Unaacha ubunge ugombee ubunge!

Muktasari:

Mabadiliko haya yananilazimu nijiulize; je, kuhama chama kimoja na kwenda kujiunga na kingine ni ukomavu au udhaifu wa mwanasiasa?

Inawezekana kabisa ikawa ni nchi yetu pekee ambako kinatokea kioja cha wabunge kuachia nafasi zao na kisha kukimbilia chama kingine kuwania tena nafasi hiyohiyo.

Mabadiliko haya yananilazimu nijiulize; je, kuhama chama kimoja na kwenda kujiunga na kingine ni ukomavu au udhaifu wa mwanasiasa?

Ninavyofahamu ni kwamba vyama vya siasa vinaundwa vikiwa na sera fulani vinazoziamini na vikiwa na katiba ambayo inaelezea lengo la vyama vyao.

Mara nyingi sera au katiba za vyama hazibadiliki mara kwa mara, ila uongozi unabadilika. Kwa mantiki hiyo basi, sababu za mwanasiasa mahiri kujiunga na chama fulani, zinapaswa kuwa ni sera au katiba ya chama husika.

Katika duru hizi mpya za kisiasa, sababu kama uungaji mkono wa utendaji kazi, pesa na kufuata mkumbo zimekua ni miongoni mwa sababu zinazohusishwa na kuhama kwa wanasiasa kutoka chama kimoja kwenda kingine.

Kumbukeni mnajinadi wenyewe kwa kuwaambia wananchi sera zenu wanawaamini bila kujali itikadi za vyama vyenu wanawachagua na mnaingia bungeni huku mkiwa mnaaminika. Ghafla mnaibuka na kusema mnaacha ubunge na mnahama vyama kwa sababu eti ya utendaji wa Serikali iliyopo madarakani umewakuna.

Mbaya zaidi ni wabunge haohao wanaotoka kwenye nafasi zao za ubunge ndio wanaowania tena wakiwa upande wa pili bila hata aibu, hii inakera.

Hivi najiuliza ikiwa wangeamua kubaki kwenye vyama vyao wasingeweza kweli kukubali utendaji wa Serikali? Mimi naamini Serikali haina chama, hivyo ni kwa ajili ya Watanzania wote.

Serikali ni ya wote haina chama na Rais ni wa wote hata yeye akipanda jukwaani amekuwa akisema ni rais wa Tanzania hajawahi kusema hawatambui wapinzani.

Sasa hili suala la kujitoa kwenye nafasi za ubunge linasababisha gharama za uchaguzi kuongezeka bila kujali kwamba kuna mambo mengi ya kufanya ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

Hii ni gharama kwa Taifa zima kwa sababu kwa sasa viongozi hawahawa ndio wanaotumia mitandao ya kijamii kujibizana badala ya kufikiria maendeleo kwa wananchi wao waliowatuma bungeni.

Lakini, nina imani kabisa kwamba wabunge tuliowachagua kwa kura nyingi wataanza kutujazia vifusi kwenye barabara zetu wakati uchaguzi utakapokaribia bila kujali kama wanaziba barabara tu.

Niwakumbushe wabunge kwamba hiki ndicho kipindi cha kutimiza ahadi kwa sababu wananchi hawasahau mlichoahidi.

Na pia kwa wale ambao wanataka kuhama vyama vyao wangesubiria kipindi cha uchaguzi watangaze kuhama ila siyo muda huu ambao tunawategemea mtuletee maendeleo jimboni ndio mnaamua kuhama.

Ikiwa wewe ni mwanasiasa unayejiamini, hata ukibaki upinzani utaweza kufanya maendeleo tu kwa kushirikiana na wananchi wako na Serikali au ukiwa CCM unaweza kuleta maendeleo yaleyale.

Kwani mambo mangapi ya maendeleo wananchi wanaamua kujitolea wenyewe kwa kushirikiana na viongozi wao wa Serikali za mitaa.

Tumeshuhudia wananchi wakijenga shule, vituo vya afya, kuchimba barabara na mambo mengine mengi tu ya kimaendeleo, sasa kama haya wabunge wakiwa karibu na wapiga kura wao wanashindwa nini kutimiza ahadi zao.

Siku hizi kuna wajanjawajanja wengi, eti siku hizi mbunge kurudi jimboni mpaka karibia kipindi cha uchaguzi.

0755 633394