Unachopaswa kufanya ikitokea unauguza majeraha

Muktasari:

  • Kipindi cha uuguzi mchezaji mwenye majeraha haya atapaswa kupata mlo uliosheheni makundi yote ya vyakula na huku akihitajika kuzingatia kanuni za afya katika uandaaji vyakula hivyo.

Ni kawaida kwa wanamichezo kupata mejaraha ya mara kwa mara kutokana na kushiriki michezo. Yapo mambo rafiki ambayo yakifanyika wakati wa kujiuguza huweza kusaidia jeraha kupona mapema.

Kipindi cha uuguzi mchezaji mwenye majeraha haya atapaswa kupata mlo uliosheheni makundi yote ya vyakula na huku akihitajika kuzingatia kanuni za afya katika uandaaji vyakula hivyo.

Mlo wa mchezaji huyo huitajika kuliwa katika ratiba maalum, ale milo mikuu minne na milo midogo midogo kama inavyojulikana vyakula vya katikati ya milo mikuu (snacks) ikiwamo matunda, juisi za matunda na vyakula jamii ya karanga.

Kipindi hiki ni vizuri kula vyakula vya protini kwa wingi ikiwamo samaki na jamii ya kunde kwani protini ndio muhimu katika ujenzi wa mwili.

Vile vile ulaji wa mboga na matunda unasaidia kwani imesheheni vitamini, madini na virutubisho ambavyo ni muhimu kwa kujenga kinga imara ya mwili.

Unywaji wa maji mengi ni muhimu sana ili keupukana na upungufu wa maji na kukosekana uwiano wa chumvi chumvi za mwilini, uwepo wa mambo haya mawili unaathiri utendaji wa tishu kiujumla ikiwamo kukaamaa kwa misuli hivyo kuongeza nafasi ya kujijeruhi. Wataalam lishe wanashauri mchezaji mjeruhiwa kutumia virutubisho lishe maalum kwani nazo zinausaidia mwili katika mambo mengi ikiwamo uungaji wa jeraha kwa haraka.

Mjeruhiwa apime uzito mara kwa mara kuona kama anaongezeka, uzito mkubwa unaongeza hatari ya kujijeruhi kutokana na shinikizo kubwa la uzito wa mwili.

Wakati wa uuguzi wa jeraha haitakiwi kujihusisha na michezo kabla ya kupona kwani kunahatarisha kujijeruhi tena.

Mjeruhiwa aanze mazoezi mepesi ya kunyoosha viungo pale tu unapoona hakuna maumivu yoyote unayohisi.

Hakikisha kipindi cha uuguzi unapata mapumziko yakutosha angalau kupumzika masaa 6-8 kwa siku.

Na ni vizuri pia kupata utulivu wa kiakili kwani shinikizo la kikakili lina athari katika kinga ya mwili ambayo ni nguzo muhimu katika kupona jeraha.

Mjeruhiwa azingatie usafi wa mwili ili kuepukana na uvamizi wa maradhi mengine.

Epuka na ulevi, uvutaji sigara au matumizi ya kilevi chochote kwani vinadhoofisha mwili na kuchelewesha uponaji wa majeraha ya tishu za mwilini. Ikumbukwe kuwa kuuguza na kupona kwa majeraha ya michezo ni ngumu zaidi kuliko kufanya mambo yapunguza hatari ya majeraha haya. Shikamana na matibabu na programu ya mazoezi tiba unayopewa na wataalam wa tiba za wanamichezo kwani ndio msingi wa kupona kwa mchezaji na kurudi mchezoni ukiwa imara kama hapo awali. Pale unapoona kuna mabadiliko yoyote yasiyo yakawaida katika jeraha ni vizuri kutoa taarifa au kufika katika huduma za afya kwa ajili ya ushauri na matibabu.