MAONI: Umefika wakati Cecafa ijitathmini

Muktasari:

  • Kufanyika kwa michuano ni baada ya kukosekana kwa miaka miwili, tangu ilipochezwa mara ya mwisho mwaka 2015.

Michuano ya kuwania Kombe la Kagame itaanza Juni 29 kwenye Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Chamazi Complex unaotumiwa na klabu ya Azam.

Kufanyika kwa michuano ni baada ya kukosekana kwa miaka miwili, tangu ilipochezwa mara ya mwisho mwaka 2015.

Cecafa imeshindwa kujipanga kutokana na kile inachosema ukosefu wa wadhamini. Mwaka huu yamefanyika baada ya hivi karibuni Azam Media kutangaza kuidhamini.

Licha ya kuwapo kwa michuano hiyo ya ngazi za klabu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati chini ya Baraza la Vyama Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), soka la ukanda huu lipo chini.

Cecafa iliyoanzishwa m3waka 1973 ndilo shirikisho kongwe zaidi la soka, lakini limeshindwa kujipanga na kupitwa na ya kanda nyingine kama lile la nchi za Afrika Magharibi la Muungano wa Vyama vya Soka vya Afrika Magharibi (Wafu) lililoanzishwa mwaka 1975, Shirikisho la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) mwaka 1997, Muungano wa Vyama vya Soka vya Afrika Kaskazini (Unaf) ulioanzishwa mwaka 2005 na Muungano wa Vyama vya Soka vya Afrika ya Kati (UNIFFAC).

Pamoja na Cecafa kujivunia ukongwe huo, imekosa dira sahihi na mwelekeo wa uhakika wa kuendesha shughuli zake kwa ufanisi na kubakia kuombaomba huku ikitegemea fadhila za taifa mwanachama kujitolea kubeba mzigo wa mashindano ndipo nalo huanza kuchangamka.

Shirikisho hili limeshindwa kufanya vyema katika maeneo matatu; Mosi, kuna michuano ya klabu Afrika kwa maana Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho huko klabu za ukanda wake hazifanyi vizuri, hazivutii na huenda mataifa ya ukanda mwingine hutamani yapangwe kucheza na timu zetu yakiamini kwamba yatapita kirahisi.

Ni timu chache zinazofanikiwa kufanya vyema katika mashindano hayo lakini nazo aghalabu huishia katika hatua za makundi.

Eneo jingine ni kwenye michuano Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon). Matokeo ya mataifa ya Cecafa ni ya kusikitisha. Angalau Uganda inafurukuta na hata mwaka jana ilikuwa katika fainali hizo japokuwa haikufanya vizuri.

Katika ngazi ya mashindano ya Kombe la Dunia la Fifa, hakuna mahali pa kujivunia, mataifa ya Cecafa hayajawahi kuingia katika fainali hizo.

Ukanda wa Afrika Magharibi na Kaskazini kila mara wanakata tiketi kwenda katika fainali za Kombe la Dunia na mara chache Ukanda wa Kusini.

Kimsingi Baraza limeshindwa kwenda na kasi ya mabadiliko ya soka yaliyopo duniani. Linaendesha mambo yake kwa mazoea au kama bora liende.

Miaka ya nyuma, soka la Cecafa lilionekana imara pengine kutokana na uwepo wa baadhi ya mataifa makali katika soka ambayo baadaye yaliamua kujitoa na kwenda kuunda kanda yao ya Kusini (Cocafa).

Nchi za Zimbabwe, Zambia, Malawi, Shelisheli na nyingine, ziliamua kujiengua kwenye ukanda huo baada ya fainali za Chalenji mwaka 1992 na ziliungana na nchi za Afrika Kusini, Angola, Botswana, Namibia, Lesotho na Swaziland na kuunda shirikisho la soka la ukanda wa Kusini na kweli wamefanikiwa kwani, timu za Cocafa zipo juu kuliko za Cecafa.

Wakati umefika kwa viongozi wa Cecafa kujitathmini, linakosea wapi na kwa nini soka ya Cecafa imedorora, tatizo ni nchi wanachama au viongozi wa mataifa husika au wa shirikisho lenyewe?