Umoja urejeshwe Kenya kwa masilahi ya Afrika Mashariki

Rais Uhuru Kenyatta

Muktasari:

Kesi moja ilifunguliwa na aliyewahi kuwa mbunge na nyingine ilifunguliwa na wanaharakati wawili. Jopo la majaji lililoongozwa na Jaji Mkuu David Maraga limeamua kwa kauli moja kutupilia mbali kesi zote kwa madai hazikuwa na msingi.

        Mahakama ya Juu ya Kenya imeridhia ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta baada ya kutupilia mbali kesi mbili ambazo zilikuwa zimefunguliwa kupinga uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.

Kesi moja ilifunguliwa na aliyewahi kuwa mbunge na nyingine ilifunguliwa na wanaharakati wawili. Jopo la majaji lililoongozwa na Jaji Mkuu David Maraga limeamua kwa kauli moja kutupilia mbali kesi zote kwa madai hazikuwa na msingi.

Uamuzi wa kutupilia mbali kesi hizo umekwenda pamoja na kuridhia matokeo ya uchaguzi huo wa marudio yaliyompa ushindi mgombea urais kwa tiketi ya chama tawala cha Jubilee, Kenyatta.

Baada ya uamuzi huo, picha za televisheni zilionyesha wafuasi wa Jubilee wakiwa na shangwe, lakini kulikuwa na maandamano katika maeneo ambayo ni ngome ya upinzani.

Jubilee wanafurahi kwamba ushindi wa mgombea wao umedumishwa, lakini kwa upinzani wanasikitika kwani walitarajia mahakama ingeweka historia ya kubatilisha matokeo kwa mara ya pili kama ilivyofanya Septemba Mosi ilipofuta ushindi wa Kenyatta kwa uchaguzi wa Agosti 8.

Duniani kote, mahakama ndicho chombo cha kutoa haki. Japokuwa uamuzi wake wakati mwingine husababisha tafrani – upande mmoja kuchukia na mwingine kufurahia kama tunavyoshuhudia sasa nchini Kenya – wahusika wanapaswa kuuheshimu.

Uamuzi wa jana umefurahisha upande mmoja na kuudhi upande mwingine.

Kutokana na hali hiyo, tunashauri wanasiasa kutoka serikali ya Jubilee chini ya Rais Kenyatta anayesubiri kuapishwa Jumanne ijayo kufanya juhudi za makusudi kuzungumza na upinzani ambao kwa takwimu pia unaungwa mkono na watu wengi.

Takwimu zinaonyesha kuwa watu 15 milioni kati ya 19.6 milioni ya waliojiandikisha walishiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 8, lakini matokeo yaliyompa ushindi Kenyatta yalipobatilishwa na mahakama hiyo Septemba Mosi kutokana na dosari na kasoro mbalimbali, walioshiriki uchaguzi wa marudio walipungua.

Katika uchaguzi wa marudio uliosusiwa na mgombea wa muungano wa upinzani wa Nasa, Raila Odinga, kinyang’anyiro kilibaki kuwa chepesi kwa Kenyatta na alitangazwa mshindi kwa kura 7,483,895 sawa na asilimia 98 huku Raila akipigiwa kura 73,228 sawa na asilimia 0.96.

Mtu akiangalia asilimia 98 alizopata Kenyatta katika uchaguzi wa Oktoba 26, ushindi huo ni mkubwa ikilinganishwa na asilimia 54 alizopata katika uchaguzi wa Agosti 8. Hata hivyo idadi ya watu walioshiriki ni ndogo. Wapigakura 7,616,217 pekee ndio walijitokeza ikiwa ni asilimia 38.84 ya waliojiandikisha.

Ndiyo maana tunasema baada ya mahakama kutekeleza wajibu wake wa kupokea kesi, kusikiliza na kutoa hukumu, wanasiasa kutoka chama tawala na upinzani wana jukumu la kuzungumza kwa masilahi ya Kenya na Wakenya.

Kuna kila sababu kwa Kenyatta na serikali yake kuandaa utaratibu wa kufanya mazungumzo na upinzani kwa lengo la kuwatuliza nyoyo ili kuwashirikisha kwa namna moja au nyingine katika maendeleo ya nchi.

Wakenya kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika Mashariki wanahitaji maendeleo. Wanataka kuona barabara zikijengwa, dawa za kutosha hospitalini, shule zinakuwa na huduma muhimu, watu wanapewa huduma kwa wepesi na kunakuwa na ustawi kwa maisha ya watu.

Tunalazimika kushauri hivyo tukiamini kuwa Afrika Mashariki itakuwa salama iwapo tu kutakuwa na amani katika nchi nyingine zinaounda jumuiya hiyo.