Uamuzi wa kumpa Kim Poulsen timu zote za vijana uangaliwe upya

Muktasari:

  • Hapo awali, Kim amekuwa kocha mkuu wa timu za Vijana kabla ya kuwa mshauri wa ufundi wa timu hizo na kocha mkuu wa Taifa Stars.

Hivi karibuni, taarifa tulizozipata ni kwamba kocha Kim Poulsen ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu zote za Taifa za vijana.

Hapo awali, Kim amekuwa kocha mkuu wa timu za Vijana kabla ya kuwa mshauri wa ufundi wa timu hizo na kocha mkuu wa Taifa Stars. Inawezekana walioamua kumpa nafasi hiyo mpya wana sababu ya msingi ambayo hata hivyo, haikufafanuliwa na wadau kuendelea kujiuliza masuali mengi kama alikuwa mshauri na sasa amepewa azifundishe.

Maoni yangu yanatofautiana na uamuzi wa TFF kumpa Kim kuwa kocha mkuu wa timu zote tatu za vijana. Kuna mambo ambayo yangetakiwa yakubaliwe kiufundi na Kamati ya Ufundi ya TFF, mkurugenzi wa ufundi pamoja, TAFCA na kocha mkuu wa Taifa Stars ili uamuzi mkubwa kama huo uweze kufanyika.

Nasema hivi kwa sababu taasisi hizo tatu zikikutana na Kocha wa Timu ya Taifa watakuwa na uwezo wa kuamua ujenzi wa mpira wetu kama Taifa unataka kupitia njia ipi (Game Philosophy) ili maelekezo kwenye timu zote za Taifa yawe yanafanana na hivyo, kuwa rahisi kujenga timu bora ya Taifa.

Haya ndiyo yanayofanyika hata kwenye ngazi ya vilabu ambako wana timu nyingi, mathalani U-10, U-12, U-15, U-17 na U-20, kocha mkuu wa timu ya wakubwa ndiye anayetoa maelekezo ya filosofia ya uchezaji wa klabu hiyo.

Niliuona uzoefu huo wakati nikiwa kocha mkaribishwa wa Klabu ya Ligi Kuu ya Denmark ya Lyngby miaka ya 2000, ambapo kocha mkuu alihakikisha kwamba makocha wa timu zote za vijana wanafuata filosofia ya mfumo wa uchezaji wa klabu hiyo ili kuijenga timu.

Kocha mkuu aliamua siku moja ya kila juma anaitumia kwa kuitembelea timu mojawapo ili kuona kama yale ambayo wamekubaliana na makocha wake wasaidizi wanayafuata.

Kwa maelezo hayo hapo juu, nina shaka kwamba TFF ilifanya hivyo kabla ya kumpa Kim kuwa kocha Mkuu wa timu zote za Taifa za Vijana. Wasiwasi ninaouona ni kwa Kim kuwa na falsafa yake ambayo inaweza isiwiane na mtazamo wa chama cha makocha na yale ya kocha mkuu wa timu ya Taifa. Ushauri wangu ni kwamba, yafuatayo yangefanyika kabla ya maamuzi hayo yaliyofanyika.

Kamati ya Ufundi ya TFF, Mkurugenzi wa Ufundi, TAFCA, kocha mkuu wa Taifa Stars wa sasa na baadhi ya makocha waandamizi (ambao walishafundisha timu ya Taifa) wangeweza kukaa na kutengeneza mpango wa muda mfupi wa kufanya ili kupata timu bora za vijana na hatimaye Taifa Stars na kukubaliana nini kifanyike.

Mawazo ya jopo la watu kama hao yasingeishia kukubali kocha mmoja awe kocha mkuu wa timu zote za vijana.

Uamuzi sahihi ungekuwa ni kila timu ya vijana kuwa na kocha mkuu na wasaidizi wake na timu zote za vijana zingekuwa na Mshauri wa Ufundi. Hapo ndipo ambapo, Kim angeweza kupewa nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake wa kuwa na timu zetu za vijana kwa kipindi kirefu na mara moja kama kocha mkuu hivyo, angekuwa na msaada zaidi badala ya kuwa kocha mkuu wa timu zote.

Kama hayo yangefanyika, Kim kama Mshauri wa Timu za Vijana angekuwa anafanya kazi kwa karibu na Kocha Mkuu wa Taifa Stars ili kwa pamoja kuona kama filosofia iliyokubaliwa na kamati ya hapo juu inafuatwa na wachezaji gani wanaelekea kupandishwa timu ya wakubwa.

Kuna madhara makubwa ya kumpa kocha mmoja kuwa kocha mkuu wa timu zote tatu. Kwanza atayafanya anayoyataka yeye kwa sababu atakuwa hana hadidu rejea ambazo anatakiwa azifuate. Anaweza pia kumleta/kuwaleta makocha wasaidizi kutoka kwao ambao, pengine wanakuwa hawana faida kwetu. Mfano rahisi ni wakati Kim alipomleta kocha Jacob Nikelsen kuwa kocha wa msaidizi wa vijana.

Kwa mtu yeyote mwenye uelewa wa nini maana ya ukocha, alishangazwa na umri mdogo wa Jacob kuja kusaidia kukuza vipaji vya wachezaji wetu. Ninavyoelewa ni kuwa, wachezaji wadogo wanahitaji wafundishwe na kocha mwenye ujuzi na uzoefu wa ukocha wa muda mrefu kwani, anakuwa na rasilimali nyingi za kiufundi na uzoefu wa kuwaendeleza wachezaji hivyo kuwa na msaada zaidi.

Makala yangu hii inalenga kuonyesha kwamba, maamuzi yaliyofanywa na TFF ya kumpa Kim (hata angekuwa kocha mzawa) timu zote za vijana za Taifa kama kocha mkuu haukuwa sahihi kutokana na maangalizo niliyoyaonyesha hapo juu. Kama hayakuangaliwa, malengo yanayokusudiwa yanaweza yasifikiwe kabisa.

Mbaya zaidi, anayemsaidia Kim ni kocha anayeinukia, ambaye kwa uzoefu wangu anaweza asiwe na msaada kwa Kim kwa sababu hatakuwa na uwezo wa kumshauri masuala ya ufundi.

Anaweza kukwama kwa maana kwamba, kama Kim hatakuwa na mawazo mbadala jambo ambalo si sahihi. Kocha msaidizi anatakiwa awe ni mtu mweledi na anayekaribiana kiufundi na uzoefu na kocha mkuu ili waweze kushauriana vizuri kwenye masuala ya ufundi na hatimaye kufanikiwa.