DARUBINI YA MTATIRO : Tunayo mahakama huru inayotenda haki?

Muktasari:

  • Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alishtakiwa kwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma, kwa kukarabati jumba lake la kifahari, kesi ikaenda mahakamani na kupokelewa, hakukuwa na mizengwe ya ofisi ya mwendesha mashtaka wa nchi hiyo wala Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ilivyo kwa Tanzania pale ambao kigogo anashtakiwa na mtu wa kawaida au bila ridhaa ya Serikali.

Maneno ya kichwa cha habari yanaweza kuzua mjadala mkubwa, lakini kabla hatujaenda hebu tuangalie mfano mmoja kuhusu mahakama. Nchini Afrika Kusini, kikatiba mtu yeyote anaweza kumshitaki rais muda wowote ambao yuko madarakani (hiyo ni tofauti na Katiba ya Tanzania ambapo rais hashtakiwi anapokuwa madarakani kisheria na hata anapostaafu ni vigumu kumshitaki kutokana na urasimu uliopo).

Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alishtakiwa kwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma, kwa kukarabati jumba lake la kifahari, kesi ikaenda mahakamani na kupokelewa, hakukuwa na mizengwe ya ofisi ya mwendesha mashtaka wa nchi hiyo wala Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ilivyo kwa Tanzania pale ambao kigogo anashtakiwa na mtu wa kawaida au bila ridhaa ya Serikali.

Kesi ikaunguruma na bila kujali kuwa Zuma ndiye bosi wa nchi, Mahakama ikafanya kazi yake, ikamkuta na hatia.

Uthibitisho wa mahakama ukalifanya Bunge la Afrika Kusini lipokee kijiti chake, likaanza mchakato wa kumsulubu Zuma ili aondoke madarakani kikatiba, chama cha ANC ambacho kina wabunge wengi kikafanya michezo yake na kumtetea kiongozi wao wa Serikali, Zuma akaponea chupuchupu kwenye kuondolewa wadhifa wake.

Kilichomsaidia Zuma siyo ukuu na ukubwa wake, ni wanasiasa wenzake wa chama chake kupitia Bunge ndiyo walichukua jukumu hilo.

Hiyo ina maana kuwa kwa nchi kama Afrika Kusini, mtawala hawezi kuitegemea mahakama kupata ulinzi baada ya kufanya makosa.

Kilichotendwa na mahakama ya Afrika Kusini kwa Zuma huwa ni kipimo cha kipekee cha uhuru wa mahakama, ukuu wa mahakama, utendaji haki wa mahakama na ushahidi tosha kuwa Serikali haiingilii mahakama fulani.

Dhana ya uhuru wa mahakama kama mhimili muhimu wa dola ni kuhakikisha inatenda haki na haki hiyo inaonekana kuwa imetendeka, mahakama huru husimamia misingi ya sheria zake (tena sheria zilizo za haki).

Mahakama huru duniani mara zote huzitengua sheria mbovu zilizotungwa na bunge, yaani (mfano) ni kama Bunge letu lilivyopitisha sheria ya makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 (The Cyber Crime Act) na hata mtoto mdogo akiisoma sheria ile siyo tu anatambua nia ‘ovu’ ya walioitunga kupora uhuru wa kikatiba wa wananchi kutoa maoni yao, bali ataona kuwa lengo kubwa zaidi ni Serikali kuwanyamazisha raia wake.

Kwa sheria kama hii ya Makosa ya Mtandao, kwa nchi kama Afrika Kusini, ikiwa Serikali ingeliitumia hasa katika vipengele vinavyovunja haki za kikatiba za wananchi, mahakama ya Afrika Kusini ingelitoa ushindi kwa raia anayeshtakiwa na ingelitangaza sheria hiyo kuwa mbaya (bad law).

Hili ni eneo lingine ambalo pia mahakama yoyote huonyesha namna gani inafanya kazi zake bila kukubali kuingiliwa na vyombo vingine vya dola, kwamba mahakama au jaji anaweza kutoa hukumu na kueleza kuwa sheria inayomshitaki mtuhumiwa fulani iko kinyume na Katiba ya nchi au siyo sheria nzuri.

Nimeeleza vigezo viwili vinavyoweza kutufanya tutambue ikiwa mahakama yetu iko huru au la. Moja ni vile ambavyo mahakama inaweza kusimamia kesi kubwa zinawahusu hata wakuu wa dola bila hofu na zikatenda haki bila kujali vyeo na ukuu wao.

Pili, ni pale ambapo mahakama inaweza kutoka kadharani na kusema kuwa sheria fulani iliyotungwa na Bunge au iliyotumika kumshitaki mtu fulani ni sheria mbaya.

Kwa sababu dhana ya uwepo wa mahakama ni kuhakikisha jamii inapata haki na haki hiyo inaonekana, wanaopewa dhamana ya kuongoza mahakama kwa ngazi mbalimbali hudhani kuwa kwa sababu wanajamii wengi hawajui sheria, lolote ambalo mahakama itaamua jamii itapokea.

Siyo sahihi! Jamii ipo kwanza ili sheria ziwepo, sheria hazipo kwanza ili jamii iwepo. Ndiyo maana mara nyingi tunashuhudia wananchi na jamii ikiguna kwa sauti kubwa pale ambapo mahakama inafanya maamuzi fulani.

Ugunaji huo una maana kuwa wananchi wa kawaida hawaridhishwi na mwenendo wa utendaji wa mahakama zao, hawaridhishwi na kile kilichotokea kwa sababu wao kama jamii walitegemea jambo fulani litokee, haki fulani ipatikane.

Mahakama zetu kama mhimili wa dola lazima zianze pia zenyewe kuamka na kuionyesha jamii kuwa haziyumbi hata aje nani pale ambapo kuna haki au haki imeporwa. Mahakama zitambue kuwa zipo ili kuitumikia jamii na siyo jamii kuzitumikia mahakama na sheria.

Ili jamii yoyote iwe na amani lazima haki itendeke kwanza na ionekane inatendeka. Mahakama inayo kazi ya kipekee ya kulinda amani katika jamii.

Kila mara mahakama ikitenda kwa weledi, kwa uwezo wake wote na ikakidhi mahitaji ya jamii katika kutenda haki, amani itakuwa siyo jambo la kujadilika.

Kila mara mahakama ikiacha misingi yake ikaungana na wapora haki, ikapindisha uamuzi ili kuwalinda wakubwa na wenye fedha jamii haiwezi kuwa na amani hata kidogo.

Kumbe basi, mahakama ikiwa ndiyo msingi wa haki inayotendwa na kuonekana, haki hiyo itaifanya jamii nzima ione inatendewa vyema na suala la kujadili umuhimu wa amani halitakuwapo.

Mahakama yetu ya Tanzania iendelee kujifunza kwa mahakama za nchi nyingine za Kiafrika ambazo zimepiga hatua.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, mtafiti na mwanasheria Simu; +255787536759/ barua pepe; [email protected]/ tovuti; juliusmtatiro.com.