Unahitajika weledi malezi kwa watoto

Muktasari:

  • Mara nyingi anayelaumiwa kwa kukosa mtoto ni mwanamke kuwa hajazaa, lakini wakati mwingine mwanamume pia huweza kulaumiwa kwani anaweza kuwa mgumba.
  • Ndiyo maana tunashauri kuwa kabla vijana ambao ni wachumba hawajaamua kufunga ndoa, waende kwanza hospitali wapimwe si tu kama wameambukizwa Ukimwi bali pia kama mbegu za uzazi za mvulana na mayai ya msichana yanaweza kutungisha mimba.

Katika utamaduni wa Mwafrika, mtoto ni kiungo muhimu katika familia. Ndoa ambayo haina mtoto huonekana imepwaya, upendo hupungua na hata kutoweka baina ya wanandoa.

Mara nyingi anayelaumiwa kwa kukosa mtoto ni mwanamke kuwa hajazaa, lakini wakati mwingine mwanamume pia huweza kulaumiwa kwani anaweza kuwa mgumba.

Ndiyo maana tunashauri kuwa kabla vijana ambao ni wachumba hawajaamua kufunga ndoa, waende kwanza hospitali wapimwe si tu kama wameambukizwa Ukimwi bali pia kama mbegu za uzazi za mvulana na mayai ya msichana yanaweza kutungisha mimba.

Mtoto anapozaliwa na kukua, hupewa huduma zote muhimu hasa upendo wa pande zote mbili. Hupewa pia huduma muhimu za maisha kama chakula, mavazi, maji na makazi salama.

Ifahamike kuwa kuwapo kwa baba na mama tangu mtoto anapozaliwa hadi anakuwa na umri wa kutambua mema na mabaya, ni hatua muhimu ya kujenga upendo na kujiamini kwa muda wote atakaokuwa anajitegemea.

Katika jamii, mtoto anakua kiakili, kimwili na kihisia kulingana na mazingira. Mwanasaikolojia Jean Piaget aliwahi kusema kuwa hatua hizi za ukuaji wa mtoto ni lazima zizingatiwe.

Kuna wakati mtoto anapotaka kufanya anachohisi kinafaa nasi hatuna budi kuwa na busara kumwelekeza. Anaweza kutaka kufanya matendo yasiyopendeza na pengine ya kuudhi, lakini tuwe makini kumwelekeza. Hatua hii isikusumbue wala kukusikitisha.

Mtoto anaweza kulia. Hili ni jambo la kawaida kwani kunaweza kusababishwa na mambo mengi. Mfano mtoto anaweza kuwa na njaa, kiu, maumivu, mazingira kuwa magumu au kujisikia kutaka kwenda haja ndogo.

Hivyo, mlezi wa mtoto anatakiwa kutambua hilo na kutafuta ufumbuzi na siyo kumkemea, kumpiga au kumfinya.

Mwanasaikolojia mwingine Sigsmund Freud anatambua kuwa mtoto anapokuwa na umri mkubwa anakuwa na mwelekeo wa kutenda mambo kulingana na jinsi yake.

Unatakiwa kutambua hilo na kumpa nafasi afanye anachopenda. Mzazi awe tayari kumpa uhuru mtoto kushiriki katika uamuzi wa masuala yanayohusu kama vile kupenda chakula cha aina fulani au kuvaa mavazi fulani.

Mzazi au mlezi awe tayari kumtimizia matakwa yake na pale ambapo haiwezekani mtoto aambiwe ukweli. Tusijaribu kumdanganya mtoto hata mara moja, kwani tunampa matumaini yasiyotekelezeka.

Hata hivyo, inashauriwa wazazi wawe na busara ya kuamua lililo bora na litakaloleta manufaa kwa mtoto na hatimaye kufanya uamuzi kwa niaba ya mtoto.

Katika kipindi hiki cha ukweli na uwazi, watoto wanatakiwa wapewe fursa ya kujiamulia wenyewe na kujieleza bila woga na bila kuwatumia mama zao kuwasemea kwa baba.

Baba na mtoto wawe karibu na wawe wawazi na wakweli. Mtoto ajengwe kusema ukweli na kujiamini hata kama kufanya hivyo kutasababisha kupata adhabu. Watoto katika familia wanatakiwa wakisema wasikike. Maana yake ni kwamba watoto wawe huru kujieleza na kutoa madukuduku yao. Wazazi nao wawe tayari kuwasikiliza kabla ya kutoa uamuzi.

Wazazi wa kisasa waliopata elimu ya kizungu wamewaiga wazungu katika kuwalea watoto wao. Wanawabembeleza na hawako tayari kuwapa adhabu. Hata hivyo, tusiwe wakali kiasi cha kuogopwa na watoto.

Ukweli ni kuwa wazazi wa kisasa wako njiapanda. Kwa maneno mengine wazazi wa sasa ni kama popo. Wanashindwa kufuata malezi ya wazazi wao ya kutumia bakora au kuwaachia kama kuku wa kienyeji na kufanya kama wanavyotaka. Tunatakiwa kunyoa au kusuka!

0754 861664 0716 694240