Viongozi waongeze uwajibikaji kwa wananchi wao

Muktasari:

  • Mabango mengi yamekuwa yakionyesha kero zao kutopatiwa ufumbuzi kwa wakati hasa katika ngazi za vijiji, kata na wilaya na hata mkoa.
  • Huu ni udhaifu katika utendaji kwani inadhihirisha wazi daraja limeanza kukatika kati ya baadhi ya watendaji wenye mamlaka ya uamuzi na wananchi.

Katika siku za karibuni, imekuwa ni kawaida kuwaona wananchi wakiwapokea viongozi wa kitaifa wakiwa na mabango kuelezea kero zao.

Mabango mengi yamekuwa yakionyesha kero zao kutopatiwa ufumbuzi kwa wakati hasa katika ngazi za vijiji, kata na wilaya na hata mkoa.

Huu ni udhaifu katika utendaji kwani inadhihirisha wazi daraja limeanza kukatika kati ya baadhi ya watendaji wenye mamlaka ya uamuzi na wananchi.

Jambo hili, siyo tu linawagusa watendaji wa Serikali, bali hata wa vyama vya siasa na mashirika mbalimbali nchini.

Hivi sasa viongozi wengi wa ngazi za vijiji, kata na wilaya, hawakutani na wananchi kusikiliza kero zao kwa wakati.

Hata wale viongozi wanaokutana na wananchi katika ofisi zao wamekuwa wakishindwa kutatua kero za wananchi maskini.

Viongozi hawa wanashindwa kutatua kero hizo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo hofu, kutojiamini, kutaka kukiuka sheria na wengine kujali itikadi za siasa.

Hivyo, mazingira haya yanawaathiri, wananchi maskini, wengi na baadhi yao wamejikuta katika migogoro kama ya kuporwa ardhi, mali na wengine kukamatwa na kufungwa.

Kuna wafugaji wanaomiliki maeneo yao kisheria lakini yamevamiwa na wakulima, pia kuna maeneo ya kilimo yamevamiwa na wafugaji bila ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

Katika mazingira haya ndiyo, sababu inakuwa ni kawaida sasa, viongozi wa kitaifa kupokewa kwa mabango ya kero za wananchi hata zile ambazo zingeweza kumalizwa ngazi ya kijiji, kata au wilaya.

Baadhi ya viongozi wa Serikali hivi sasa wanashindwa kufanya uamuzi sahihi kutokana na sababu za kisiasa tu, pale ambako mlalamikaji anakuwa ni mwanachama wa chama fulani.

Naamini mtazamo huu siyo ambao Rais John Magufuli amekuwa akihubiri hadharani, Serikali yake ni ya Watanzania wote bila kujali itikadi zao, rangi, kabila wala dini.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara mkoani Arusha ambako alipokewa kwa mabango ya kero za wananchi.

Kwa busara zake, Waziri Mkuu aliagiza kuyasoma mabango yote na kufuatilia baadhi na kuchukua hatua au kuyatolea matamko.

Miongoni mwa malalamiko katika mabango hayo yalikuwa ni kutotatuliwa migogoro ya ardhi, kutopatikana huduma bora za afya, wizi wa watoto katika hospitali na ukiukwaji wa taratibu.

Hata hivyo, baada ya kutatua baadhi ya kero, Waziri Mkuu katika majumuisho ya ziara yake, pia alionyesha kukerwa na tabia ya viongozi kutotatua kero za wananchi hadi kufika na mabango kwake.

Waziri Mkuu alisema wazi ukiona wananchi wanasubiri viongozi wa kitaifa ndiyo watoe kero zao ina maana waliopewa nafasi ya kutatua kero hizo ngazi za chini wameshindwa.

Nakubaliana na Waziri Mkuu . Kutosha kwa kiongozi ni pale anapokuwa na uwezo wa kushirikiana na wananchi kutatua kero zao ili waishi maisha bora.

Hivyo, viongozi wa umma wanapaswa kuwajibika zaidi kwa wananchi kwani ndiyo wao wamewaweka madarakani ili kuwaongoza.

Hivi karibuni, akiwa katika utaratibu wake wa kawaida, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alifanya ziara wilayani Karatu kusikiliza kero za wananchi.

Katika mikutano aliyofanya Karatu, pia kulikuwa na mabango. Akiwa katika Kijiji cha Rotia, kuna mwananchi alikuwa na bango akimlalamikia ofisa maliasili na mazingira kutotimiza wajibu wake.

Wengine walilalamikia kero ndogo ndogo ambazo zingeweza kushughulikiwa na ama wenyeviti wa vijiji, watendaji wa vijiji, kata, madiwani au mkuu wa wilaya.

Mfano katika Kijiji cha Lositete, wananchi walilalamika kutokuwa na ofisa mtendaji wa kijiji mwenye sifa kwa miaka tisa na nafasi hiyo inakaimiwa na mwanakijiji mwenzao.

Kero kama hii inasikitisha kwani katika eneo hilo, kuna diwani, kuna mtendaji wa kata, kuna watendaji wa halmashauri na kuna mkuu wa wilaya husika.

Baada ya wananchi kutoa kero hiyo, papo hapo aliteuliwa mwalimu wa shule kukaimu nafasi hiyo na kutolewa ahadi hivi karibuni kuwa atapelekwa ofisa mtendaji.

Ni ukweli ulio wazi kwamba, Rais, Waziri Mkuu, mawaziri au wakuu wa mikoa, hawezi kutatua migogoro ya vijiji kwani “siyo hadhi yao”.

Itoshe kutoa wito kwa watendaji wa Serikali, kuwajibika kwa wananchi na kuhakikisha wanatenda haki na kufuata sheria. Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki viongozi wetu watimize wajibu wao.

Mussa Juma ni mwandishi mwandamizi gazeti la Mwananchi Mkoa Arusha. 0754296503 email [email protected].