Viongozi TFF, Watanzania wana kiu ya mafanikio

Muktasari:

  • Kila mmoja ameyapata matokeo na viongozi wameshapatikana kwa Wallace Karia na Michael Wambura kupewa jahazi la kuongoza soka la Tanzania kwa kipindi hicho. Kazi kubwa ya wajumbe ilikuwa ni kuusimika uongozi mpya na sasa wamepatikana baada ya safari ndefu iliyoanza Juni mwaka huu, kuanzia kuchukua na kurudisha fomu, usaili na kampeni.

Mwishoni mwa wiki, mji wa Dodoma ulikuwa katika pilikapilika za uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambako lilipata viongozi wa kuongoza taasisi hiyo kwa miaka minne ijayo.

Kila mmoja ameyapata matokeo na viongozi wameshapatikana kwa Wallace Karia na Michael Wambura kupewa jahazi la kuongoza soka la Tanzania kwa kipindi hicho. Kazi kubwa ya wajumbe ilikuwa ni kuusimika uongozi mpya na sasa wamepatikana baada ya safari ndefu iliyoanza Juni mwaka huu, kuanzia kuchukua na kurudisha fomu, usaili na kampeni.

Kimsingi, walioshinda wakumbuke kuwa wana madeni ya ahadi zao na wana jukumu kubwa la kumaliza kiu ya Watanzania ambao waliwaamini kupitia wajumbe wa uchaguzi huo na kuchaguliwa kuiongoza TFF.

Hatutaki kurejea yaliyofanyika, ila tunasema, uchaguzi umekwisha sasa tunataka kuona kilichoahidiwa na wagombea kinachukua nafasi yake.

Kwa muda mrefu sasa, Watanzania wanataka kuona soka ikipiga hatua, lakini wamekatishwa tamaa na ubabaishaji na mipango yetu mibovu. Kumekuwa na mipango mingi ya maendeleo ya soka, lakini haina mwendelezo.

Tunawaambia wale walioingia madarakani kwamba kuna mambo mengi yaliyo mbele yao, lakini haya machache wanaweza kuyaangalia zaidi;

Mosi, soka la vijana. Huko ndiko kwenye chimbuko. Kinachotakiwa ni kuanza upya, kufufua michuano kama ya Copa-Coca Cola iliyokuwa na mtiririko mzuri wa kupata wachezaji kuanzia ngazi za vijiji hadi taifa, kuboresha mashindano ya U-20 na mengine ya vijana chini ya utaratibu wa TFF.

Pili ni eneo la wadhamini. Viongozi wa TFF, inatakiwa kuunda kamati ya kusimamia/kutafuta wadhamini kwa ajili ya Ligi Kuu.

Ligi ikiwa na wadhamini wengi, klabu zitafaidika na itakuwa faida zaidi kwa klabu zenye wadhamini binafsi. Hivi sasa Ligi Kuu ina mdhamini wake, Kampuni ya Vodacom na wadhamini wachache, kazi ya uongozi ni kutafuta wengine ili kuongeza msisimko.

Mbali na hilo, lakini pia kuboresha muundo wa uendeshaji wa ligi, ili iwe na msisimko zaidi. Wanapaswa kuangalia wapi pa kufanyia maboresho ili kuwa na ligi yenye mvuto.

Eneo la tatu; tunaweza kuliangalia hili la usimamizi na uendeshaji wa timu za Taifa, kuanzia U-17 hadi Taifa Stars. Kuwepo na wasimamizi wa kila eneo. Wasimamizi wa timu moja wanaweza kubadilishwa, ikiwa timu moja haina majukumu makubwa. Itapendeza zaidi endapo Taifa Stars itakuwa na usimamizi unaojitegemea kulingana na majukumu yake.

Usimamizi wa timu za Taifa, utawafanya wahusika kuwa na mwelekeo mmoja tu wa timu ikiwamo kubuni mikakati na mipango ya kuendeleza timu inapokaribia au kuwa na mechi za kimataifa.

Eneo la nne na mwisho ni hili la viongozi walioingia TFF kutambua uwepo wa Zanzibar. Hivi karibuni, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilifuta nafasi ya Zanzibar kuwa mwanachama wa 55 wa CAF.

Kutokana na hali hiyo, jukumu zima imepewa TFF, sasa viongozi hawa wasiiache, waangalie jinsi watakavyoivusha katika medani ya soka.

Yako mengi ya kutekeleza lakini kwa hayo machache na mengine watakayopanga, tunaamini yataisogeza Tanzania kufika mahala katika soka, kwa kuzingatia misingi na katiba inayoliongoza shirikisho hilo. Watanzania wana kiu ya mafanikio ya soka.