Mwananchi -

Vyombo vya habari vinatoa mwanga uletao wepesi wa kufikiri

Friday February 9 2018Ndimara Tegambwage ni  Mhariri Meza ya wa Jamii

Ndimara Tegambwage ni  Mhariri Meza ya wa Jamii 

Kutoka Meza ya Mhariri wa Jamii

Wasomaji wawili wa gazeti hili ndio wachangiaji wakuu wa maoni katika safu hii leo. Mmoja ni Mgengeli Deo anayeuliza: “Nimekuwa nikiona habari na picha za washindi au waliofanya vizuri katika mitihani ya ‘kumaliza masomo.’

“Je, mbona hatuoni picha za watu waliofanya vibaya? Hamuoni kuwa mnafanya upendeleo na kuninyima haki yangu kikatiba ya kupata habari; na kufanya kosa la kuleta habari za upande mmoja?”

Mwingine ni Noor Shija anayechangia mjadala juu ya matumizi ya cheo au sifa ya mtu katika kuandika vichwa vya habari kama ilivyoandikwa katika gazeti hili toleo la 8 Januari 2018.

Kichwa hicho kinasomeka hivi: ‘Jinsi mhasibu alivyomuua mkewe, mtoto na shemeji yake.’ Hiki kilipingwa na msomaji Richard Mgendi.

Hoja za Richard na ufafanuzi wa Mhariri wa Jamii vilibebwa na kichwa cha habari kisemacho, ‘Kazi, cheo ni vifafanuzi vya kumtambulisha mtuhumiwa lakini havitendi kosa.’

Tuanze na hoja ya Mgengeli Deo kuhusu kutotangaza wanaofeli. Mhariri wa Jamii aliomba wahariri watatu wa gazeti hili kutoa maoni binafsi juu ya hoja hiyo.

Fidelis Butahe ambaye ni mmoja wa wahariri wa gazeti hili anasema, “Kutoanika walioshindwa kunalenga kutowavunja moyo; kwani lengo la kwenda shule ni kujifunza na kufaulu; na siyo kufeli…”

Esther Mvungi, mmoja wa wahariri wa gazeti hili amesema, “…kutangaza aliyeshindwa, tena kwa picha, hakumsaidii; kunamfanya azidi kudidimia; na labda kunyong’onyea zaidi hata kama angekuwa na nia na uwezo wa kuibuka.”

Rashid Kejo ambaye ni msanifu mkuu wa gazeti hili anasema, “Hilo nalo ni wazo (kutangaza waliofeli mmojammoja). Lakini ni wengi mno. Chukua mfano wa shule moja mkoani Njombe ambako imetangazwa kuwa wanafunzi wote wa Kidato cha Nne wamefeli.”

Unahitajika upekuzi wa kina na muda mrefu, anasema Kejo, “kujua waliofeli na kupata alama ‘F’ za chini zaidi nchini kote. Hata hao waweza kukuta ni 50 au 100, au 500 au zaidi; na huwezi kutangaza wote.”

Hata hivyo, Meza ya Mhariri wa Jamii ina maoni kuwa kutotangaza majina ya waliofeli hakuna uhusiano wowote na kuvunja “haki za binadamu;” bali wahusika wanatumia weledi na hekima, kuamua kipi kitangazwe wapi, kwenye nafasi ipi, lini na kwa maarifa au “furaha” na faraja ya wengi.

Hapa, vyombo vya habari vinatoa mwanga uletao wepesi wa kufikiri (kama ilivyo kwa aliyeuliza swali); bila kuziba fursa ya kupata taarifa zaidi.

Msomaji anayeleta hoja ya pili, Noor Shija anapingana na msomaji Richard Mgendi aliyelalamikia kichwa cha habari, ‘Jinsi mhasibu alivyomuua mkewe, mtoto na shemeji yake.’

Mgendi anajenga hoja kwamba “mhasibu hakuua;” aliyeua ana jina lake na wahasibu hawapaswi kuhusishwa.” Ingawa hasemi jina ndilo litumike, yeye haoni sababu ya kutaja ‘jina la kazi’ katika nafasi ya mtuhumiwa.

Bali Shija, mmoja wa wahariri katika gazeti hili, anasema “…kutaja cheo cha mtu mwenye taaluma fulani au nafasi ya uongozi serikalini pale anapofanya (au anapohusishwa) na tukio la uhalifu, kunafanya habari ishike nafasi kubwa; vilevile ni fursa kwa wanataaluma wengine kutazama upya nafasi zao au mafunzo yao.”

Shija anasema, “…majina ya watu, vyeo vyao au umaarufu wao ndivyo vinavyopima uzito wa habari…mfano, kama tukio linamhusu mwalimu Juma kumbaka mwanafunzi, kichwa cha habari kinachofanya habari iwe kubwa ni ‘Mwalimu ambaka mwanafunzi’ na siyo ‘Juma ambaka mwanafunzi.’

“Juma anaweza kuwa mtu yeyote; pengine mlevi, mwehu au kibaka. Hakuna atakayeshangaa iwapo mtu wa aina hiyo ametenda ubakaji.

“Mwalimu ndiye mwenye jukumu la kumlea mwanafunzi shuleni, ndiye ana mafunzo yote ya namna ya kumlea mwanafunzi. Kwahiyo, itashangaza wengi atakapohusika kwenye ubakaji,” anasisitiza.

Shija anasema kutaja jina la kazi (mwalimu) katika nafasi ya mtuhumiwa, kunaweza kuonesha kuwa anahitaji kusaidiwa; lakini pia kunasaidia wazazi kuchukua tahadhari za haraka kwa watoto wao.

“Kichwa cha habari lazima kitengenezwe kwa namna ya kumvutia msomaji na kumfikirisha. Kiongozi wa dini… polisi au mwanajeshi akibaka, ni vema kutumia jina la cheo chake kwa kuwa hatarajiwi” kufanya tendo la aina hiyo, anasisitiza Shija.

Mjadala unaendelea.

Tuandikeje: Tutengeneze vichwa vya kuvutia, kuongeza ‘ukubwa’ na ‘uzito wa stori’ au kwa uhalisia? Je, ni majina pekee yawezayo kueleza kwa uzito, katika kichwa cha habari, kile kilichomo katika taarifa/habari? Wewe unasemaje?

Advertisement