Ukiwa na cheti cha mlipakodi, u kamili sokoni

Justine Kaleb

Muktasari:

  • Cheti hiki hutoa fursa kwa mfanyabiashara kuendelea na mchakato mwingine kama vile kutafuta leseni au kufungua akaunti ya benki. Cheti hiki hutolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA) pekee kwa wafanyabiashara na asasi kijamii.

Baada ya kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) mfanyabiashara anahitaji cheti cha uthibitisho wa mlipakodi ambacho hutolewa kuonyesha mhusika amekamilisha malipo ya makadirio kwa mwaka wa fedha husika.

Cheti hiki hutoa fursa kwa mfanyabiashara kuendelea na mchakato mwingine kama vile kutafuta leseni au kufungua akaunti ya benki. Cheti hiki hutolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA) pekee kwa wafanyabiashara na asasi kijamii.

Kupata namba ya utambulisho wa mlipa kodi haimaanishi kuwa umemaliza kila kitu na hudaiwi, kuthibitisha huna deni ni lazima upatiwe cheti hiki ambacho hakina mlolongo mrefu kukipata. Mhusika anahitaji kuwa TIN na baadhi ya viambatanisho kukipata.

Kuna viambatanisho tofauti vinavyohitajika kwa wafanyabiashara au asasi za kiraia kupata cheti hiki. Kwa wafanyabiashara ambao hujumuisha, mtu binafsi, biashara ya ubia na Kampuni mahitaji huwa tofauti pia.

Muombaji wa cheti cha uthibitisho wa mlipakodi katika kundi hili, licha ya namb aya utambulisho wa mlipakodi, atatakiwa awe amelipa makadirio ya awamu kama atakavyoelekezwa na mtathimini wa mamlaka ya mapato pamoja na ushuru wa forodha. Vilevile atapaswa kuwa amelipa kodi ya mapato.

Kwa taasisi za kidini na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) ambazo zina msamaha wa kulipa kodi, bado utaratibu wa kisheria unazitaka asasi hizi kuhakikisha baada ya kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi zinapata cheti cha utambulisho wa mlipakodi ili kuondoa usumbufu wowote utakaoweza kujitokeza baadaye.

Muhimu kuzingatia kuwa nyaraka hizo ni lazima ziwasilishwe katika ofisi za TRA wilaya ambako biashara husika inapatikana. Kama nyaraka zote zitakuwa zimekamilika kuna uwezekano mkubwa wa kupatiwa cheti chako ndani ya siku moja au mbili pekee.

Kw abiashara za uhakika zinazohusisha mikataba minono cheti ni muhimu. Kwa baadhi ya mikataba, unaweza ukakosa biashara kama huna. Zipo taasisi za umma ambazo hiki ni miongoni vigezo muhimu kuwa navyo kwa chochote zinachotaka kununua kutoka nje.

Wapo wanaokitegemea kwa ajili ya kujiridhisha na taarifa za biashara yako kutokana na kila kinachokuwamo ndani yake. Cheti hiki, licha ya kuwa na namba inayokitambulisha ambayo ni ya pekee, huwa na nembo ya TRA pamoja na maneno yaliokolezwa yanayosomeka tax clearance certificate.

Vilevile, huwa na namba yako ya utambulisho wa mlipakodi, kinaonyesha wilaya au eneo kilipotolewa na kinapoweza kutumika, tarehe ya kutolewa na mwisho wa matumizi. Kinaonyesha namba ya usajili kutoka Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (Brela), jina la mlipakodi na shughuli zinazofanywa na mlipakodi husika.

Kuthibitisha uhalali wake, cheti hiki ni lazima kiwe na sahihi ya aliyekihidhinisha pamoja na kugongwa muhuri wa moto wa TRA. Hili ni muhimu zaidi kukifanya cheti chako kisiwe na mashaka. Vinginevyo, unaweza kujikuta unakumbwa na mashtaka ya kughshi nyaraka za serikali.

Kuwa na cheti hiki kuna faida nyingi. Kwanza utaweza kukitumia kupata leseni ya biashara, kuomba mkopo benki au wakati wa kufungua akaunti ya biashara. Pia, kitakusaidia kukuza kipato chako kwa amani na kuepuka usumbufu wa kufungiwa biashara yako.

Mambo ya kuzingatia baada ya kupata cheti hiki ni kuhakikisha unalipa makadirio ya kila baada ya miezi mitatu kama unavyotakiwa na kupeleka mrejesho (returns) ili kuepuka faini.

Mwandishi ni wakili wa kujitegemea. Anapatikana kwa namba 0755 545 545 600