Uzito wa mwili unavyoweza kuwa afya au kifo chako

Muktasari:

  • Kuna athari za kiafya kwa mtu kuwa na uzito chini ya kiwango yaani kuwa na uwiano wa uzito na kimo (body mass index/BMI) sawa na 18.5 au chini ya hapo.

Tatizo la uzito kupita kiasi ni la kawaida duniani kote.

Wataalamu wengi wa afya wamekazia fikra katika kutatua tatizo la uzito kupita kiasi, ili kuwasaidia watu wasipatwe na maradhi kama kisukari, kupanda kwa shinikizo la damu, kiharusi na saratani.

Kuna athari za kiafya kwa mtu kuwa na uzito chini ya kiwango yaani kuwa na uwiano wa uzito na kimo (body mass index/BMI) sawa na 18.5 au chini ya hapo.

Uwiano wa Uzito na Urefu/Body Mass Index (BMI) ni njia nzuri ya kuangalia kama uzito wako upo katika afya njema.

BMI hutumika kutathmini hali ya lishe ya mtu yeyote na ni muhimu katika kugundua mapema baadhi ya matatizo ya kiafya na kilishe na hivyo husaidia watoa huduma za afya kuweza kutoa ushauri ipasavyo kwa wateja wao.

BMI kati ya 18.5 na 24.9: Huonyesha mipaka ya afya njema. Huonyesha uzito wako unaendana na kimo chako kiafya. Unaweza ukawa na BMI nzuri lakini bado ukawa na mafuta kuzunguka tumbo kitu kinachoweza kukuongezea hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo, Kisukari Aina ya pili na Kiharusi.

Hivyo kupima kiuno ni njia nzuri kuangalia kama una mafuta ya ziada kuzunguka tumbo lako.

Ili kupima kiuno, tafuta mbavu ya mwisho na juu ya nyonga na zungusha futi yako katikati ya mbavu ya mwisho na nyonga. Inashauriwa kutoa pumzi nje kabla ya kupima.

Bila kujali kimo au BMI, unapaswa kupunguza uzito ikiwa kiuno chako ni sentimeta 94 au zaidi kwa wanaume au sentimeta 80 au zaidi kwa wanawake.

Uzito uliozidi

BMI kati ya 25.0 na 29.9: huonyesha umezidi mipaka ya kawaida, inayomaanisha uzito wako umezidi kawaida (Over Weight). Pia, inamaanisha wewe ni mzito zaidi kuliko mtu mwenye afya njema kwa kimo chako. Uzito uliopita kawaida unakuweka katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo, Kiharusi na Kisukari aina ya pili.

BMI ya 30 na zaidi: inachanganuliwa kama uzito kupita kiasi au kiriba tumbo (Obesity). Kuwa na uzito kupita kiasi, kunakuweka katika hatari zaidi ya matatizo ya kiafya kama magonjwa ya moyo, Kiharusi na Kisukari aina ya pili.

Utafiti wa aina mbalimbali umethibitisha kuwa mtu kuwa na uzito pungufu, huongeza hatari ya kifo. Hii ni kwa mujibu wa profesa wa jerontolojia (tanzu ya elimu inayohusu uzeekaji) Kay-Tee Khaw kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge cha nchini Uingereza.

Hatari ya kifo cha haraka hutokana na mambo mengi. Baadhi ya sababu zinazofanya mtu kufa haraka ni kushuka kwa kinga ya mwili na kupatwa kirahisi na maradhi yanayodhoofisha mwili kama saratani.

‘’Mifupa na nyama za mwili huchangia sana kwenye uzito wa mtu. Kuwa na uzito pungufu huweza kumaanisha mifupa imedhoofu na kukosa nyama za kutosha hasa katika umri mkubwa, ‘’anasema Profesa Khaw.

Watu wembamba kiasili wanaweza kufikiri wanaweza kula vyakula vyovyote, kuvuta sigara na kutofanya mazoezi kwa kudhani wana afya bora wakijilinganisha na watu wanene, kitu kinachoweza kuhatarisha afya.

Je, unataka kuongeza uzito?

Ikiwa wataka kuongezeka uzito/unene kwa kuhisi wewe ni mwembamba au uwiano wa kimo na uzito (BMI) ni chini ya 18.5, unapaswa kujua njia bora za kufuata ili kufikia lengo bila kuathiri afya.

Unapaswa kuongeza vyakula vyenye virutubisho vingi kama vyakula vyenye mafuta kama mafuta ya mzeituni, maparachichi, karanga, samaki wenye mafuta, mtindi na jibini.

Ili kuongeza uwezekano wa kunenepa na kuongeza uzito, mtu anapaswa kula milo mikuu mitatu na midogo miwili.

Hupaswi kula vyakula vya aina moja tu, kwa maana unaweza kuathiri afya. Mtu anapaswa kula vyakula vingine pia kama matunda, mboga za majani, nafaka, jamii za kunde na vyakula vya protini.

Ulaji wa vyakula vya protini husaidia kukarabati na kujenga nyama za mwili. Kufanya mazoezi ni muhimu kwa ajili ya kujenga uzito wa mwili.

Mazoezi ya kujenga stamina mfano kubeba vitu vizito huimarisha misuli na mifupa na kufanya iwe na uzito mkubwa.

Mazoezi pia huchochea hamu ya chakula kwa kukufanya uhisi njaa, hivyo kukusaidia kula vyakula vyenye kalori nyingi kama wanga ili kupata nguvu.

Ikiwa umejaribu njia hizi na bado hujafanikiwa kuongeza uzito/unene kama ulivyotarajia, ni vyema kuzungumza na daktari au mtaalamu wa lishe.

Inawezekana ukawa na ugonjwa ambao haujabainika kama vile ugonjwa wa tezishingo unaozuia kuongezeka uzito.