lakini pia hatutaki kusikia klabu iliyoshindwa kukamilisha usajili wake kwa wakati ikiruhusiwa kufanya kazi hiyo nje ya wakati kwa visingizio ambavyo aghalabu havina kichwa wala miguu.

Tukiwa makini katika masuala ya msingi kama haya, itakuwa ndiyo chachu ya kufanya vyema katika mambo mengine makubwa zaidi hususan michuano ya kimataifa.