Umakini unahitajika suala la mchanga wa madini

Muktasari:

Kamati hiyo ni ya kwanza kati ya mbili zilizoundwa na Rais kuchunguza suala hilo. Kamati ya pili ilipewa jukumu la kuangalia athari za kiuchumi ambazo nchi inazipata kwa kusafirisha mchanga huo nje badala ya kazi ya kuyeyusha ili kupata madini yaliyosalia baada ya kuchenjua dhahabu, ifanyike hapa nchini.

Jumatano iliyopita, kamati iliyoundwa na Rais kuchunguza kiwango cha madini kilichomo katika mchanga uliozuiwa bandarini jijini Dar es Salaam, ilikabidhi ripoti yake.

Kamati hiyo ni ya kwanza kati ya mbili zilizoundwa na Rais kuchunguza suala hilo. Kamati ya pili ilipewa jukumu la kuangalia athari za kiuchumi ambazo nchi inazipata kwa kusafirisha mchanga huo nje badala ya kazi ya kuyeyusha ili kupata madini yaliyosalia baada ya kuchenjua dhahabu, ifanyike hapa nchini.

Kampuni ya Acacia ndiyo inayosafirisha nje mchanga huo kutoka migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu ambayo inazalisha dhahabu.

Hoja ya kusafirisha mchanga huo nje ni kwamba kinu cha kuuyeyushia hakipo hapa nchini na kwamba kukijenga kwa kutegemea shehena ndogo ya mchanga wa madini inayozalishwa hapa nchini, haitakuwa sahihi kibiashara.

Mchanga huo, au kwa jina jingine makinikia, ni ule unaobakia baada ya dhahabu kuchenjuliwa mgodini na hivyo kuhitaji teknolojia nyingine kwa ajili ya kuuyeyusha kupata dhahabu iliyosalia pamoja na madini mengine.

Lakini ripoti ya kamati hiyo inaonyesha kuwa kiwango cha dhahabu kilichomo katika makontena 277 yaliyozuiwa bandarini, ni takriban mara kumi ya kiwango kilichotangazwa na Acacia na kwamba kampuni hiyo ya kigeni haikuweka bayana kuhusu madini mengine yanayoweza kupatikana katika mchanga huo.

Ripoti hiyo ya awali imesababisha Rais John Magufuli kuvunja bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), kumsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo, kuagiza wafanyakazi wake na wa Wizara ya Nishati na Madini kuchunguzwa na pia kutengua uteuzi wa aliyekuwa waziri, Profesa Sospeter Muhongo.

Serikali pia imeendeleza tamko lake la kupiga marufuku mchanga kusafirishwa nje hadi hapo suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, Acacia na wataalamu wengine wa madini, wamepinga matokeo ya ripoti hiyo wakisema kuwa kiwango cha madini kilichoripotiwa kuwa katika mchanga huo kimekuzwa na kwamba hadi jana ilikuwa haijapata ripoti kamili ya kamati hiyo.

Tayari kampuni hiyo imeonyesha nia ya kufungua kesi katika mahakama za kimataifa, huku ikidai kuwa uamuzi wa kuzuia mchanga kusafirishwa nje unaisababishia hasara ya dola 1 milioni kila siku, ambayo itaweza kutumiwa kama moja ya hoja.

Hapa vitisho vya Acacia kwamba itafungua kesi si hoja kwa kuwa kama kuna ushahidi wa kutosha hakuna haja ya kuogopa masuala ya mahakamani.

Lakini tunachopenda kushauri ni jinsi ya kushughulikia suala hilo. Hili ni suala la kitalaamu ambalo halihitaji jawabu la haraka, mihemko wala siasa.

Ni suala linalohitaji utulivu, busara na tahadhari katika mambo mengi wakati wa kuelekea kupata jibu sahihi la masuala ya madini.

Sekta ya madini imekuwa ikisumbua kwa muda mrefu na mawaziri wamekuwa wakituhumiwa kuhusika katika kashfa moja hadi nyingine. Wakati wote, uamuzi unaochukuliwa huwa ni ule wa kutatua matatizo ya wakati huo tu, halafu baadaye matatizo mengine kuibuka.

Suala hili lina athari za kisheria, kiuchumi, kisiasa na hasa maliasili zetu ambazo tulizizuia kwa muda mrefu kusubiri kupata uwezo wa kuzitumia.

Na kwa maana hiyo, suala hili limewekwa kisheria, lina mikataba yake ya ndani, linaangaliwa na mikataba ya kibiashara na uwekezaji tuliyosaini na mataifa mengine na masuala mengine mengi.

Hivyo, linaposhughulikiwa ni lazima lishughulikiwe kitaalamu kwa kuchukua tahadhari ya mambo mengine mengi ili linapoisha lisiathiri nchi kwa namna yoyote ile bali litujengee mwongozo bora wa kushughulikia maliasili zetu hapo baadaye.