MAONI: Tusishikiwe bango kuweka safi mazingira yetu

Muktasari:

  • Makonda alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na vijana hao waliojitokeza katika usaili wa kuajiriwa ili kusimamia usafi kwa nia ya kuhakikisha wanawawajibisha wachafuzi wa mazingira jijini humo.

Hivi karibuni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliondoa utaratibu wa usafi wa kila Jumamosi uliokuwa unafanyika kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa nne. Badala yake aliunda timu ya vijana wa mgambo na JKT ambao watakuwa wanakagua mazingira na kuwakamata wachafuzi wa mazingira.

Makonda alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na vijana hao waliojitokeza katika usaili wa kuajiriwa ili kusimamia usafi kwa nia ya kuhakikisha wanawawajibisha wachafuzi wa mazingira jijini humo.

Kwa mujibu wa Makonda, suala la wafanyabiashara kufunga maduka siku za Jumamosi hadi saa nne asubuhi sasa halitakuwapo, badala yake watu wote watawajibika kwa usafi katika mazingira yao na watakaokaidi watakamatwa.

Makonda alienda mbali zaidi na kusema kuwa vijana hao pia watakuwa na jukumu la kusimamia kampuni zilizopewa kazi ya usafi kwenye maeneo husika, kuwakamata na kuwatoza faini watupaji wa taka pamoja na kufuatilia kujua kila nyumba inakopeleka taka wanazozalisha majumbani mwao.

Hatua ya Makonda inafuatia Serikali kurasimisha siku ya Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kuwa siku ya usafi kitaifa kupitia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 191 inayosema mtu yeyote anayekaidi kufanya usafi anatozwa faini isiyopungua Sh50,000 au kifungo cha kuanzia miezi mitatu mpaka miaka saba, huku wanaobainika kutupa taka hovyo wakitozwa kiasi cha Sh200,000 papo hapo.

Sheria hiyo iliyotangazwa mwaka 2016 na aliyekuwa naibu waziri katika Ofisi Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina pamoja na mambo mengine, Serikali iliridhia iwe maalumu kwa ajili ya usafi ambapo utekelezaji wake utasimamiwa na viongozi kuanzia ngazi za chini kupitia muongozo wa tangazo la Serikali uliochapishwa katika gazeti namba 139/2016 la Aprili 23, 2016.

Kimsingi, nia hiyo ya Makonda ina lengo zuri kwa kuwa suala la usafi wa mazingira, kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji ni la mtu binafsi bila kujali cheo au nafasi yake katika jamii.

Hata hivyo ni vyema tukiri kuwa ni aibu kwa Watanzania kusubiri kushurutishwa kwa sheria na kushikiwa mtutu wa bunduki ndipo wafanye usafi, badala yake ni jukumu la kila mtu kuwa mlinzi na mwangalizi wa mazingira katika sehemu anayoishi.

Tunaamini kwamba kila mwananchi kwa nafasi yake anao wajibu wa kushiriki kikamilifu kufanya usafi wa mazingira kwenye makazi yake, maeneo ya biashara, taasisi za umma na yale yenye mikusanyiko ya watu mbalimbali kama masoko na minada.

Tunasema ni aibu kwa sababu hakuna asiyefahamu kuwa kuishi katika mazingira machafu kuna athari kubwa kiafya kutokana na kuwa katika tishio la milipuko ya magonjwa ikiwemo kipindupindu, kuhara na matumbo. Kila mwaka watu wengi hukumbwa na magonjwa ya milipuko kutokana na hali isiyoridhisha ya usafi wa mazingira tukichukulia mfano wa mwaka 2017 pekee ambapo Watanzania 196 walipoteza maisha kutokana na kipindupindu.

Takwimu za Wizara ya Afya kwa mwaka huo zinaonyesha idadi hiyo ilitokana na watu 12,222 waliougua ugonjwa huo katika mikoa 20 ya Tanzania.

Ni wakati sasa wa kuchukua hatua na kuacha kuishi kwa mazoea. Watanzania tunapaswa kufanya usafi na kujitengenezea utamaduni wa uwajibikaji binafsi katika kutunza mazingira bila kulazimishwa na Serikali. Tunaamini kuwa kwa kuzingatia usafi, kila Mtanzania bila kujali nafasi yake au ushawishi wake kwenye jamii atatimiza wajibu ili kulinda afya zetu, kupendezesha mazingira na kuondokana na adha ya uchafu katika mazingira yanayomzunguka.

Vilevile Serikali iweke miundombinu itakayotoa fursa kwa uchafu wote kukusanywa na kupelekwa sehemu mahsusi unakopaswa kupelekwa.