Monday, September 11, 2017

Tutegemee mbio pekee Michezo ya Madola?

 

Aprili 8, Tanzania ilipokea Kifimbo cha Malkia ikiwa ni takribani siku 26 baada ya safari yake katika nchi mbalimbali duniani kuzinduliwa na Malkia wa Uingereza Machi 13.

Kifimbo hicho ni kama tarumbeta la kuashiria kuanza kwa Michezo ya Jumuiya ya Madola, ambayo safari hii itafanyika Aprili mwakani mjini Gold Coast, Australia.

Michezo hiyo hushirikisha mataifa yaliyokuwa chini ya utawala wa Waingereza, ikiwemo Tanzania ambayo iliwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza.

Michezo ya Madola, ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne, ni mojawapo ya michezo inayopendwa kwa kuwa hutoa nafasi kwa mataifa kushindana kama sehemu ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki.

Ni michezo inayoshiriki karibu nusu ya nchi zote ulimwenguni na hivyo kuwa na umuhimu mkubwa.

Kwa kuwa mbio za kifimbo hicho zishaanza, maana yake ni kwamba maandalizi kwa Michezo ya Madola itakayofanyika miezi sita kuanzia sasa, yanatakiwa pia kuwa yameshanza.

Itakumbukwa kuwa katika michezo hiyo, Tanzania iliweka historia duniani baada ya mwanariadha wake, Filbert Bayi kuweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500, rekodi iliyodumu kwa muda mrefu.

Bayi, ambaye sasa ni katibu mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), aliweka rekodi hiyomjini Christchurch, New Zealand akitumia dakika 3:32.2 na ilichukua miaka mitano kuvunjwa. Mwingereza Sebastian Coe ndiye aliyeivunja, lakini jina la Bayi linaendelea kukumbukwa duniani kote kama mtu aliyefanya mapinduzi ya ukimbiaji katika mbio hizo za kati.

Hiyo ndiyo rekodi pekee ya dunia katika riadha iliyovunjwa na Mtanzania. Leo hii tunapojiandaa kwa Mchezo ya Madola, suala hilo inabidi liwe akilini mwetu.

Hadi sasa hakuna maandalizi makubwa yanayoonekana kuanza kwa ajili ya kufikia au kukaribia mafanikio ya Bayi kwenye michezo hiyo.

Kuna michezo mingi inayochezwa Tanzania, lakini inaoonekana nguvu kubwa imewekwa katika riadha pekee katika taifa ambalo lina watu takriban milioni 50.

Kama ndio mkakati wa nchi, ni suala jema lakini maandalizi ya kina yaonekani ili muda utakapofika, Watanzania wawe na imani kuwa kuna kitu kinaweza kupatikana.

Hivi sasa, mwanariadha wa mbio ndefu, Alphonce Simbu ndiye pekee anayeonekana kuwapa matumaini Watanzania kuwa anaweza kurejea na chochote baada ya kufanya vizuri katika mbio za ubingwa wa dunia zilizofanyika London.

Simbu pia alishinda mbio za marathoni za India mapema mwaka huu.

Lakini kuna matumaini gani katika mbio za mita 10,000, mita 5,000, mita 800, mita 400 au mita 200? Michezo kama ya kurusha tufe, mkuki, kuruka chini na kuruka kwa upondo imeishia wapi? Hivi ni kweli hatuna wanamichezo wa kuweka kutuwakilisha Michezo ya Madola kwa kushiriki kurusha tufe, mkuki, kisahani, kupokezana vijiti au kuruka kwa upondo?

Chama cha Riadha (AT) kimefanya juhudi gani kuandaa watu kwa ajili ya michezo hiyo mingine? Je, ni busara kuendelea kutegemea mbio pekee katika Michezo ya Madola, Olimpiki na Michezo ya Afrika?

-->