Uhamasishaji afya ya uzazi kwa vijana uimarishwe

Muktasari:

  • Lakini tunaambiwa kuwa moja kati ya Malengo ya Milenia ilikuwa ni kuhakikisha huduma za afya ya uzazi kwa vijana zinaboreshwa ili kuwawezesha kuchangia maendeleo ya Taifa.

Ili kijana ajitambue anapaswa kukua akielewa mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza mwilini mwake pamoja na njia sahihi ya kudhibiti mihemko.

Lakini tunaambiwa kuwa moja kati ya Malengo ya Milenia ilikuwa ni kuhakikisha huduma za afya ya uzazi kwa vijana zinaboreshwa ili kuwawezesha kuchangia maendeleo ya Taifa.

Nchini, baadhi ya halmashauri na manispaa na zimeanza kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na maradhi mengine ya zinaa, baada ya vijana wengi kuhamasika na kuhudhuria kliniki ya huduma rafiki kwa vijana zihusuzo afya ya uzazi na mtoto.

Huduma hizo zinazotolewa katika zahanati mbalimbali za serikali zinahusisha matibabu na elimu ya namna ya kujikinga na maradhi hayo.

Aliwahi kusema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuwa afya kwa vijana ni muhimu na wizara yake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini zinapaswa kusaidia kutoa elimu hiyo kwa kina.

Naunga mkono kauli hiyo ya Waziri Ummy, kwa sababu hivi sasa idadi ya vijana wanaohudhuria kliniki kupima afya zao ni kubwa baada ya kuhamasishwa.

Shirika la Utafiti wa Tiba na Afya barani Afrika (Amref) ni miongoni mwa wafadhili wa shughuli za kuwaleta karibu vijana na kuwapatia mafunzo ambayo siyo tu yanasaidia kupunguza maambukizi ya maradhi ya zinaa na mimba za utotoni. Shirika hilo ambalo liliwahi kupeleka miradi ya afya ya uzazi wa mama na mtoto iliyodumu kwa miaka mitano katika manispaa za Iringa, Temeke, Ilala na Kinondoni, ilisaidia kushawishi vijana wengi kujitokeza kupata huduma za afya ya uzazi zinazotolewa kwenye zahanati na hospitali za serikali.

Tunaelezwa kuwa vituo hivyo vinawasaidia vijana kwa kuwawezesha kupata huduma mbalimbali ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa. Pamoja na juhudi hizo zifanywazo na Serikali kwa kushirikiana na wadau, jamii nayo ijue inalo jukumu kubwa la kutatua changamoto zinazo wakabili vijana kwa kushirikiana na hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Kwa sababu elimu inayotolewa katika vituo hivyo inasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za afya ya uzazi, ushauri wa kijamii na kisaikolojia, upimaji wa maradhi ya ngono na tiba, uzazi wa mpango na ushauri kwa makundi ya vijana wanaotumia dawa za kulevya.

Tutambue kuwa kazi ya utoaji huduma na upimaji unaendeshwa kwa kuzingatia usiri mkubwa baina ya mtoa ushauri na mpokeaji majibu, hutolewa kwa muhusika tu bila kushirikisha mtu mwingine, hivyo kijana akielimika itamsaidia kuwa muwazi juu ya afya yake.

Lakini kila jambo linachangamoto zake, wakati ninaposema Serikali na wadau juhudi zao zinaonekana, lakini bado wakumbuke hususan Serikali kuwa bado kuna upungufu wa wataalamu wa kutosha wa kutoa elimu kwa vijana wa uelimishaji rika, muda wa watoa huduma kuwa mdogo na wataalamu kuwa na muda finyu kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine.

Pia kuna changamoto ya wadau kushindwa kuwakutanisha vijana kutokana na ukosefu wa viwanja vya michezo. Haya yanastahili jicho la haraka.

Niliwahi kuzungumza na baadhi ya vijana ambao kwa sasa ni waelimishaji rika wa Wilayani Kinondoni, walisema wanakumbana na changamoto kutoka kwa baadhi ya wazazi wenye imani potofu kuwa kumpa elimu ya uzazi kijana ni kumhamasisha akafanye vitendo vya ngono.

Kwa majibu hayo, nilibaini wapo baadhi ya wazazi wanaoamini utoaji wa huduma rafiki kwa vijana ni jambo linalosababisha mimba za utotoni pamoja na maambukizi ya maradhi ya zinaa.

Tayari kuna wazazi au walezi wanawakatisha tamaa wanaotoa elimu kwa vijana hata ya kwenda kuelimisha shuleni au vyuoni kwasababu ya mawazo mgando .

Lilian Timbuka ni Mhariri wa Jarida la Afya anapatikana kwa namba 0713-235309

kwamba kijana akipatiwa elimu juu ya afya ya uzazi ni kumfundisha kufanya ngono, jambo ambalo si la kweli.

Halmashauri na manispaa nazo, zisichoke bali ziendelee kuchochea kwa kuhimiza elimu hiyo itolewee kwenye shule na vituo vya afya.

Kwasababu, kadiri vijana wanavyoelimika ndivyo wanavyoweza kujikinga dhidi ya maradhi ya zinaa, mimba za utotoni na kujitunza ili wawe na afya njema.

Nasema hivyo kwakuwa manispaa zinaelewa jinsi vijana wanavyofanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamoto nyingi za maisha.

Hivyo kukosa elimu ya uzazi kwa kundi hilo ni sawa na kuwaacha gizani na kuwaweka hatarini kuambukizwa maradhi ya ngono na kupata mimba zisizotarajiwa.