Tuesday, September 12, 2017

Tutumie mtandao kusukuma mbele gurudumu la huduma na maendeleo

 

By Aidan Eyakuze

Dunia inakwenda kwa kasi ya ajabu ya maendeleo ya kiteknolojia. Vifaa vinavyonekana vya kushangaza wakati fulani, ndani ya kipindi kifupi cha mwezi mmoja tu huonekana ni vya kawaida.

Pata picha kama miaka 10 iliyopita ningekueleza kuwa mtu anaweza kubeba kompyuta mfukoni na kuitumia kuongoza safari za kwenda mwezini na kurudi, huku akipiga picha, akizungumza na marafiki kila kona ulimwenguni, kwa hakika ungeniita punguani.

Hivi leo, simu yako ya mkononi ina uwezo mkubwa mara mamilioni kuliko teknolojia za Kimarekani kuhusu masuala ya anga miaka ya 1969.

Cha ajabu pamoja na uwezo mkubwa wa simu uliyonayo, pengine unachokifanya wewe ni kuitumia tu kusoma makala haya au kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa kuwa tunachukulia maendeleo haya kama kitu tu cha kawaida, tunashindwa kutambua umuhimu wa teknolojia hii katika kurahisisha maisha yetu kwa kuifanya Serikali kutoa huduma kwa wananchi kwa wepesi, haraka na kwa unafuu.

Hata ufisadi nao tungeweza kupambana nao kiraisi kwa kutumia teknolojia.

Hivi karibuni nimepata mifano ya namna Serikali inavyotumia teknolojia na kufanya mambo yake kwa uwazi katika kurahisisha maisha yetu.

Takribani miezi mitatu iliyopita niliepukana na usumbufu wa kujua deni langu la kodi ya ardhi.

Naishukuru tovuti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuniwezesha kukokotoa kiasi nilichokuwa nadaiwa na Serikali.

Hapo ndipo niliposema: ‘kwa heri mambo ya kale ya kunifanya nipange foleni kwa muda mrefu katika ofisi za Wizara nikisubiri kulipia kiwanja changu.

Kwa hakika, tovuti hii imetupunguzia maumivu na usumbufu katika suala zima la ulipaji wa kodi ya majengo.

Baadaye Juni, nikabahatika kubaini kuwapo kwa tovuti ya watumishi kupitia Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Tovuti hiyo inawawezesha zaidi ya nusu milioni ya watumishi wa umma kupata taarifa za malipo yao, upandishwaji madaraja, mishahara kwa njia ya mtandao, kuuliza maswali na kuwasilisha malalamiko yao.

Jambo la maana kwa upande wangu kuhusu tovuti hii ni ule ubadilishanaji au upashanaji habari wa taarifa ndani kwa ndani, unaowawezesha watumishi wa umma kubadilishana nafasi zao za kazi.

Kuna tovuti ya wazi ya Serikali (Government Open Data Portal). Hii ina taarifa za kutosha kwa wazazi wanaotaka kufahamu taarifa za uandikishwaji wa wanafunzi, taarifa za walimu, ufuatiliaji wa matokeo ya mitihani na kufahamu uwiano uliopo kati ya walimu na wanafunzi katika shule zote nchini.

Kwa sasa takwimu za elimu zinapatikana kwa wakati. Mathalani, hadi kufikia Julai 31, 2017 taarifa za mwaka 2016 zilikuwa tayari kwenye mtandao.

Tovuti nyingine ni ile ya idara ya Uhamiaji kuhusu uombaji wa hati za kusafiria.

Utaratibu huu wa kisasa unaondoa usumbufu ikiwamo upotezaji wa muda kwa kuharakisha mchakato wa kuomba hati kwa njia ya mtandao.

Kama mdau wa maendeleo, lazima nisifu jitihada hizi za kimaendeleo kwa nchi yangu. Lakini ninapotoa sifa hizi, furaha yangu imeingia dosari.

Kuna maswali mawili nahitaji kuuliza; Je, wananchi wanafahamu jitihada hizi muhimu zinazofanywa na Serikali kwa maendeleo yao? Aidha, ni kwa kiwango gani wananchi wanatumia huduma hizi?

Februari 2017, asasi ya Twaweza ilifanya mahojiano na watu 170 wanaotumia taarifa hizi kutoka serikali za mitaa na asasi za kiraia kuhusu matumizi yao ya tovuti ya wazi ya Serikali.

Utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 94 wanatumia taarifa zinazokusanywa na Serikali katika utaratibu wake wa kazi, kwa ajili ya kuchochea uboreshaji wa utumishi wa umma.

Hata hivyo, wachache kati ya asilimia 40 walisema kuwa wanaifahamu tovuti ya wazi ya Serikali na kati ya watu 170 waliohojiwa ni watu 30 tu (sawa na asilimia 18) ambao walishatumia au kutembelea tovuti hiyo.

Kimsingi, hapa ndipo penye fursa. Mahali ambapo muuza viatu haoni fursa katika jamii ya watembea peku, kwa mwingine hilo ndilo soko lake jipya.

Kati ya Watanzania 10, wanne huwa katika mtandao kwa njia moja ama nyingine. Serikali ya Tanzania inafanya jitihada kubwa kutoa huduma zake kwa wepesi, haraka na unafuu kwa njia ya mtandao.

Hizi ni hatua nzuri za awali na ninatazamia kuona ni jinsi gani huduma hii itapanua wigo kufungua mipaka, ili kufanya huduma zipatikane kwa wananchi wote.

Aidan Eyakuze ni mkurugenzi mtendaji wa Twaweza East Africa anapatikana kwa baruapepe: aeyakuze@twaweza.org

-->