UCHAMBUZI: Kuzagaa wamachinga ni watendaji kukosa ubunifu

Mara kadhaa Rais John Magufuli ameweka wazi kwamba wamachinga wasibughudhiwe badala yake waachwe wafanye shughuli zao maeneo ya mijini kama wanavyofanya wafanyabiashara wengine.

Pamoja na kauli hiyo, kiongozi huyo amekuwa akiwaeleza watendaji wa mamlaka za miji, majiji na manispaa wawaandalie mazingira bora ya kufanya biashara zao badala ya kuwafukuza na kuwanyang’anya bidhaa zao.

Kauli yake ya “sitaki kuona watu hawa wakibughudhiwa maana na wao wanatakiwa kupata riziki, waandalieni mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya biashara zao maana hakuna mwenye hati ya miji” imekuwa ikijirudia kila mara masikioni mwao.

Nikitumia mfano wa Mkoa wa Mwanza, awali viongozi walitenga maeneo kwa ajili ya wamachinga kufanya biashara zao ambayo baadaye yalionekana si rafiki na hakukuwa na miundombinu kama vyoo.

Sitaki kuamini kwamba kauli ya kiongozi huyu ya kutaka kundi hilo liandaliwe mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao kama haikueleweka kwa watendaji au ni kukosa kwao ubunifu.

Kuna kipindi ilifika hatua Rais Magufuli akiwa Mwanza akasema kama watendaji wameshindwa kuwaandalia mazingira mazuri wamachinga wanaweza kutenga moja ya barabara za mji huo kwa ajili yao ili waitumie kufanyia biashara zao kila mwisho wa wiki. Yote hayo ni kuangalia namna ya kuwaweka pamoja, lakini bado viongozi wetu hawaoni cha kufanya.

Kwa sasa katika miji mikubwa kama Arusha, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza wamachinga wametumia mwanya huo kupanga bidhaa zao pembezoni barabarani na kusababisha usumbufu kwa wapita njia. Tena kwa kiburi hichohicho, mpita njia akipita na kugusa bidhaa kwa mguu husindikizwa na matusi na wengine hudiriki kuwapiga kwa kuwa tu wamekanyaga bidhaa zao. Kero hiyo siyo tu kwa watembea kwa miguu maana hata kwa magari na vyombo vingine vya usafiri hupata shida kupita kutokana na mpangilio mbovu wa biashara hizo.

Mathalan katika barabara za Kenyatta, Nyerere, Pamba, Stesheni, Mitimirefu na nyingine za Mwanza ni kero na hazipitiki kwa raha kutokana na kufurika wamachinga.

Kama hiyo haitoshi hali hiyo pia ni hatari kwao wenyewe, maana yapo magari yanayoweza kufeli breki, lakini pia kutokana na ufinyu wa barabara hizo yanaweza kupinduka na kusababisha athari zaidi.

Haya yote yanafanyika watendaji wakiwa wanaona na wala hawachukui hatua za kubuni njia bora za kuendesha shughuli hizo. Sasa sijui tuseme kwamba ni mgomo baridi wanasubiri nini kitatokea baada ya mipango yao ya awali kukataliwa na mkuu wa nchi au lengo ni nini. Kulingana na hali ilivyo sasa jinsi bidhaa zinavyopangwa lolote linaweza kutokea.

Huenda Rais aliwatega ili kuona nani anaweza kuwa mbunifu zaidi badala ya kusubiri kila kitu kuelekezwa ambapo watendaji wengi wanaelekeza nguvu nyingi katika kuzungumza nadharia bila vitendo. Kukosekana mpangilio maalumu wa bidhaa mitaani imekuwa kichaka pia cha hata wafanyabiashara wa maduka makubwa kuondoa bidhaa zao na kuzipanga nje wakitumia kivuli cha wamachinga.

Pengine kauli ya Rais inaweza kuwa mtego kwa watendaji hao, ambapo imedhihirisha ukweli kwamba wengi wao hawana mipango mbadala ya kukabiliana na kero za wananchi.

Pamoja na Rais kuwapigania wamachinga ili waendelee kufanya shughuli zao wakati wakiandaliwa mazingira rafiki, pia aliwaonya wasitumie fursa hiyo kupanga bidhaa zao katikati ya barabara.

Ingawa hakuwaambia kwamba wapange bidhaa zao katikati ya barabara, wao wamekuwa wakitumia kauli hiyo vibaya bila kujali kama wafanyacho ni hatari kwa maisha yao. Wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wa mikoa hawawezi kukwepa lawama kwamba wameshindwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala hilo.

Inashangaza kuona kila jambo watasubiri kupewa maelekezo na maagizo kutoka juu, ilhali Rais amewaweka ili wamsaidie kuondoa kero za wananchi na kusimamia maendeleo ya wananchi.

Hilo pia limekuwa lijidhihirisha pindi viongozi wengine wakuu wa kitaifa wanapokuwa kwenye ziara na kukutana na mabango ya wananchi yanayoeleza hisia na kero walizonazo ambayo yanaashiria kuwa watendaji wa ngazi za chini hawashughulikii ipasabyo kero za wananchi wanaowaongoza.

Ifike wakati sasa waamke, wawajibike na kutambua majukumu yao bila kuelekezwa au kusukumwa. Ni vyema tuondoe kero hii badala ya kusubiri majanga yakitokea ndipo tunahangaika kutafuta ufumbuzi.

Mikofu ni mwandishi wa gazeti hili mkoani Mwanza; 0755-996593.