Tuungane kukomesha mauaji na utekaji wa watu ovyo

Muktasari:

Sitaki hata kuwataja waliokumbwa na vifo vya kutisha, bali maeneo ambayo yamekithiri kwa kipindi kirefu ni ya Kibiti mkoani Pwani ambako wengi waliuawa. Wapo waliokatwa kwa mapanga katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mwanza huku wauaji wengine wakiiweka miili ya marehemu kwenye viroba.

Kumekuwapo na matukio ya kutisha yakiwamo ya mauaji ya kikatili kwa watu mbalimbali wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara. Hata kupotea kwa mwandishi wa kujitegemea wa gazeti hili, Azory Gwanda ni kielelezo kuwa hali si shwari.

Sitaki hata kuwataja waliokumbwa na vifo vya kutisha, bali maeneo ambayo yamekithiri kwa kipindi kirefu ni ya Kibiti mkoani Pwani ambako wengi waliuawa. Wapo waliokatwa kwa mapanga katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mwanza huku wauaji wengine wakiiweka miili ya marehemu kwenye viroba.

Hili linasikitisha na ni vigumu kuamini kama wanaofanya hayo ni Watanzania. Je, ni kweli Watanzania wanafikia kumuua mtu kwa kumkatakata mapanga na hatimaye kumuweka kwenye kiroba?

Ni kweli wapo watu wanaodaiwa kuwa na hasira ambao wanapiga na kuwachoma moto watuhumiwa wanaokutwa wakifanya matukio mabaya dhidi ya jamii kama vile wizi, uporaji, lakini mauaji ya viongozi katika jamii ni ya kushtua zaidi.

Watendao haya wanamkosea Mungu na kwenda kinyume na sheria za nchi, licha ya kujitetea kwamba wanapandwa na hasira. Wengi sasa wanaamini kwamba mauaji ya kikatili yanayofanyika yanatekelezwa na watu waliojipanga Ni kweli karibu nchi zote zimegubikwa na matukio ya mauaji katika vipindi tofauti tofauti. Hata hapa nchini matukio ya mauaji yamekuwapo miaka karibu yote na kwa sababu tofauti.

Kwa mfano, mikoa ya Kanda ya Ziwa iliwahi kukumbwa na mauaji ya vikongwe, ambapo uchunguzi wa vyombo va dola ulionyesha chanzo ni imani za kishirikina.

Wauaji waliamini vifo vya watu wanaougua magonjwa mbalimbali vinasababishwa na vikongwe wenye macho mekundu waliodaiwa kuwa ni wachawi.

Hali kadhalika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nayo ilivuma kwa mauaji ya watu kwa ajili ya kutafuta utajiri kwa imani za kishirikina.

Pia ipo mikoa ambayo watu wenye vipara waliuawa kwa imani za kishirikina, lakini mambo hayo yote yaligundulika kuwa chanzo kikuu ni ujinga.

Hivyo asasi za kijamii kwa kushirikiana na vyombo vya dola zilifanikiwa kutoa elimu kwa wajinga hao na hatimaye mauaji yalipungua.

Miaka hiyo Polisi walieleza wazi kwamba baadhi ya watuhumiwa walisema waliua watu baada ya kualikwa na kupewa fedha kwa kazi hiyo.

Ukatili unaoendelea sasa unatokana na nini? Je, ni sababu za kisiasa, kijamii, wivu ujinga au ni nini?

Kama mauaji ni ya kisiasa, kuna masIlahi gani ya kumuua mtendaji wa mtaa, diwani wa kata au mwenyekiti wa mtaa ambaye kisiasa bado hajakomaa na wala hana uwezo wa kutikisa wilaya wala mkoa?

Hata kama ni sababu ni za kisiasa kupitia uchaguzi, tukumbuke katika uchaguzi wapo wanaopata na kukosa, hivyo kama ulikosa au ulipata unawajibika kujipanga kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

Kama mauaji ni ya wivu, je, jambo gani kubwa amelifanya mwenzako kiasi cha kuamua kumuua kama hayawani mwituni? Bila shaka wote tunajua kwamba kuua binadamu mwenzako ni dhambi, hivyo hata kama mhusika kabla ya kifo chake alifanya mapenzi na mke au mume wa watu au kama nao waliwahi kuua au kudhulumu, kinachotakiwa ni kushtakiwa.

Kwa kawaida kuua kunaongeza mauaji, kwani kama ni kulipiza kisasi, ukoo wa marehemu nao unaweza kujipanga kwa lolote, hivyo ipo haja kwa watu kujiepusha kabisa na masuala ya mauaji. Viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya dini na wananchi tuungane kuzuia mauaji bila ya kumlau mtu.

0767-338897