Tuesday, November 7, 2017

Udhalilishaji uliofanywa na mwalimu huyu usivumiliwe

By Mwananchi

Katika toleo la Mwananchi jana, tuliripoti kisa cha mwalimu mkuu wa shule moja ya msingi wilayani Biharamulo, Kagera aliyeamua kumcharaza mwalimu mwenzake viboko kadhaa kama njia ya kumrudi.

Kisa hicho kilitokea katika Shule ya Msingi Migango ambako mwalimu mkuu alimchapa viboko mwalimu mwenzake mbele ya wanafunzi akimtuhumu kwa wizi wa sahani tano pamoja na nusu kilo ya sukari iliyotolewa kwa ajili ya mahafali ya wahitimu wa darasa la saba.

Taarifa zilizokifikia Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Biharamulo zimeeleza kwamba badala ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, mwalimu mkuu huyo alitafuta ridhaa ya kumaliza kesi kienyeji, hivyo akajipa mamlaka ya kutoa adhabu; akamkamata mtuhumiwa, akamfunga kamba chini ya mti ili asifurukute kisha akamcharaza viboko saba.

Tumesikitishwa namna maadili ya uongozi yanavyoporomoka kwa kasi kiasi kwamba watu ambao hawana mamlaka kisheria kuwaadhibu wakosaji au watovu wa nidhamu au wakiukaji wa taratibu hujichukulia sheria mkononi.

Tumeshuhudia katika miaka ya hivi karibuni wakuu wa mikoa na wilaya wakishindana ama kuwasimamisha kazi watumishi wa halmashauri au kuwaweka ndani viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa.

Waziri mkuu amewahi kukemea tabia hiyo bila mafanikio. Pia Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma iliwahi kutoa orodha ya watu wenye mamlaka ya kutoa adhabu ukiwa ni mwongozo kwamba wale ambao hawakutajwa wasithubutu, lakini juhudi zao hazijazaa matunda.

Sasa tabia hii ya kujichukulia sheria mkononi imeshuka hadi chini kufikia mwalimu mkuu wa shule kujiona ana uhalali wa kuwaadhibu walimu wenzake.

Hii ina maana kwamba mwalimu mkuu huyu hajui mipaka ya mamlaka yake na hajui kumcharaza viboko mwalimu mwenzake mbele ya wanafunzi kwamba ni kitendo cha udhalilishaji na kinyume cha haki za mtumishi na binadamu.

Hii ina maana kwamba mwalimu mkuu huyu hajui mwizi akikamatwa anapelekwa wapi. Ni kweli mwanafunzi mdokozi huadhibiwa shuleni lakini mwenye mamlaka ya mwisho hata kwa mwanafunzi mwizi, mgomvi, anayejihusisha na mapenzi na makosa mengine makubwa ni bodi ya shule.

Tunajiuliza kwa nini mwalimu mkuu huyu wa shule alijipa mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC)?

Itakumbukwa kwamba Februari 2009, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Bukoba katika mkoa wa Kagera alifanya kosa kama hilo alipoamuru polisi mmoja kuwachapa viboko walimu wa shule tatu za msingi kutokana na wilaya hiyo kuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba. Waliocharazwa viboko ni walimu tisa wa Shule ya Msingi Katerero, kumi na moja wa Kanazi na 12 kutoka Kansenene.

Mkuu yule wa wilaya alidhani kwamba uamuzi ule ungesaidia kuwakumbusha walimu wajibu wao ili waache kuchelewa, wafundishe inavyopaswa ili wilaya ya Bukoba isiwe ya mwisho kimkoa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Lakini alisahau kuwa yeye hakuwa mamlaka ya kuwaadhibu walimu na hata kama angekuwa nayo, adhabu ile haikustahili na ulikuwa udhalilishaji mkubwa. Baadaye uteuzi wake ulitenguliwa na mamlaka iliyomteua.

Tunashauri mwajiri wa mwalimu mkuu huyu na wengine wa aina yake kuwakumbusha mwisho wa mipaka ya mamlaka yao ili kuondoa migongano, usumbufu na udhalilishaji.

-->