Friday, November 13, 2015

Utoaji mimba na athari zake kiafya

Mwaka 1997 na  madaktari wa Finland waligundua

Mwaka 1997 na  madaktari wa Finland waligundua kwamba wanawake wanaotoa mimba mara kwa mara wana uwezekano wa kufa mapema zaidi kuliko ambao hawatoi. 

By Hadija Jumanne, Mwananchi

Utoaji wa mimba kwa njia isiyo salama umechangia kuongezeka kwa tatizo la ugumba na vifo vya watoto chini ya miaka mitano nchini Tanzania.

Mratibu wa Kituo cha  Kuhamasisha Hadhi ya Wanawake (WPC), Martha Jerome anasema tatizo hilo ni kubwa na juhudi za pamoja zinahitajika kukabiliana nalo.

Jerome anasema kwa hapa nchini wanawake wengi hutoa mimba hizo kwa njia za kificho kwa kukosa elimu pia kuogopa jamii inayowazunguka na sheria za nchi.

Anasema vifo hivyo vimechangia Serikali kushindwa kufikia Malengo ya Milenia (MDG) namba tano la kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kwa asilimia 75 kuanzia mwaka 1990 hadi 2015.

 “Nchi ilijiwekea malengo ya kupunguza kiwango cha vifo kutoka vifo 454 kwa kila wanawake 100,000 hadi vifo 193 ifikapo mwaka 2015, lakini mpaka sasa idadi ya vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi ni  410 badala ya 193 hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kukabiliana na hali hii hapa nchini,” anasema Martha.

Anasema  mikoa  yenye vitendo vya ukatili wa kijinsia ndiyo inaongoza kwa kuwa na kesi nyingi za utoaji wa mimba usio salama na kwamba asilimia 13 hadi 61 ya wanawake wanafanyiwa ukatili wa kijinsia  huku wanaume wakifanyiwa ukatili kwa asilimia tatu.

Chanzo cha utoaji wa mimba

Mutoka anasema jamii haijawa na uelewa wa kutosha kuhusiana na tatizo la utoaji wa mimba  hivyo jamii inahitaji elimu ya kutosha kukabiliana na hali hiyo huku umasikini nao ukitajwa kuwa ni chanzo cha utoaji mimba kwa njia isiyo salama.

Anasema mfumo dume pia umechangia wanawake wengi kutoa mimba kutokana na kukosa maelewano ndani ya ndoa na wakati mwingine kukosa uamuzi sahihi.

Madhara ya kutoa mimba

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Vingunguti, Dk Modest Mwinuka anasema wanawake wengi wanaofika hospitalini hapo wanadai kuwa mimba imetoka yenyewe wanaogopa kusema ukweli kwa kuhofia kukosa huduma.

Dk Mwinuka anasema moja wapo ya madhara makubwa ambayo yanampata mwanamke anayetoa mimba vichochoroni ni kutoka kwa damu nyingi na kupasuka kwa kizazi.

“Madhara ya baadaye ni kupata maambukizi katika viungo vya uzazi, kuharibikiwa  mimba kila wakati kutokana na shingo ya kizazi kulegea pamoja na kupata msongo wa mawazo,” anasema Dk Mwinuka.

Anasema kuwa madhara mengi ni kupata shida wakati wa kuzaa kwa sababu shingo ya kizazi inakuwa imepata majeraha, kupata ugonjwa wa Anemia kutokana na kutoka damu nyingi na  pamoja na kupata shida ya kushindwa kupata mimba kutokana na maambukizi katika viungo vya uzazi.

“Vilevile kuna madhara mengine ambayo ni mwanamke kupata ugumba, mimba kutunga nje ya kizazi, kuzaa watoto wasio kuwa na akili nzuri, kupata kansa ya mlango wa kizazi na kuathirika kisaikolojia,” anaongeza.

Muuguzi wa Chama cha Wauguzi nchini (Prinmat), Joseph Siga anasema mfuko wa uzazi una utando maalumu ambao  hufanya mimba iliyotungwa kwenye mirija iitwayo fallopian kuwezesha yai kushuka hadi kwenye mifuko ya uzazi, Lakini utoaji wa mimba huambatana na magonjwa ya mirija hiyo na kupoteza utando huo na kusababisha mimba kukulia nje ya kizazi na  matibabu ya tatizo hilo ni kukata mrija husika husababisha kuongeza hatari ya ugumba.

“Wanawake wanaotoa mimba wana hatari kubwa ya kupata kansa ya mlango wa uzazi kuliko wengine ambao hawajatoa mimba na hii ni kwa sababu ya kusumbuliwa kwa mlango huo kwa dawa za kutoa mimba, vifaa vya kutoa mimba na mabadiliko ya ghafla ya homoni za uzazi,” anasema Siga.

Anasema baadhi ya njia zisizo salama zinazotumika kuwa ni pamoja vyuma vyenye ncha kali kama spoku za baiskeli, mikasi, utomvu wa mti wa muhogo na vidonge

Siga anasema idadi kubwa ya wanaotoa mimba kiholela, hupata madhara mbalimbali ikiwamo kutoboka utumbo, kuchanika kwa kizazi, kuoza na wengine kuharibu figo.

Utafiti uliofanywa mwaka 2011 na Shirika la Afya Dunia (WHO) umeonyesha kuwa msichana mmoja kati ya wanne hutoa mimba kwa njia za kienyeji na kati ya mimba 210 milioni zinazopatikana kila mwaka, 46 milioni sawa na asilimia 22 hutolewa.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa  mwanamke mmoja hufa kila baada ya dakika nane kutokana na matatizo ya utoaji mimba usio salama.

Sheria inasemaje

Ofisa sheria wa kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake nchini (Tawla), Jovin Sanga na Julius Titus wanasema kwa mujibu wa kifungu 150 hadi 152 cha Sheria ya Makosa ya Jinai  kinazuia utaoji mimba wa aina yoyote.

“Kwa mujibu wa sheria adhabu zipo za aina tatu ambazo ni kwanza,  mtu ambaye atamsaidia mwenye mimba kutoa ujauzito huo, atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka 14 jela, kwa mtu ambaye atatoa dawa au vifaa kwa ajili ya kutoa mimba adhabu yake ni kifungo cha miaka  mitatu jela na kwa upande wa mhusika mwenyewe kwa maana ya mwenye mimba akibainika kutoa ujauzito wake mwenyewe atahukumiwa kifungo cha miaka saba jela,” anafafanua  Titus.

Titus anasema Sheria ya Makosa ya Jinai kifungu 230 kinaruhusu  utoaji wa mimba kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama pekee endapo atapewa ruhusa kwa kibali maalumu cha daktari.

“Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sehemu ya tatu ibara 14 inaeleza bayana kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria,” anasema Sanga.

Nini kifanyike?

Wadau mbalimbali wa masuala ya afya, wamependekeza  Serikali itunge sheria mpya ambayo itasaidia suala la utoaji mimba liwe la kisheria ili vifo vinavyotokana na masuala ya uzazi vipungue.

Mutoka anasema nchi zilizoruhusiwa utoaji mimba kwa wanawake zina idadi ndogo ya vifo vinavyotokana na uzazi pia zina kiwango kidogo cha utoaji mimba  kwa njia salama kwa sababu jamii imepata elimu ya kutosha tofauti na nchi ambazo hazijaruhusu utaoji wa mimba, zimekuwa na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na masuala ya uzazi.

“Ukibana sheria, unaruhusu utoaji mimba usio salama na ukiruhusu sheria hiyo vifo vinavyotokana na masuala ya uzazi vitapungua, kwani utoaji mimba kwa njia salama unamfanya mwanamke kuwa salama zaidi lakini kwa utoaji mimba usiofuata njia salama una muweka mwanamke katika hatari ya kupata magonjwa na pengine kifo,” anaongeza.

Maoni au maswali tuma afya@mwananchi.co.tz au 0713247889

-->