Usafi wa mwili ni msingi wa kuepuka maambukizi ya UTI

Muktasari:

DOKEZO

Maambukizi ya njia ya mkojo hutokea pale tu bakteria wanaoeneza maradhi hayo wanapoingia kwenye njia ya mkojo.


Ukifanikiwa kudhibiti hilo kwa kuimarisha usafi, huwezi kupata ugonjwa huu.


Kukojoa mara kwa mara kunakoambatana na maumivu ni miongoni mwa dalili za maambukizi kwenye njia ya mkojo au UTI. Baadhi ya wagonjwa huhisi kichefuchefu, wengine hutapika.

Zipo dalili nyingi za maradhi haya. Homa, mkojo kuwa mwekundu usio na harufu ya kawaida, pia uchovu wa mara kwa mara na maumivu chini ya mgongo ni dalili nyingine ambazo hujitokeza.

Mfumo wa mkojo unaundwa na figo na ureta mbili, kibofu pamoja na urethra. Binadamu wote wana vitu hivyo ingawa ipo tofauti ya mfumo huu kati ya wanawake na wanaume.

Tofauti hiyo ni kwamba, wanawake huwa na urethra fupi wakilinganishwa na wanaume. Kutokana na ufupi wa urethra, wanawake wapo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi haya kuliko wanaume.

Takwimu zinaonyesha takriban watu milioni 150 duniani kote, hupata maambukizi kwenye njia ya mkojo, wanawake wakiongoza hasa wenye umri kati ya miaka 16 na 35. Wanawake hupata maambukizi haya mara nne zaidi ya wanaume.

Watoto pia ni waathirika wa maambukizi haya. Inaelezwa kwamba, asilimia 10 ya watoto hupata maambukizi haya kila mwaka. Watoto wa kiume ambao hawajatahiriwa na walio chini ya miezi mitatu wapo kwenye hatari hii na wa kike chini ya mwaka mmoja.

Utafiti unaonyesha asilimia mbili mpaka 20 ya watoto wenye umri wa miaka miwili hupata maambukizi ya njia ya mkojo pia.

Sababu

Bakteria wanaelezwa kuwa chanzo kikuu cha maambukizi. Bakteria aina ya  escherichia coli wanaelezwa kusababisha maradhi haya kwa kati ya asilimia 80 mpaka 85 na wale wa staphylococci kwa asilimia tano mpaka 10. Ni mara chache virusi au fangasi husabababisha UTI.

Bakteria aina ya staphylococcus saprophyticus husababisha UTI kwa watoto na wanawake waliovunja ungo au waliopo kwenye uhusiano wa ndoa. Clamydia trachomatis na E.coli huchangia kwani huweza kusababisha UTI ndani ya saa 12 mpaka 72 baada ya kufanya tendo la ndoa.

Ugonjwa huu pia huweza kusababishwa na mawe yaliyopo kwenye figo (nephrolithiasis) ambayo huongeza msongamano wa  njia ya mkojo hivyo kuvifanya vijidudu vya maradhi vizaliane kwa urahisi.

Tezi dume nalo ni miongoni mwa vitu vinavyorahisisha maambukizi ya njia ya mkojo. Kuvimba kwa tezi hili husababisha kufungwa kwa njia hivyo mkojo kukaa kwa muda mrefu kiasi cha bakteria kuzaliana na kusababisha madhara kwa mgonjwa.

Ugonjwa wa kisukari pia huchochea maambukizi ya UTI kutokana na kiwango kikubwa cha sukari kinachokuwapo katika figo na kibofu kwa muda mrefu  ambacho huchangia bakteria kuzaliana na kusababisha ugonjwa.

Kinga

Inashauriwa kuzingatia usafi wa mwili kwa ujumla ila njia ya mkojo ipewe kipaumbele. Kinachotakiwa ni kuoga maji safi na kusafisha sehemu hizo kwa umakini.

Kwenye usafi wa mwili, wanawake wanashauriwa kujisafisha kutoka mbele kwenda nyuma mara baada ya kujisaidia kwani hii huzuia bakteria walio sehemu ya kujisaidia kufika ukeni na kwenye urethra.

Unywaji wa maji safi na salama ya kutosha husaidia kusafisha njia ya mkojo kwa kukojoa mara kwa mara, hivyo kuruhusu bakteria kutolewa kabla hawajasababisha maradhi.

Usafi wa choo na bafu pia ni muhimu katika kukabiliana na maambukizi haya. Inashauriwa kusafisha maeneo haya kila mara kadiri iwezekanavyo hasa kabla ya kujisaidia au kuoga kwa wanawake.

Baada ya kushiriki tendo la ndoa, inashauriwa kukojoa kwani husaidia kuwaondoa bakteria wanaoweza kuwa wameingia kwenye kibofu wakati huo kabla hawajaleta madhara. Haishauriwi kutumia manukato hasa marashi sehemu za siri.

Wakati wote, inashauriwa kuepuka matumizi ya maji yasiyo salama wakati wa kuoga au kusafisha sehemu za siri zinazounda mfumo wa mkojo ili kutochochea maambukizi haya.

Kushiriki tendo la ndoa mara kwa mara pia ni kichocheo kingine cha maambukizi haya kwani hurahisisha bakteria kuingia kwenye mfumo wa mkojo kutokana majimaji yanayokuwapo ukeni.

Mambo haya yakizingatiwa, hurahisisha uwezekano wa kudhibiti ongezeko la maradhi haya ambayo huwakumba zaidi wasichana na wanawake walio shuleni na vyuoni.

Madhara

Maambukizi ya njia ya mkojo yanaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi endapo hayatatibiwa kwa wakati muafaka. Miongoni mwa maambukizi yanayoweza kujitokeza ni kupata ugonjwa sugu wa figo (pyelonephritis).

Ipo hatari kwa wajawazito kujifungua mtoto kabla ya muda au mtoto mwenye uzito chini ya kiwango. Inawezekana UTI kujirudia iwapo tiba itacheleweshwa. Hili hutokea kati ya asilimia 25 mpaka 40.

Vilevile, kwa wanaume, huwa kichocheo cha kupata maambukizi ya tezi dume au prostatitis.

Mwandishi ni daktari. Kwa ufafanuzi, anapatikana kwa namba 0759 775 788