Ubunifu wa watendaji vyama vya ushirika utaongeza tija ya sekta hiyo

Muktasari:

Ni muhimu vyama vya ushirika tuone wivu na kujifunza siri za mafanikio kwa taasisi hizi ili tujiwekee malengo ya kuboresha na kupiga hatua kuipa thamani sekta ya ushirika nchini.

        Vyama vya ushirika vinaendeshwa kwa kufuata sheria na sera kama ilivyo kwingineko kama vile benki na taasisi za fedha ambayo imefanikiwa kutokana na ubunifu, uboreshaji wa huduma kukabili ushindani uliopo.

Ni muhimu vyama vya ushirika tuone wivu na kujifunza siri za mafanikio kwa taasisi hizi ili tujiwekee malengo ya kuboresha na kupiga hatua kuipa thamani sekta ya ushirika nchini.

Zamani kulikuwa na muingiliano mkubwa wa maamuzi na kiutendaji kutokana na Serikali kuhusika moja kwa moja kwenye usimamizi wa sekta hii. Kwa kiasi kikubwa utaratibu ule ulisababisha baadhi ya vyama kushindwa kufanya vizuri hata kufa kabisa.

Kwa wakati huu hali hiyo imepungua na kutoa nafasi kwa vyama kusimamia maamuzi na mipango mizuri inayofanyika kwa weledi na kujali maslahi mapana ya taasisi na wanachama wake. Ni jambo la kufariji.

Pamoja na nafasi hii kuna maeneo ambayo bado vyama vya ushirika vimekuwa vikishindwa kubuni na kuleta mapinduzi kwa ajili ya kuongeza ubora wa huduma na bidhaa za vyama vya ushirika kwa muda mrefu sasa.

Kwa nyakati hizi za ushindani wa kibiashara ni vema kuwapa nafasi viongozi na wafanyakazi wa vyama vyetu kuvumbua, kugundua na kujaribu vitu vipya vyenye tija kwa wanachama. Uhuru huu unatakiwa utumike kwa kutumia rasilimali za chama vizuri.

Ubunifu uelekezwe kwenye miradi, bidhaa na huduma kuinua sekta ya ushirika kwa ujumla wake. Ili kuzifanya taasisi hizi za wakulima na wajasiriamali wadogo kushindana ni lazima kubuni mbinu sahihi za kufikisha na kutoa huduma husika.

Uhuru huu hautakiwi kutumiwa vibaya kwa sababu sekta hii ina sera na sheria zake za kufuata hivyo wenye majukumu ya kuendesha vyama vya ushirika ni lazima wafanye maamuzi mazuri na kusimamia taasisi kisasa bila kukiuka sheria za sekta na zile za nchi.

Lengo kubwa la kuwaachia uwanja wataalamu hawa ni kuziacha akili na busara zao pamoja na ubunifu bila kuingiliwa, kupendekeza mema yatakayoongeza tija kwa kuleta vitu vipya kwa wadau wa sekta hiyo.

Lengo ni kuwapa uhuru kuona namna wanavyoweza kujisimamia kutafuta majibu chanya ya changamoto zinazowakabili kama taasisi na taifa kwa ujumla. Jambo la msingi ni kuepuka kuutumia uhuru huu na utendaji mbovu na kufuja mali na rasilimali chache za wanachama.

Kikubwa ni kufanya kazi kwa weledi kwa mawasiliano mazuri ya wafanyakazi, kamati, bodi na wanachama ambao ndio wamiliki lakini kubwa zaidi kwa ushirikiano wa viongozi warajisi wasaidizi mpaka uongozi wa juu kabisa wa tume na serikali.

Hakuna nchi inayopenda kuwa na taasisi zinazodumaa na kukaukiwa rasilimali kila kukicha hivyo tunaamini kwa kutumia ubunifu na kufanya kazi kwa uhuru na kujiamini tutapata majibu ya namna ya kutumia teknolojia ya kisasa kwenye vyama vya ushirika.

Uwekezaji kwenye viwanda na maeneo mengine yenye tija kwa chama na taifa, ubunifu na utafiti wenye tija kwenye kilimo na biashara ndogo ni miongoni mwa yanayosubiriwa na wadau.

Viongozi na wafanyakazi wa vyama vya ushirika waamke na kufikiria mambo makubwa ili kuisaidia sekta hii muhimu kukua na kuleta mapinduzi ya kipato na kijamii wanachama na taifa kwa ujumla.

Vyama vya ushirika vijitathimini, wapi vimetoka na mabadiliko ya dunia kwenye ushindani na ubunifu halafu viweke mikakati ya namna ya kusogea mbele taratibu.

Mwandishi anapatikana kwa namba 0657 157 122.