Ujio Rais Fifa fursa kwa viongozi wa vyama na klabu

Muktasari:

  • Kigogo huyo ambaye jina lake kamili ni Giovanni Vincenzo ‘Gianni’ Infantino, anatarajiwa kuwasili wiki hii akiwa ni mgeni wa Tanzania kupitia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Gianni Infantino, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi Tanzania kwa mara ya kwanza tangu alipoingia madarakani.

Kigogo huyo ambaye jina lake kamili ni Giovanni Vincenzo ‘Gianni’ Infantino, anatarajiwa kuwasili wiki hii akiwa ni mgeni wa Tanzania kupitia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, ugeni huo unatarajiwa kukutana na Rais John Magufuli.

Ratiba ya rais huyo, ambaye ataongozana na maofisa wa Fifa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), inaonyesha kwamba atazungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya mpira wa miguu.

Bila shaka Infantino ametimiza ndoto yake kwa Tanzania, baada ya kuahidi kumpa ushirikiano Karia muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa TFF.

Karia alichaguliwa rais wa TFF katika uchaguzi mkuu uliofanyika mkoani Dodoma Agosti 12, mwaka huu akirithi mikoba ya Jamal Malinzi.

Katika barua yake aliyomwandikia Karia Agosti 14, mwaka jana kutoka Zurich, Uswis, Infantino alisema milango ya ofisi yake iko wazi na alimuahidi kumpa ushirikiano katika nyanja zote ili Tanzania ipate mafanikio.

Kauli ya Infantino mwenye uraia wa Uswis na Italia, aliyechukua nafasi ya aliyekuwa rais wa Fifa, Joseph ‘Sepp’ Blatter imedhihirisha ana dhamira ya dhati ya kuiletea maendeleo Tanzania.

Infantino atakuja na ujumbe wake kwa ajili ya semina maalumu ya Fifa itakayohusisha nchi 21, wakiwemo wenyeji Tanzania, ambayo itadumu hadi Februari 23.

Kwa muda mrefu tumeshindwa kupata mafanikio katika soka tangu mwaka 1980 ambako tulishiriki kwa mara ya kwanza na mwisho fainali za Afrika mjini Lagos, Nigeria.

Kwa bahati mbaya udhaifa wa viongozi wengi wa vyama vya soka na klabu ndio chanzo cha Tanzania kuboronga katika medani ya soka.

Idadi kubwa ya viongozi wanaoingia madarakani hawana dhamira ya dhati ya kuleta mapinduzi ya soka kwa kuwa tayari wanakwenda na ajenda zao mkononi wakati wa uchaguzi.

Ni ukweli usiopingika wapo baadhi ya vigogo wameingia madarakani wakitaka kutumia fursa ya soka kama ngazi ya kupandia kwenda katika nafasi nyingine za uongozi nje ya mchezo huo.

Pia wapo baadhi ya viongozi walioingia madarakani wakiwa na dhamira ya kujinufaisha hasa baada ya kutumia gharama kubwa kupenya katika uchaguzi.

Mfumo unaotumika sasa katika uchaguzi unatoa mwanya kwa baadhi ya viongozi kuwahadaa wapiga kura kwa njia yoyote ile ili kutimiza azma yao ya kuingia madarakani.

Bila shaka ujio wa Infantino na ujumbe wake unaweza kuzaa matunda kwa kubadili fikra za viongozi wetu ambao wamekuwa na mtazamo hasi katika kusimamia utawala wa soka.

Semina ya Fifa inaweza kuibua mjadala kwa viongozi wetu wa soka kubadilika na kufanya soka kuwa bidhaa inayoweza kuiletea mafanikio Tanzania.

Soka ni mchezo wenye hadhi ya pekee duniani, tumeshuhudia nchi nyingi duniani zikipata mafanikio ya kiuchumi kupitia sekta ya mpira wa miguu.

Nashauri viongozi wa soka kutumia fursa ya ujumbe wa Fifa kubadili mtazamo na kuona kwamba soka ni fursa inayoweza kuwaletea Watanzania maendeleo.

Serikali kupitia TFF iweke utaratibu mzuri utakaotoa nafasi kwa viongozi wa vyama vya soka na klabu kujifunza kupitia ziara ya Infantino.

Semina ya Fifa ina maana kubwa, ni nafasi pekee kwa viongozi na wataalamu kutengeneza mtandano mpana wa mawasiliano baina ya Tanzania na nchi nyingine zilizopiga hatua katika medani ya soka.

Ni fursa nzuri kwa makocha, wataalamu wa masuala ya uongozi wa soka, viongozi wa vyama na klabu kujinadi kwa kuwa semina hiyo itaitangaza Tanzania duniani.