Vijana lazima waifahamu sera ya maendeleo inayowahusu

Muktasari:

  • Mipango iliyomo kwenye sera hiyo kama ingetumiwa ipasavyo naamini ingepunguza tatizo la ajira kwa vijana na ingegusa maisha yao wote hata waliopo vijijini.

Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 katika sura ya nne imeainisha malengo 13, ikiwamo mipango mizuri ya ajira au kujiajiri kwa vijana.

Mipango iliyomo kwenye sera hiyo kama ingetumiwa ipasavyo naamini ingepunguza tatizo la ajira kwa vijana na ingegusa maisha yao wote hata waliopo vijijini.

Badala yake kila kilichomo kingefanywa kwa vitendo kama inavyoelekeza, majibu ya maswali yao yangepatikana huko huko vijijini.

Kwa bahati mbaya sera hii imebaki makabatini na vijana wa vijijini wanazidi kuchukia kubaki huko na kukimbilia mijini wakidhani watapata majibu ya maswali na changamoto zao, ikiwamo ajira.

Baadhi waliokomaa na kubaki vijijini wakilima wanakutana na changamoto kila kukicha ikiwamo kukosa masoko ya bidhaa zao na mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa.

Ukiachilia mbali changamoto hizo, zipo pia za kutokuwa na teknolojia ya kilimo inayowasababisha kuendelea kulima kilimo kisicho na tija na kubaki pale pale licha ya kupoteza nguvu nyingi juani.

Kutokana na kupuuzwa kwa utekelezaji wa sera hiyo vijana wanaendelea kuwa masikini zaidi wakiwa vijijini kutokana na kutomilikishwa ardhi.

Hizo ni baadhi ya sababu zinazowafanya vijana wakimbilie mijini kutafuta maisha au ajira ambazo kwa bahati mbaya hata wanakokimbilia ni changamoto pia.

Kwa mujibu wa Takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zilizotolewa mwaka 2016 kuhusiana tatizo la ajira kimataifa, zilionyesha kuwa eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, tatizo la ukosefu wa ajira liko kwa asilimia 7.4.

Kiwango hiki kinatofautiana na wastani wa kawaida wa ukosefu wa ajira kwa ngazi ya kimataifa, kwa mujibu wa Ripoti ya Mwelekeo wa Mtazamo wa Ajira Kijamii ya ILO kwa mwaka 2017, iliyotolewa mwaka 2016.

Ripoti hiyo ilitaja wastani wa kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia 5.8 kwa mwaka 2017 kutoka asilimia 5.7 kidunia za mwaka 2016.

Asilimia 5.8 ya kiwango cha ukosefu wa ajira kwa mwaka 2017 ni sawa na idadi ya watu milioni 3.4 inaonyesha kuwa watu wasio na ajira duniani ni zaidi ya milioni 201.

Inakadiriwa kuwa hadi vijana milioni moja wanaingia katika soko la ajira kila mwaka hapa nchini, lakini miongoni mwao ni vijana kati ya 150,000 na 200,000 ndio wanaopata ajira kwenye utumishi wa umma ama sekta binafsi.

Ili kuonyesha bado tatizo la ajira ni kubwa hapa nchini hata matokeo ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mwaka 2014 kuhusu watu wenye uwezo wa kufanya kazi ni watu milioni 22. 3.

Wanaume wakiwa milioni 11 na wanawake ni milioni 11.2, huku idadi ya Watanzania walio nje ya nguvu kazi ya taifa wakifikia milioni 3.4.

Waathirika wa tatizo hilo kwa kiasi kikubwa ni vijana kama ilivyo kwa nchi nyingi.

Hii inaonyesha au inakumbusha umuhimu wa kuitendea haki sera ya maendeleo ya vijana kwa kuyafanyia kazi mambo muhimu iliyoainisha ambayo huenda yakasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Vijana wenyewe wana jukumu pia la kuisoma sera hiyo, kuielewa na kudai vilivyomo kwa kufanya mijadala na makongamano mbalimbali ambayo yatawafikia wahusika na wataona umuhimu wa kuyafanyia kazi.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa baruapepe