Tusherehekee Iddi El Fitri tukiendeleza matendo mema

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa dini hiyo, waumini walitumia kipindi cha Mfungo wa Ramadhani kuongeza bidii ya kumcha Mwenyezi Mungu, jambo ambalo ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu.

Waislamu nchini na duniani kote jana waliungana kusherehekea sikukuu ya kuadhimisha sikukuu ya Iddi El Fitri baada ya kumalizika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Kwa mujibu wa dini hiyo, waumini walitumia kipindi cha Mfungo wa Ramadhani kuongeza bidii ya kumcha Mwenyezi Mungu, jambo ambalo ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu.

Ndani ya Ramadhani, Waislamu walichukua ahadi kwa ajili kutekeleza ibada ya funga kwa kujinyima mambo mbalimbali waliyohalalishiwa, ikiwa ni pamoja na kula, kunywa au makutano ya wanandoa mchana wa Ramadhani.

Kuanzia jana wameruhusiwa, lakini kukiwa na mipaka.

Hivyo wale ambao watajipa mamlaka na uhuru kupita kiasi na kusahau mipaka ya Mwenyezi Mungu, imani inatuelekeza kuwa mwenyewe anawaona na anayajua yaliyomo ndani ya mioyo yao.

Tangu juzi ulipotangazwa mwandamo wa mwezi, waumini wa dini hiyo wamekuwa wakijumuika na ndugu jamaa na marafiki zao kula na kunywa majumbani na katika sehemu maalumu, na kama ilivyo ada kwa utulivu bila kufanya mambo ya kuwabughudhi, kuwakera au kuhatarisha maisha ya wengine.

Ni matarajio yetu kwamba yale matendo mema ambayo tumekuwa tukiyasimamia wakati wa Ramadhani tutayaendeleza kwa kuwa ndiyo msingi wa utu na ubinadamu wetu.

Hatutarajii baada ya kipindi hicho kuibuka watu kufanya vitendo visivyoifurahisha jamii kama vya ufuska, ulevi, ugomvi na vingine ambavyo haviendani na mafunzo yaliyokuwa yakitolewa katika Mwezi wa Ramadhani.

Tunapenda kutumia fursa hii kuwataka wananchi kujiepusha na vitendo viovu katika siku hizi tunapoadhimisha na nyingine za usoni ili tuweze kuwa na jamii inayoishi kwa amani na kamwe asiwepo mtu wa kuvuruga furaha za watu na kuharibu siku waliyoisubiri kwa hamu kubwa.

Ni matarajio yetu kwamba hata baada ya mfungo, waumini wa Kiislamu wataendelea kuwa watulivu na wenye maadili mema kama walivyokuwa na kuyaishi mafunzo na mawaidha waliyopata katika kipindi cha Ramadhani.

Huo ndiyo msingi wa sherehe iliyoanza jana ambayo furaha yake huambatana na kuwatembelea wagonjwa na kuwasaidia watu wenye matatizo mbalimbali ya kijamii ili nao wajisikie furaha kama wengine.

Hata kwa Watanzania ambao si Waislamu, tunatarajia kuwaona wakiungana na wenzao katika kuienzi amani ya nchi, hivyo kulinda utamaduni wetu wa kuishi bila kubughudhiana kama Watanzania.

Katika kipindi hiki ipo kila sababu na haja ya kumuomba Mwenyezi Mungu azipe nguvu na imani nafsi za kila mtu kuepuka fitna, maovu, husda, ukatili na mabalaa mbalimbali ya nyuma na mbele yao.

Kama tulivyotangulia kusema, siku ya Idd ni siku ya kuwaangalia kwa jicho la huruma wagonjwa waliomo majumbani na hata hospitalini, wafungwa magerezani kwa kuwatembelea na kuwasaidia kwa kila hali sambamba na kuwaombea dua ya kuwatakia afya njema, ili nao wamshukuru Mwenyezi Mungu na wajione ni sehemu muhimu katika sherehe hii.

Tunawasihi Waislamu wote na hata wasiokuwa waumini wa dini hiyo kuyazingatia mawaidha yote yaliyotolewa na viongozi wa dini katika swala na Baraza la Idd, hasa kwa kuwa yalikuwa yanalenga katika kukumbushana, kuhamasishana, kuelekezana na kusisitizana kuendeleza utiifu, wema, ukarimu, upendo na heshima iliyojengwa ndani ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani.