Umuhimu wa utafiti masoko ya sanaa

Muktasari:

Pia, kutokana na ukosefu wa vifaa bora na mazingira duni ya kuzalishia au kufanyia kazi inasababisha uzalishaji wa bidhaa zisizokuwa na ubora hivyo kushindwa kufikia viwango vya ubora vilivyowekwa katika masoko ya Kimataifa ambayo yatoa fursa za kuuza bidhaa za Tanzania kama vile AGOA.

        Tafiti za masoko ambapo wazalishaji wengi wa bidhaa za sanaa hawafanyi ni pamoja na kufahamu soko linahitaji nini, kwa kiasi gani na muda gani kwani linabadilika mara kwa mara. Hii inasababisha kushindwa kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji ya soko na hivyo kutokuwa na uwezo wa ushindani kimataifa.

Pia, kutokana na ukosefu wa vifaa bora na mazingira duni ya kuzalishia au kufanyia kazi inasababisha uzalishaji wa bidhaa zisizokuwa na ubora hivyo kushindwa kufikia viwango vya ubora vilivyowekwa katika masoko ya Kimataifa ambayo yatoa fursa za kuuza bidhaa za Tanzania kama vile AGOA.

Taarifa za masoko zimekuwa haziwafikii wazalishaji au huwafikia wakati zikiwa tayari zimechelewa hivyo inasababisha kutojua ni bidhaa gani inauzwa katika soko na inauzwa kwa bei gani inayosababisha kuendelea kuzalisha bidhaa za aina moja bila kujua hali ya soko na bei ya bidhaa hizo.

Pamoja na changamoto zilizopo ni muhimu kuendelea kutolewa kwa mafunzo ya ujasiriamali ambayo itakuwa endelevu kwa wazalishaji na wafanyabiashara ya namna ya kutengeneza bidhaa bora, kuitangaza, kuisambaza na kutumia vifungashio bora; hii itasaidia kuwa na bidhaa zenye ubora na kuwa na mbinu za kiushindani wa biashara katika soko la Kimataifa.

Kufanya utafiti wa masoko ili kubaini nini kinahitajika katika soko ili kuzalisha bidhaa inayoendana na mahitaji ya watumiaji bidhaa hiyo pamoja na bei hizo kutokana na aina ya walaji unaowahudumia kwani walaji hutofautiana mambo mbalimbali kama vile mahitaji na kipato na hivyo mahitaji ya bidhaa ni tofauti pia.

Ubunifu katika uzalishaji wa bidhaa lazima uongezeke na sio kuendelea kuzalisha bidhaa kwa kuiga. Ubunifu unamsaidia kutofautisha mzalishaji mmoja na mwingine na hivyo kufanya mzalishaji kuwa wa kipekee katika soko na hivyo kuwafanya watumiaji wa bidhaa kuwa tayari kupokea bidhaa za kipekee, kutoka kwa mzalishaji hivyo kumsaidia kuwa mshindani katika soko.

Matumizi ya teknolojia ya kompyuta ambapo wasanii na wajasiriamali wanatakiwa kujifunza na kutumia katika shughuli za kibiashara. Matumizi ya vifaa vya mawasiliano yatasaidia kupata taarifa mbalimbali za masoko, kudadilishana na kupeana taarifa mbalimbali pamoja na kujifunza kupitia mtandao (internet) kutoka kwa watu mbalimbali na nchi tofauti. Hivyo itasaidia kukua kwa biashara na kufahamu mbinu mbalimbali za ushindani katika soko la Kimataifa.

Kuwa na taasisi za fedha zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu hata riba nafuu, na kusiwe na mlolongo mrefu katika suala zima la kutoa mkopo ili kumrahisishia mzalishaji kufanya kazi kwa haraka kutokana na muda na soko kwa ujumla kwani mahitaji ya soko yanabadilika mara kwa mara na kwa haraka sana . Pia hii itasaidia kuzalisha kwa wingi na kutumia vifaa bora vya uzalishaji.

Uhamasishaji wa soko la ndani liwe endelevu kwa kuhamasisha watanzania kuwa wazalendo na kununua bidhaa za Tanzania . hii itasaidia kuinua soko la ndani litakalomsaidia mzalishaji wa kazi za sanaa kupata kipato cha kutosha kitakachomwezesha kuzalisha kazi nyingi na zenye ubora itakayomsaidia kuwa na uwezo wa kuuza hata katika soko la nje na kuifanya Tanzania itambulike kwa kuzalisha bidhaa bora kimataifa.

Katika zama hizi za utandawazi, dunia imekuwa kama kijiji hivyo bidhaa nyingi zinatoka sehemu moja kwenda nyingine kwa wingi na kwaurahisi zaidi inayopelekea kuwa na ushindani mkubwa katika soko unaohitaji ubunifu na mbinu tofauti za kibiashara ili kuwa mshindani katika soko. Tanzania ina fursa kubwa katika soko la nje kwani bidhaa mbalimbali zinazopelekwa katika masoko ya nje kupitia maonyesho zimeonekana kupendwa na watumiaji kwani zimenunuliwa kwa wingi, kuuliziwa na baadhi ya waliopeleka wamepokea oda na baadhi kuingia mkataba ya kufanya biashara pamoja na wafanyabiashara kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.

Ikumbukwe kuwa Watanzania tumekuwa tukishiriki maonyesho mbalimbali ya nje mfano maonyesho ya China maonyesho ya Zimbabwe, maonyesho ya Malawi(Solo exhibition) maonyesho ya Madagascar(expo Madagascar) Maonyesho ya Rwanda. Aidha watanzania wamekuwa wakishiriki matamasha mbalimbali likiwemo tamasha la Jumuiya ya Afrika mashariki( JAMAFEST) ambalo lilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Rwanda mwaka 2013, na mwaka 2015 lilifanyika Nairobi – Kenya na mwaka huu 2017 tamasha hili litafanyika Kampala Uganda kuanzia tarehe 7/09 hadi 15/09/2017 ambapo Watanzania wanajiandaa vema kwa ajili ya kushiriki kuonyesha kazi bora za sanaa katika soko hilo.

Mwisho tunaamini kuwa ili kuendeleza na kukuza sanaa za Kitanzania ni lazima kuwe na juhudi za ziada za kufanya bidhaa hizo zikubalike kwanza na watumiaji wa soko la ndani kuanzia ofisi za serikali, taasisi mbalimbali, watu binafsi na jamii kwa ujumla watumie bidhaa hizo.

Kwa mawasiliano, maoni na ushauri wasiliana nasi kwa e-mail;[email protected] simu; 0756 700 496/0715 082 889/0715 973 952