Vyakula vya watoto wenye udumavu vipo, tutafakari

Muktasari:

  • Kauli hiyo aliitoa baada ya kubaini mkoa huo unatatizo la udumavu na utapiamlo mkubwa kwa watoto.

        Mapema wiki hii, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Rukwa kuhakikisha unapambana kutokomeza udumavu kwa watoto unaosababishwa na ukosefu wa lishe.

Kauli hiyo aliitoa baada ya kubaini mkoa huo unatatizo la udumavu na utapiamlo mkubwa kwa watoto.

Lakini wataalamu wa Lishe wanasema mtoto asiyepata lishe yenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya vyakula tangu siku ya kwanza mbegu ya uzazi inapotungwa hadi siku ya 1,000, hali yake ya kiafya huzorota. Wanasema udumavu wa lishe si urefu wala ufupi, ni akili. Na Taifa lolote lenye wadumavu haliwezi kupiga hatua.

Hivyo, ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha anatokomeza hali ya udumavu na utapiamlo.

Ripoti na machapisho mbalimbali ya Huduma ya Mama na Mtoto yanaeleza mtoto anapozaliwa, utumbo wake huwa hauna uwezo wa kusaga vyakula vigumu vya aina yoyote ile zaidi ya maziwa ya mama yake.

Ndiyo maana inasisitizwa mama amnyonyeshe mtoto kwa miezi sita mfulullizo bila kumpatia chakula kingine huku naye akisisitizwa kupata vyakula bora kwa lengo la kulinda afya yake na ya mwanawe.

Hivyo, kauli ya Naibu waziri imekuja wakati muafaka, kwani tatizo la udumavu na utapiamlo linaonekana kushika kasi nchini hasa kwenye mikoa yenye neema ya vyakula. Wazazi na walezi licha ya kulima mazao ya aina tofauti na kufuga mifugo midogo na mikubwa, lakini wao hutoa kipaumbele cha kuuza na kusahu kutoa lishe bora kwenye familia zao.

Ili kuondokana na kadhia hii, kama kaya inalima vyakula vinavyosaidia kupatikana kwa lishe, ielimishwe namna ya kuvitumia.

Wataalamu wa Lishe wanasema kula chakula bora kunamaanisha kula vyakula vya aina tofauti yakiwamo matunda, mboga, maziwa na aina ya vyakula vyenye asili ya wanyama wa kufuga kama kuku, mbuzi, ng’ombe, samaki na vyakula vya nafaka na ukichunguza, hivi vyote vinapatikana kwenye familia zetu.

Kwa mfano mkoani Iringa, Mkoa wenye neema ya vyakula lukuki lakini takwimu za Tanzania Demographic Health Survey(TDHS) za mwaka 2016/17, zinaonyesha takribani nusu ya watoto Mkoani humo ni wadumavu kwa asilimia 41.6. Mkoa huo una jumla ya watoto 29,825 walio chini ya miaka mitano.

Hivi karibuni, Kaimu Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoani Iringa, Rwosita Msangi alisema watoto wanaozaliwa wakati wazazi wao wananyonyesha, wako kwenye hatari ya kupata utapiamlo na udumavu kutokana na maandalizi duni ya lishe wanayopatiwa na wazazi wao.

Kuna ujinga unaoendelea huko mitaani, baadhi ya wazazi hupotoshana, wanadai eti mama akiwa na ujauzito huku ananyonyesha, maziwa yake yanachacha hayafai kumnyonyesha mtoto.

Hiyo ni dhana potofu, mama huamini hilo na kuacha kumnyonyesha mtoto na matokeo yake mtoto huyo hudumaa na kupata utapiamlo kwasababu anakosa lishe yenye virutubisho.

Kwa upande mwingine, tatizo hili linasababishwa na watu kushindwa kupanga uzazi pia.

Ifike mahala sasa, elimu juu ya lishe bora na ya uzazi wa mpango isisitizwe kama ilivyo elimu kwa masuala mengine.

Hii itasaidia jamii kutambua lishe bora ni ipi na umuhimu wa kutumia njia za uzazi wa mpango ili kuepuka matatizo kama haya ya utapiamlo na udumavu yanayowapata watoto. Kwani takwimu za Baraza la Afya Duniani zinaonyesha katika kila watoto watano wenye umri chini ya miaka mitano nchini, wawili wamedumaa. Watanzania tubadilike, wataalamu wa Tiba lishe waielimishe jamii namna ya kuandaa vyakula na ulaji bora. 0713235309

Ingawa kati ya mwaka 1992 hadi 2014 kiwango cha udumavu nchini kilipungua kwa asilimia 30, lakini idadi ya watoto waliodumaa imeongezeka kutoka milioni 2.4 hadi milioni 2.7 katika kipindi hicho.

Shirika la Afya la Dunia (WHO) nalo linaonyesha kila siku, zaidi ya watoto 270 wenye chini ya miaka mitano hupoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya lishe duni.

Watu hasa vijijini, wasione haya kula unga wa dona ambao unavirutubisho vingi wala kula mboga za Majani kila siku au maharagwe, hivi ni miongoni mwa vyakula vyenye lishe bora.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo alipozungumza na wakuu wa mikoa ya Tanzania Bara Desemba 19, 2017, juu ya suala la lishe, alisema Serikali katika mwaka wa fedha 2017/18, imetenga Sh11 Bilioni kwa ajili ya kufanikisha suala la lishe, ikimaanisha kila mtoto ametengewa Sh 1,000.

Umefika wakati sasa kwa Serikali kupitia Serikali za mikoa kulisimamia hili ili kumaliza tatizo la utapia mlo na udumavu nchini.