Ukimuita mwanao mbumbumbu, usitarajie matokeo mazuri shuleni

Muktasari:

Kwa sababu mama huyo alikuwa na hatua kubwa, mtoto alijitahidi kuharakisha lakini hakuweza kumkuta.

        Ni saa 12 asubuhi napita kwenye mtaa Golani uliopo Ubungo mkoani Dar es Salaam. Mbele yangu namuona mwanamke akitembea haraka huku mtoto anayeweza kuwa darasa la kwanza au pili akija nyuma yake.

Kwa sababu mama huyo alikuwa na hatua kubwa, mtoto alijitahidi kuharakisha lakini hakuweza kumkuta.

“We mbumbumbu tembea haraka huko, usinicheleweshe, mjinga nini?” ilikuwa sauti ya mwanamke huyo akimkaripia mwanawe.

Mtoto hakujibu chochote na alijitahidi kutembea haraka lakini hakuweza kumkuta mama yake.

‘Nitakutwanga makofi sasa hivi ohooo! Embu kimbia unachelewa shule, paka shume mkubwa we!” aliendelea kumuita kwa sauti ya juu zaidi.

Baadaye mama yule alisimama na mwanawe alivyomkuta alimshika mkono kwa nguvu na kuanza kumtembeza haraka, huku akimwambia maneno mengi ya kashfa nisiyoweza kuyaandika katika makala haya.

Binafsi niliumia na kwa sababu nilikuwepo sikuweza kuvumilia, nilimsihi mama yule amtembeze mwanawe polepole kwani hatua zao hazikuwa zinalingana.

“Mjinga tu huyu anadeka, anaacha kuamka mapema yeye anachelewa hii ndio dawa yake,”alijibu huku akimtembeza mwanawe huyo haraka zaidi.

Moyoni mwake aliamini kwa kufanya hivyo anampa mtoto huyo funzo la kutochelewa kuamka na kutembea polepole anapokwenda shule.

Mwanamke huyo anabeba sura ya wazazi au walezi wengi nchini. Wazazi ambao kwa matusi, kebehi na lugha ya kuudhi ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Kuna baadhi ya familia ni jambo la kawaida kwa wazazi au walezi kuwatamkia watoto wao maneno ya kashfa hata kuwaita majina ya wanyama, huku wakitegemea matokeo mazuri baadaye.

Vitabu vya Mungu vinaeleza wazi nafasi ya mzazi katika malezi ya mwanawe. Ni uhalisia kwamba matamshi ya mzazi au mlezi yanaweza kumfanya mtoto awe hivyo ukubwani.

Utasikia mzazi anamwambia mwanawe ‘paka mkubwa’ mara ‘jibwa pori we’, lione kwanza kichwa kubwa akili hakuna au domo kama birika na mengine mengi yasiyostahili kwa watoto. Wakati mwingine mama anaweza kumfananisha mtoto na tabia mbaya ya baba yake.

Bila shaka hakuna mtu mzima anayeweza kukubali kutamkiwa maneno ya aina hiyo akakaa kimya.

Ni ukatili mkubwa kumtamkia mtoto wako maneno ya laana halafu ukatarajia kuwa akiwa mkubwa, awe mtu wa hekima.

Itakua ajabu pale unapomuita mwanao mbumbumbu halafu ukatarajia aje kuwa mwanafunzi mwerevu darasani.

Kuna baadhi ya wazazi au walezi wanaamini kwa kufanya hivyo wanawafundisha watoto wao la hasha! Wasichojua ni kuwa maneno yanaumba.

Ni uwazi usiopingika kwamba moja ya makosa wanayofanya baadhi ya wazazi katika malezi ni kuwadekeza watoto wao pindi wanapokosea.

Mtoto hafundishwi kwa maneno makali na ya kashfa wala hapaswi kupewa adhabu kali kupita kiasi.

Kuna baadhi ya wazazi au walezi wamesha wachoma mikono watoto wao pale wanapohisi wameibiwa hata kama ni Sh10.

Huu ni ukatili usiokubalika hata kidogo. Watoto wana haki ya kuheshimiwa, kutunzwa, kujaliwa, kuthaminiwa na kupewa mahitaji yote ya msingi bila ubaguzi wala kupewa maneno ya kashfa.

Kwa nini kitu kinachoweza kukuudhi wewe umfanyie mtoto wako? Lazima jamii ibadilike na kuona umuhimu wa kuwaheshimu, kuwathamini na kuwalinda watoto.

Maendeleo mazuri ya elimu yanatokana na vile unavyomtendea mwanao tangu akiwa mdogo. Kwa kusema hivi simaanishi kwamba mtoto akikosea asionywe. Mtoto anapaswa kuonywa kwa lugha ya staha isiyo na madhara kwake baadaye katika maisha yake.

Kiuhalisia watoto wanapolelewa kwa maneno mabaya na ya kuudhi, ndivyo watakavyokuja kuwa baadaye.

Ikiwa utakutana na mtoto anatoa maneno ya kashfa yasiyo na hata chembe ya staha mbele za watu, bila shaka tabia hiyo mbaya ameichukua kwa wazazi au walezi wake.

Maandalizi mazuri ya mtoto ni malezi bora tangu akiwa mdogo.

Mwenye jukumu kubwa la kuhakikisha mtoto analelewa kwenye misingi mizuri ya kimaadili ni mzazi na mlezi sio walimu peke yao shuleni.

Ikiwa mzazi hatomjengea misingi mwanaye tangu utotoni, asitegemee muujiza kwa mtoto wake kutimiza ndoto zake za kimaisha siku za baadaye.

Kama ulivyo msemo wa Wahenga kuwa maneno yanaumba; mtoto akiitwa jambazi kwa mfano, jina hilo linaweza kuja kuwa sehemu ya maisha yake ukubwani.

Tuwaite watoto majina mazuri ili waje kuwa wanajamii bora baadaye.

Tumaini Msowoya ni mwandishi wa Mwananchi. [email protected]