Utu wa Mtanzania ulivyo shakani

Muktasari:

  • Kinachoonekana sasa ni ubinadamu kumezwa na ‘ubwanadamu’ kutamalaki
  • Mwandishi maarufu wa Marekani Richard Wright aliwahi kuandika: “Hatari inayoukabili ulimwengu wa leo ni kusahau kile kiainishacho ubinadamu wetu.”

Naanza kupata shaka kuwa sasa huko tunakoelekea, siasa, dini, ukabila na tofauti ya kiuchumi, vinaweza kutugawa, tukasahau utu wetu kama Taifa.

Kinachoonekana sasa ni ubinadamu kumezwa na ‘ubwanadamu’ kutamalaki

Mwandishi maarufu wa Marekani Richard Wright aliwahi kuandika: “Hatari inayoukabili ulimwengu wa leo ni kusahau kile kiainishacho ubinadamu wetu.”

Kuna mambo yanayopaswa kujadiliwa kisiasa, kiitikadi, kisera na kifalsafa. Aidha, kuna masuala mengine yanapaswa kujadiliwa pasipo na chembechembe zozote za kisiasa.

Kwa mfano, mambo yanayohusu utu na haki ya binadamu, yanafaa yajadiliwe katika mizani ya utaifa na uzalendo. Kuchanganya mambo hayo mawili ni kuonyesha ujinga wa wazi wazi tulio nao.

Historia ya taifa hili imejengwa katika misingi ya kuthaminiana, kuheshimina na kuvumilina katika mazingira tofauti tofauti.

Si vema kuvunja misingi hiyo na kujenga misingi mingine ya chuki, uovu, visasi, husda na kutothaminiana kama Watanzania.

Viashiria vyovyote vya kuvunja sifa nzuri za Taifa hili vinatakiwa kukemewa na kudhibitiwa ipasavyo kabla havijaleta maangamizi makubwa zaidi.

Viongozi wengi wa nchi nyingi duniani kwa sasa wanatumia nguvu kubwa kuisaka Amani.

Nchi hizo zilishatumbukia katika adha ya mateso; ardhi zao zinatapakaa damu za wasio na hatia.

Ni kazi ya kila Mtanzania kuilinda amani kuliko kusubiri ipotee halafu tuje kuaanza kuitafuta; tutakuwa tumechelewa.

Kuna ishara ndogo ndogo mithili ya tone la maji zinazoonyesha Watanzania wengi tumekuwa watu tusiothaminiana tena.

Mtanzania mwenzetu anaweza kupatwa na tatizo likaonekana ni jambo “lao” siyo letu. Ni suala la chama X, au suala la watu fulani.

Tumeruhusu mbegu hii kupata ardhi ya rutuba na kumea. Kama haitoshi, viongozi walio na jukumu la kulinda amani ya nchi hii, wapo baadhi waliomua kuipalilia, matunda yake yataliangamiza Taifa; yataleta majuto na kubadilisha historia ya nchi hii.

Utu ni tabia ya kiungwana ya kusaidiana pale panapotokea matatizo, tabia hiyo ni sifa ya utu wema, ni utanzania na uzalendo.

Tumeshashuhudia matukio mengi ya kuogofya nchini, ambayo hayakuwa desturi yetu kama vile watu kupotea, kupigwa risasi, kutekwa, kuteswa na kuuawa.

Haiyumkiniki matukio haya kutopewa uzito unaostahili katika kuyashughulikia kwa kuwa yanawahusu Watanzania wenzetu.

Hatari kubwa zaidi ni kuona hadhi na heshima ya ubinadamu inashuka, huku kibaya zaidi kikiwa ni kuona wapo baadhi yetu wanaoyapigia makofi matukio hayo ya kikatili.

Wajibu wetu kama taifa bila kujali itikadi yoyote au nyadhifa za kisiasa,ni kusimama pamoja, kukemea na kupinga kila aina ya madhila yanayotokea kwa mmoja wetu. Katu tusiyapa kibali cha kuishi matukio haya kwenye ardhi yetu.

Lazima tuwe na bidii na shabaha moja katika kulinda utu na uhai wa kila mmoja wetu. Uhai wa Mtanzania mmoja popote pale alipo nje ya nchi au ndani una thamani kubwa.

Kama tutashindwa kumtetea mmoja wetu aliye katika matatizo, maendeleo ya kujali utu yatakuwa shakani.Kipimo cha utu wetu kitakuwa si utu tena bali ukatili na ‘ubwanadamu’

Ndoto yangu ni kuona ustawi wa taifa, haki, uzalendo, na heshima ya utu na ubinadamu.

Tusimame kuonyesha thamani ya asili ya damu ya Mtanzania; hayo ndiyo yanafaa kuwa matamanio ya kila Mtanzania.

[email protected] +255769735826