Usalama barabarani, tutoke hapa twende pale

Muktasari:

  • Vilevile, aliwataka askari hao kutonyanyasa madereva ambao wanazingatia sheria za usalama barabarani.

Juzi, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliwaonya askari wa usalama barabarani kutogeuza tochi kuwa chanzo cha kudai rushwa huku akiwataka kufanya kazi zao kwa uadilifu. Samia aliyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama kitaifa yaliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Vilevile, aliwataka askari hao kutonyanyasa madereva ambao wanazingatia sheria za usalama barabarani.

Onyo hilo la Makamu wa Rais limekuja huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa madereva wanaodai kuwa askari hao wamegeuka kuwa ‘maofisa wa kodi’ kwani kila wanaposimamisha magari barabarani wanachokimbilia ni kuwaandikia makosa madereva husika ili walipe faini, badala ya kuwa waelimishaji wa nini wanapaswa au walipaswa kufanya madereva hao wawapo barabarani.

Kutokana na hali hiyo, askari wetu wa usalama barabarani wamepewa majina lukuki huko mitaani ikiwamo kuitwa maofisa mapato wa Serikali kwa kuwa kazi wanayofanya ni sawa na uwakala wa kukusanya kodi badala ya usimamizi wa sheria, uelimishaji na utoaji huduma kwa wateja ambao ni madereva, abiria na watumiaji wa barabara.

Hata hivyo, kama alivyosema Makamu wa Rais pia madereva wanapaswa kuwaona askari hao kuwa ni watu muhimu maana kwa pamoja wanaunda ushirika ambao unalenga kuyafanya maisha ya wananchi kuwa salama muda wote wanapotumia barabara.

Ushirika baina ya pande hizo ndio unaoweza kupunguza au kumaliza kabisa asilimia 76 ya ajali za barabarani zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu yanayotokana na utumiaji wa simu wakati wa kuendesha gari, uchovu wa madereva na ulevi.

Kutokana na wingi huo wa ajali, Taifa limeendelea kupoteza nguvu kazi, watu kupata ulemavu wa maisha na wengine kubaki wajane.

Kwa mujibu wa takwimu, mwaka huu kuanzia Januari hadi Septemba kumekuwapo na ajali za pikipiki 42,721 zilizoua watu 1,613 na kusababisha majeruhi 1,597 ikiwa ni ombwe jingine katika usalama barabarani linalohitaji wadau wapambane nalo ili kuokoa maisha ya watu.

Kinachosikitisha zaidi ni kitendo cha Tanzania kutajwa kwenye ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa nchi inayoongoza kwa ajali duniani ikiwa na asilimia 33. Jambo la kujiuliza ni kwa nini Tanzania iongoze kati ya nchi zaidi ya 200 duniani kwa kuwa na wingi wa ajali ilhali kuna vyombo vichache vya usafiri tofauti na mataifa yaliyoendelea, miundombinu sawa na mataifa mengi yanayoendelea na sheria kali za usalama barabarani?

Wingi huu wa ajali tulipaswa kuusikia ukitokea katika nchi zilizoendelea kama Marekani, Uingereza, Ufaransa na China ambazo zina vyombo vingi vya usafiri barabarani, lakini pia hata miundombinu yao inaruhusu magari kusafiri kwa mwendo mkali tofauti na yetu ambayo ubora wake haufikii ile ya kwao.

Pamoja na hayo, tunapenda kuwaomba wadau kushirikiana ipasavyo ili kuhakikisha kwamba tunapunguza kama si kumaliza kabisa ajali za barabarani. Jambo hilo linawezekana tu iwapo sheria za barabarani zitazingatiwa na askari wetu wasipochoka kuwa walimu wa madereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Ni vyema Baraza la Usalama Barabarani na kikosi cha usalama barabarani waache kutoa elimu pale inapofika wiki ya usalama barabarani au nyakati zingine za sherehe za kitaifa, bali uwe ni wajibu wao kila mara na kila wakati ikiwezekana kwa kuwafuata watu wanapokuwa na kuanza kutoa elimu.