Utapiamlo ni zaidi ya lishe duni

Muktasari:

  • Uzito pungufu ni hali ya mtoto kuwa na uzito mdogo ukilinganishwa na watoto wengine wa umri wake wenye afya njema. Uzito pungufu huweza kujionyesha kwa watoto wenye matatizo hayo mawili ukondefu na/au udumavu.

Utapiamlo ni hali mbaya ya lishe ambayo inaweza kuwa pungufu au iliyozidi. Katika nchi zinazoendelea kama Tanzania, utapiamlo ulioenea zaidi ni ule wa ulaji duni, ambao umekuwa ni changamoto kubwa katika kuboresha afya ya jamii.

Kuna aina kuu nne za utapiamlo ambazo ni utapiamlo wa nishati na utomwili, upungufu wa wekundu wa damu, upungufu wa madini joto mwilini na upungufu wa vitamin A.

Utapiamlo wa nishati na utomwili

Utapiamlo huu unatokana na ulaji duni wa vyakula vyenye virutubishi vinavyotoa nishati na utomwili. Vilevile upungufu wa baadhi ya vitamini na madini hujitokeza katika utapiamlo huu.

Utapiamlo wa nishati na utomwili huwapata zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano na watu wanaoishi na VVU. Lakini tatizo hili pia linaweza kuwaathiri watu wa makundi mengine. Utapiamlo wa nishati na utomwili huweza kutambuliwa kwa kulinganisha uzito, urefu na umri. Kipimo kingine ni mzingo wa mkono ambao hutumika kutambua hali ya ukondefu.

Kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, ukondefu ni hali ya mtoto kuwa na uzito pungufu ukilinganishwa na uzito wa watoto wengine wa kimo chake wenye afya njema. Ukondefu hutokana na ukosefu wa chakula au tatizo la kiafya lililojitokeza karibuni. Ambapo udumavu ni hali ya mtoto kuwa mfupi akilinganishwa na watoto wengine wa umri wake wenye afya njema. Hali hii hutokana na ukosefu wa chakula au tatizo la kiafya la muda mrefu. Uzito pungufu ni hali ya mtoto kuwa na uzito mdogo ukilinganishwa na watoto wengine wa umri wake wenye afya njema. Uzito pungufu huweza kujionyesha kwa watoto wenye matatizo hayo mawili ukondefu na/au udumavu.

Upungufu wa wekundu wa damu

Hili ni tatizo linalotokana na ulaji duni ambao husababisha upungufu wa virutubishi vinavyohitajika katika utengenezaji wa chembe chembe nyekundu za damu. Upungufu wa wekundu wa damu huchangiwa pia na magonjwa kama vile Malaria, ugonjwa wa selimundu (sickle cell), minyoo aina ya safura na kichocho.

Tatizo hili huathiri makundi yote ya watu katika jamii lakini watoto na wanawake ndio wanaoathirika zaidi. Upungufu wa wekundu wa damu huwapata zaidi watoto kwa sababu mahitaji ya madini ya chuma na virutubishi vingine ni makubwa zaidi kutokana na ukuaji wa haraka. Kwa upande wa wanawake, ujauzito husababisha ongezeko la mahitaji ya virutubishi mwilini. Mimba za karibu karibu huongeza ukubwa wa tatizo hili kwani mwili hushindwa kurudushia akiba ya virutubishi vilivyotumika katika ujauzito uliopita.

Dalili za upungufu wa wekundu wa damu ni uchovu na ulegevu wa mwili, mapigo ya moyo kuongezeka, kizunguzungu, kupumua kwa shida na weupe usio wa kawaida kwenye viganja, kucha, macho, midomo na hata ngozi ya mwili. Kuvimba miguu ni dalili ya upungufu mkubwa wa wekundu wa damu na wa muda mrefu.

Upungufu wa madini joto mwilini

Upungufu wa madini joto mwilini huwapata zaidi watu wanaoishi kwenye maeneo ya miinuko na milima kwa sababu sehemu hizo madini joto kwenye ardhi huwa yamepungua kutokana na kuchukuliwa na maji (mvua, mito, chemchem, mafuriko) na kuelekezwa mabondeni na baharini. Hivyo ni kiasi kidogo tu cha madini joto hupatikana katika vyakula vinavooteshwa kwenye ardhi hiyo.

Vyakula vinavyopatikana baharini au mabondeni huwa na madini joto mwilini ni pamoja na uharibifu wa ubongo (tahahira) na ukuaji duni wa mtoto. Wajawazito hupatwa na tatizo la kuharibika mimba na watoto kufia tumboni. Kwa watu wazima tatizo hujitokeza kama uvimbe wa tezi la shingo.

Upungufu wa Vitamini A mwilini

Upungufu wa vitamini A mwilini husababishwa na ulaji duni wa vyakula vyenye vitamini hiyo. Mtoto asiponyonyeshwa maziwa ya mama ipasavyo, hasa yale maziwa ya mwanzo, huwa kwenye hatari ya kupata upungufu wa vitamini A.

Magonjwa kama vile surua, magonjwa ya njia ya hewa na kuharisha pia huweza kusababisha upungufu wa vitamini A mwilini. Upungufu wa vitamini A husababisha kutoona vizuri katika mwanga hafifu. Tatizo lisipodhibitiwa mapema husababisha madhara zaidi kwenye macho na hata upofu. Vilevile husababisha ongezeko la magonjwa na vifo vya watoto.

Utapiamlo huletwa na sababu mbalimbali ambazo mara nyingi zinahusiana. Hali mbaya ya kiuchumi ni moja ya sababu kuu, ingawa baadhi ya wazazi hudai wana uwezo wa kuwalisha watoto wao ila watoto tu ndio hawataki kula. Hivyo nimeamua kuweka mbinu za kuwalisha watoto kiurahisi kama inavyopendekezwa na wataalamu wa lishe.

0712 366 660