Tusibembelezane hatua zichukuliwe ukeketaji ni hatari

Muktasari:

  • Licha ya juhudi kufuanyika, lakini bado baadhi ya watu wanaendelea kuikumbatia mila hiyo potofu yenye madhara makubwa kwa afya ya wanawake na watoto wa kike.

Siyo jambo geni masikioni mwa watu. Japo awali ukeketaji ulionekana hauna madhara lakini kadiri muda ulivyozidi kusogea na kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia na utandawazi, ndipo madhara yakaanza kuonekana.

Licha ya juhudi kufuanyika, lakini bado baadhi ya watu wanaendelea kuikumbatia mila hiyo potofu yenye madhara makubwa kwa afya ya wanawake na watoto wa kike.

Februali 6, kila mwaka, imetengwa maalumu kwa ajili ya kupinga mila hiyo kwa Serikali na wadau mbalimbali kutoa elimu ya kuipinga na kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya milo hiyo.

Hata hivyo, licha ya elimu kuendelea kutolewa bado kuna watu hawajapata uelewa wa kutosha.

Asilimia kubwa ya wanaohudhuria matamasha ya kupinga ukeketaji wameendelea kuuliza maswali kadhaa kwa wataalamu wa afya wakitaka majibu sahihi ya kwanini mila hiyo inapingwa.

Nikiwa mtaalamu wa afya, kupitia makala haya ninayatolea majibu baadhi ya maswali hayo.

Wapo wanaohoji ukeketaji ni nini?

Kwa kifupi, ukeketaji ni kitendo kinachohusisha kuondoa kwa baadhi ya sehemu ya nje ya viungo vya uzazi vya mwanamke.

Inakadiriwa zaidi ya wanawake milioni 200 duiniani kote wamefanyiwa ukeketaji na hasa katika nchi za kiafrika na jamii za kiarabu.

Na utamaduni huu wanafanyiwa kwa wasichana na wanawake wenye umri tofauti kulingana na utamaduni wa jamii husika.

Kwa baadhi ya jamii wanafanya kwa watoto wachanga siku chache baada ya kuzaliwa na wengine wanawafanyia wasichana wanapokaribia umri wa kubalehe, kuolewa na wakiwa wajawazito baada tu ya kujifungua.

Utafiti unaonyesha hivi karibuni ukeketaji umekuwa ukifanyika zaidi kwa watoto wa kike wenye umri wa kuanzia 0 hadi 15.

Lakini pia ukeketaji unaweza kufanywa na makundi mengine ya watu wakiwamo waganga wa jadi.

Changamoto kubwa leo hii sio tu kuwalinda wasichana ambao wapo kwenye mazingira hatarishi ya kukeketwa, lakini pia kuhakikisha watoto wadogo wanaozaliwa wanaepushwa na vitendo hivi.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) kwa mwaka 2010 zinaonyesha zaidi ya asilimia 45 ya a wanawake waliokeketwa kwa nchi za Gambia, Mali, Somalia na Uganda walikua chini ya miaka 15.

Kwa nini ukeketaji unafanyika?

Sababu za kuendeleza mila na desturi hizi zimegawanyika katika Nyanja kuu tatu:

Sababu za kihisia: kupitia sababu hii, ukeketaji unafanywa ili kuondoa mapokeo ya kihisa hasa wakati wa kufanya tendo la ndoa.

Kibailojia; mwanamke husisimka na kupokea hisia zote wakati wa tendo la ndoa hasa anapoguswa sehemu zake za siri.

kwa baadhi ya jamii na hasa zile zisizozingatia usawa wa kijinsia na zinazoendekeza mfumo dume, zinadai mwanamke hana haki ya kufurahia tendo la ndoa kama mwanaume.

Hivyo, wanadai kazi ya mwanamke ni kumridhisha mwanaume, lakini pia wanaamini kufanya ukeketaji kunamzuia mwanamke asiwe na hisia zozote kwenye tendo la ndoa na itamfanya atulie kwenye ndoa yake asiwe na uhusiano nje.

Sababu za kijamii na za kiutamaduni:

Baadhi ya watu wanachukulia ukeketaji ni ishara kuwa msichana amekua na sasa anaingia hatua ya utu uzima.

Kwa kufanya hivyo wanamtambulisha kwa jamii sasa anastahili kurithishwa baadhi ya mali ikiwamo ardhi ya kujenga na hata mashamba na kuanzisha himaya yake na familia yake.

Saabu za kijamii na kiuchumi

Baadhi ya jamii na hasa zile ambazo mila na desturi zao ni lazima mwanamke amtegemee mume wake kiuchumi, huwa zinajiwekea utaratibu kuwa mwanamke pekee anayestahili kuolewa ni yule aliyekeketwa.

Wanadai kupitia kuolewa, wazazi wa mwanamke huwa wanatoza mali zinazowanufaisha kiuchumi na mara zote hushunikiza watoto wao wa kike wakeketwe ili wapate mali.

Ni kwa namna gani ukeketaji unawaathiri wasichana na wanawake kiafya

Huenda hili ndilo swali kubwa linalowasumbua wengi. Jamii nyingi bado zimeendelea kujihusisha na vitendo vya ukeketaji bila kujua madhara yake kiafya. Kwa mtazamo wa kimila wanadhani kufanya hivyo wanasaidia wanawake kutulia kwenye ndoa zao.

Hili halina ukweli wowote. Ukeketaji unamuathiri mwanamke kiafya na kisaikolojia.

Na madhara yake ni makubwa zaidi jamii inavyoyachukulia.

Athari za ukeketaji zinaambatana na wingi wa sababu kutegemea na aina ya ukeketaji wenyewe, umahiri wa yule anaekeketa, usafi wa vifaa vinavyotumika kwenye ukeketaji na hali ya afya ya msichana au mwanamke anayekeketwa.

Lakini ijulikane kuwa ukeketaji unaathari kubwa kwa afya ya uzazi ya mwanamke.

Ni madhara yepi ya afya uzazi yanatokana na ukeketaji?

Tafiti mbalimbali zinathibitisha kuwa, ikilinganishwa na idadi ya wanawake ambao hawajafanyiwa ukeketaji, wale waliokeketwa wapo kwenye hatari kubwa ya kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua.

Na upasuaji huo ni ule wa kupasua sehemu ya chini ya uke ili kuongeza njia kwenye mlango wa uzazi, hali inayosababisha atokwe na damu nyingi, hivyo kumlazimu kukaa hospitali kwa muda mrefu kwa ajili ya matibabu.

Ukeketaji upo wa aina ngapi?

Upo wa aina mbalimbali na aina moja wapo ni ile ambayo sehemu ya mashavu ya uke inaunganishwa kwa kushonwa ili kuziba nafasi ya mlango wa uke kwa dhumuni la kumzuia muhusika asijamiiane. Aina hii ya ukeketaji kitaalamu inaitwa ‘infibulation’.

Aina hii inatekelezwa zaidi kwenye nchi za Afrika ya Kaskazini na huhatarisha maisha ya mama wakati wa kujifungua na mara zote husababisha fistula na vifo vingi.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Unicef zinaonyesha nchi zinazoendeleza utamaduni huu ndizo zinaongoza kwa vifo vya watoto na wajawazito wakati wa kujifungua.

Kuna uhusiano kati ya ukeketaji na maambukizi ya virusi vya ukimwi?

Ikumbukwe kuwa ukeketaji ni jambo linalofanywa ili kudumisha mila za jamii fulani, na kwa kiasi kikubwa halizingatii maadili ya kiafya.

Ukeketaji una uhusiano mkubwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwani Kifaa kimoja kinaweza kutumia kukeketa wasichana wengi kwa wakati mmoja bila kufanyiwa usafi jambo ambalo ni hatari kwa maambukizi ya VVU.

Pia kutokana na kuharibiwa kwa ogani za uzazi za mwanamke, mara afanyapo tendo la ndoa ni rahisi kupata michubuko, hali inayotoa mwanya wa kumuweka katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU kirahisi. Hali hiyo pia inatokea wakati wa kujifungua na huweza kusababishia maambukizi mapya kwa mtoto atakayezaliwa.

Ni madhara yapi ya kisaikolojia ya ukeketaji?

Matokeo hasi ya ukeketaji yanaonekana kudumu kwa muda mrefu kwenye akili za wasichana na wanawake waliofanyiwa kitendo hicho.

Ukeketaji unaharibu utu wa mwanamke, mwanamke anaweza kupata msongo wa mawazo ambao kisaikolojia unaweza kumsababishia matatizo ya kitabia ikiwamo kushindwa kujiamini, kupoteza matumaini na imani.

Imeripotiwa wanawake wanaokeketwa wapo kwenye hatari kubwa ya kupata sonona kutokana na ile hali ya kukosa matumaini na kujiona hawana thamani tena baada ya kufanyiwa vitendo vya ukeketaji.