Ukimya wa wazazi utawaangamiza vijana

Muktasari:

Msaada wa mzazi katika kumsaidia kijana kujitambua hasa pale anapoanza kubadili mienendo ni mkubwa sana na pale mzazi anapojisahau anajikuta akiilaumu jamii kuwa imemharibia mwanaye bila kufahamu kuwa na yeye ni miongoni mwao.

        Ukuaji wa vijana hasa wa Kitanzania na kiafrika kwa ujumla unakumbana na mambo mengi ambayo wakati mwingine wengi hushindwa kuyakabili kwa uzito wake na kujikuta wakitumbukia kufanya matendo ambayo kama wangetayarishwa mapema wasingeyafanya mambo hayo.

Msaada wa mzazi katika kumsaidia kijana kujitambua hasa pale anapoanza kubadili mienendo ni mkubwa sana na pale mzazi anapojisahau anajikuta akiilaumu jamii kuwa imemharibia mwanaye bila kufahamu kuwa na yeye ni miongoni mwao.

Inaelezwa kuwa ubongo wa mtoto mdogo mpaka anapofikisha umri wa miaka 18 ni mwepesi kukariri jambo na kuliingiza katika vitendo bila kutafakari faida na hasara .

Wataalamu wanashauri wakati huo ndio wa mzazi au mlezi kutumia uwezo wake kumuelekeza kijana huyo ni kipi cha kufanya na ni kipi cha kuacha.

Moja kati ya udhaifu ambao unaelezwa kwa wazazi walio wengi wa sasa ni tatizo la ukimya hasa linapokuja suala la kuwaelekeza vijana au watoto wao ukweli juu ya maisha na kuwaeleza kinagaubaga ni kipi cha kuzingatia kama wanahitaji kuwa na maisha imara hapo baadaye.

Tatizo la ukimya halikuanza miaka ya karibuni lilikuwepo tangu enzi. Japo zamani lilitumika kama mbinu sahihi kabisa ya kuwakinga vijana wasijishirikishe katika matendo maovu na hii ilitokana na ukweli kuwa zamani maelekezo yote ya maisha yalikuwa yanatoka kwa wazazi na walezi hivyo ilikuwa rahisi kumficha kijana jambo na akaendelea kutokulijua kwa muda mrefu.

Mbinu hii imekumbwa na changamoto ya utandawazi ambayo imefanya kila kitu kuwa wazi ambapo kama utaamua kukaa kimya basi mwanao ataelekezwa na watu wengine na anaweza kuelekezwa jambo baya likampelekea kuwa na tabia chafu kuliko ungemuelekeza wewe kama mzazi.

Tuchukue mfano huu. Zamani wengi tuliambiwa na wazazi wetu kuwa watoto hununuliwa . Kwa kuwa hatukuwa na mahala pengine pa kujua ukweli kuwa watoto wanazaliwa tuliamini, hivyo ilikuwa rahisi sisi kuamini na kulishika kichwani.

Lakini je, leo unaweza kumwambia mwanao kuwa watoto wananunuliwa sokoni akakuamini? Jibu ni hapana anaweza kukuitikia lakini atakutana na ukweli kama sio kwa wenzake basi kwenye mitandao.

Wazazi wamekuwa waoga kuzungumza na watoto mambo kadhaa kama masuala ya afya zao, magonjwa ya zinaa, namna ya kujikinga na magonjwa hayo, kuhusu mahusiano na mabadiliko ya miili yao, mambo ambayo ni muhimu kwa vijana hasa wale wanaoelekea kubalehe.

Masuala haya tukubali tukatae hakuna mtu mwingine atakayemwelewesha kijana wako kwa usahihi zaidi kama wewe mzazi.

Hii inatokana na kuwa mzazi ndiye anayemjua mwanae, tabia zake, mienendo yake hivyo ni rahisi kumfuatilia na kujua ni kipi anastahili kuelezwa kwa undani na kwa wakati gani.

Vijana wengi wamejikuta wakijiingiza katika matendo machafu kama kufanya ngono zembe, uvutaji wa bangi na dawa za kulevya na tabia nyingine chafu.

Sababu ikiwa ni moja tu, wazazi walikaa kimya wakiamini kuwa umri wa watoto wao hawastahili kuelekezwa maswala hayo.

Ni wakati sasa wazazi tukubali kuwa dunia tunayoishi kwa sasa hakuna kitu cha kuficha tena kwa mwanao, ukimficha wewe ataambiwa na wengine na watamwambia kwa njia mbaya. Tunaweza kuwalaumu vijana hasa pale wanapotumbukia kwenye tabia ovu lakini kwa upande mwingine wazazi tunastahili kulaumiwa.

Exaud Mtei

0712098645/0752402602