Uwajibikaji wa pamoja unatakiwa ili kuwadhibiti wahamiaji haramu

Muktasari:

  • Hivyo, hali hii inaashiria kuwa mazingira kama haya ni tishio kwa usalama wa nchi kwa kuwa makundi hayo yanaingia kupitia njia za panya na inasaidikika baadhi yao wanahusika kuingiza silaha za kivita zinazokamatwa maeneo mbalimbali ya nchi zikiwa zimefanya uhalifu ama bado.

Karibu kila siku hukosi kusikia taarifa za kukamatwa kwa wahamiaji haramu maeneo mbalimbali nchini. Hii ni dalili kuwa kuna udhaifu wa ulinzi katika mipaka yetu.

Hivyo, hali hii inaashiria kuwa mazingira kama haya ni tishio kwa usalama wa nchi kwa kuwa makundi hayo yanaingia kupitia njia za panya na inasaidikika baadhi yao wanahusika kuingiza silaha za kivita zinazokamatwa maeneo mbalimbali ya nchi zikiwa zimefanya uhalifu ama bado.

Kasi hiyo inatutaka sasa tuwe na uwajibikaji wa pamoja wa wizara za Ulinzi; Mambo ya Ndani na Maliasili ili kudhibiti tishio kubwa la usalama wetu na maliasili za Taifa.

Watu hawa kuendelea kupita kila kukicha si afya njema kwa nchi. Rais John Magufuli wakati anazindua hati za kusafiria za kielektroniki, alisema kwa uchungu na kuagiza wahusika kuchukuliwa hatua kutokana na kukithiri kwa matukio ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu nchini.

Pia, alimtaka kamishna wa Uhamiaji kuwachukulia hatua maofisa wa mikoa itakayobainika wahamiaji haramu kuingilia.

Hata hivyo, kasi ya wahamiaji kutoka nchi mbalimbali hususan Ethiopia na Sudan inaonekana.

Baadhi ya watu wanasema hali hiyo inakithiri kwa madai wana wenyeji wao ambao ni Watanzania wanaojua udhaifu wa ulinzi wa mipaka na namna ya kupenya wakiwa na silaha.

Hata kama kamishna wa Uhamiaji ataamua kutekeleza agizo la Rais la kuwachukulia hatua maofisa wa mikoa, atawawajibisha wote na hakutakuwa na suluhu ya tatizo kama uwajibikaji wa pamoja hautakuwapo, kwa kuwa tatizo halipo kwa maofisa wa uhamiaji pekee, bali ulinzi wa mipaka yetu.

Hii maana yake ni kwamba maofisa Uhamiaji wanajikita zaidi kwenye mipaka ya kisheria ambako kundi hilo halipiti na wanatumia njia za pembeni ambazo udhibiti wake umeonekana ni dhaifu.

Hivyo ni lazima tukubali kujipanga vizuri ili kudhibiti tatizo hili na kikubwa ni kuongeza uwajibikaji wa pamoja kati ya wizara za Mambo ya Ndani; Ulinzi pamoja na ile ya Maliasili kwa kuwa wahamiaji haramu hao ndiyo wanaohusika pia na ujangili wa wanyamapori.

Pia, ni miongoni mwa makundi yanayohusika na uingizaji wa silaha hapa nchini ambazo zimekuwa zikinaswa wakati mwingine zikiwa zimetumika kufanyia uhalifu na ujangili.

Ongezeko la wao kuingia na wakati mwingine kukutwa wakiwa na mavazi ya asili ya Kimasai, kwa maana nyingine linaonyesha kuwa mtandao wao unazidi kutanuka ndani ya jamii. Hivyo kuna kila sababu ya kuijengea jamii uelewa juu ya athari za kuwaficha wahamiaji hao kwa usalama wao.

Kwa sababu kuwakamata kila siku wakiingia nchini bila kuweka mikakati ya kuwadhibiti wasiingie, ni tatizo kubwa.

Umefika wakati sasa kwa kila Mtanzania kuwajibika kudhibiti uvunjifu wa sheria za nchi.

Tishio lingine ni jinsi silaha zinavyokamatwa ndani ya nchi na nyingi zikibainika ni kutoka nje na mara zote hutumika kufanyia uhalifu ikiwamo kwenye hifadhi za Taifa na mapori ya akiba.

Historia ya ukamatwaji wa silaha hizo inaonyesha nyingi hutokea nchi jirani ambako kuna mapigano ya mara kwa mara.

Hivyo, kama Taifa huru lazima tutambue kuwa tuna maadui wa kisiasa na kiuchumi na wapo ambao wanaweza kutumia mwanya huo wa uingizaji wa wahamiaji haramu kuja kufanya matukio makubwa yatakayoliletea Taifa hasara kubwa kiuchumi na kisisa.

Binafsi nasema kasi lazima iongezwe katika udhibiti wa wahamiaji haramu kuanzia ngazi ya vitongoji.

Yeyote atakayemtilia shaka mtu katika eneo lake analoishi, ni vyema atoe taarifa kwa vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.