Tunataraji kuona ndege nyingi zaidi Dodoma

Muktasari:

  • Ndege hiyo aina ya Bombadier Q400 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) iliwasili Dodoma saa 1:00 asubuhi ikitokea Dar es Salaam ikiashiria kuimarika kwa safari ya kuugeuza mkoa huo kuwa makao makuu ya Serikali na kituo kikubwa cha kibiashara.
  • Tunapongeza jitihada hizi za ATCL na Serikali kwa ujumla katika kutimiza ndoto ya kihistoria ya kuifanya Dodoma makao makuu ya nchi ambao ulitangazwa kwa mara ya kwanza na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1973.

Kwa mara ya kwanza katika historia, ndege ya kwanza ya abiria ilitua juzi mjini Dodoma ikiwa na abiria 76, akiwamo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Ndege hiyo aina ya Bombadier Q400 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) iliwasili Dodoma saa 1:00 asubuhi ikitokea Dar es Salaam ikiashiria kuimarika kwa safari ya kuugeuza mkoa huo kuwa makao makuu ya Serikali na kituo kikubwa cha kibiashara.

Tunapongeza jitihada hizi za ATCL na Serikali kwa ujumla katika kutimiza ndoto ya kihistoria ya kuifanya Dodoma makao makuu ya nchi ambao ulitangazwa kwa mara ya kwanza na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1973.

Tunapongeza kwa sababu moja ya sifa za kuufanya mji wenye hadhi ya makao makuu ya nchi ni upatikanaji wa huduma za usafiri hususani wa anga. Kwa miaka nenda rudi, licha ya Dodoma kuwa na shughuli nyingi za kitaifa ikiwamo mikutano ya Bunge na ile ya chama tawala (CCM), huduma ya usafiri wa anga ilikuwa kitendawili na maelfu ya watu wamekuwa wakilazimika kutegemea aina mbili tu usafiri, barabara na reli.

Lakini, ndege hiyo iliyotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma ikiwa ni dakika 35 baada ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, inamaanisha kwamba si mji huo pekee ambao sasa utakuwa ukifikika kirahisi, bali miji yote ya Kanda ya Kati.

Kama Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alivyokaririwa akisema kwamba safari hiyo haikuja kwa bahati mbaya, bali ni mipango iliyokuwa imewekwa ambayo imefanikiwa, tunayashauri mashirika mengine ya ndege kuanza kuitupia jicho Dodoma kama sehemu mahsusi ya uwekezaji katika biashara ya anga.

Upanuzi wa uwanja ulioanza mwaka jana sasa unaruhusu ndege kubwa kama Bombadier Q400, Gulfstream 550 na ATR 72 kutua kwenye uwanja huo wa makao makuu ya nchi hivyo ni jukumu la mashirika yenye ndege hizo kuchangamkia fursa hiyo.

Tunaamini kwamba kuongezeka kwa mashirika yenye kufanya safari katika mji huo kutasaidia si tu uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo lakini pia unafuu wa bei ambao utawashawishi abiria kutumia zaidi ndege na kukwepa kusafiri umbali mrefu wa kilomita zaidi ya 500 kwa barabara au reli.

Tutaamini mashirika mengi zaidi yakijitokeza, idadi ya abiria itaongezeka pia na bei ya sasa ya Sh165,000 kwa safari kati ya Dodoma na Dar es Salaam huenda ikapungua zaidi kutokana na ushindani wa kibiashara.

Mfano mzuri ni wa bei ya huduma hiyo ulitolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliyekuwa mmoja wa abiria wa safari hiyo ya kwanza ya ATCL Dodoma. Alisema ndege hiyo ambayo inafika mpaka mkoani Kigoma kupitia Dodoma imeleta unafuu wa nauli kwa wananchi wa Kigoma ambao usafiri ulikuwa ni wa tabu na nauli kuwa kubwa kwani walikuwa wanalipa Sh1.4 milioni kwenda na kurudi Kigoma kutoka Dar es Salaam lakini sasa wanalipa Sh600,000 pekee.

Tunaamini kwamba kauli ya mkurugenzi mkuu wa ATCL kwamba safari hiyo haikuja kwa bahati mbaya, bali ni mipango iliyokuwa imewekwa ambayo imefanikiwa na ile ya Waziri Mkuu Majaliwa kwamba shirika hilo linazidi kutatua changamoto zilizopo ili kufika maeneo yote kwa usafiri wa ndege wa gharama nafuu, yatazingatiwa na kuchukuliwa na mashirika mengine kama changamoto ya ushindani.