Wabunge wajitathmini kwa aliyosema Rais Magufuli

Rais John Magufuli

Muktasari:

  • Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL baada ya kutokubaliana katika tozo ya uwekezaji. Tanesco ambalo ni shirika la umma lilikuwa linadai limepangiwa tozo kubwa kinyume cha gharama halisi za uwekezaji.

Juzi Rais John Magufuli alimmwagia sifa mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila kwa kuibua na kulivalia njuga sakata la uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.

Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL baada ya kutokubaliana katika tozo ya uwekezaji. Tanesco ambalo ni shirika la umma lilikuwa linadai limepangiwa tozo kubwa kinyume cha gharama halisi za uwekezaji.

Magufuli alimwaga sifa hizo mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wake wa hadhara katika vijiji vya Uvinza na Nguruka wilayani Uvinza, Kigoma ambako alizindua mradi wa maji uliogharimu Sh2 bilioni. Mradi huo utahudumia vijiji vya Nguruka, Bweru, Nyangabo, Itebula na Kasisi.

Kwa msisitizo alisema: “Lazima niwe mkweli na nisiposema hapa nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu. Siku zote ukweli utabaki kuwa ukweli tu na ndio maana nampongeza Kafulila kwa sababu alisimama imara kupigania masilahi ya umma. Alionyesha uzalendo wa hali ya juu unaopaswa kuigwa na kila mmoja wetu.”

Hatua ya Rais Magufuli kumpongeza mbunge huyo wa zamani, iwazindue wabunge wote, wa chama tawala na upinzani kuzingatia hoja katika mijadala yao badala ya sura na vyama.

Kila mbunge yupo bungeni kujadili maendeleo ya wananchi wa jimbo lake na nchi na si vinginevyo na Kafulila ingawa alikuwa mbunge wa chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi alitanguliza uzalendo akatetea maslahi ya nchi. Jambo la kusikitisha ni kwamba baadhi ya wabunge waliompinga hawakujadili hoja zake, bali walimpinga kwa sababu ya itikadi za kisiasa na kichama. Wengi hao hawakuwa na hoja zaidi ya kusema Kafulika alikuwa mwongo.

Madhara ya kupinga kila hoja kwa sababu ya itikadi kutoka kwa wapinzani au wabunge machachari kutoka CCM ndio maana wengi wao walijikuta wakimpinga Kafulila ambaye alikuwa akitumia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyefanya ukaguzi na kufafanua kwamba, Sh306 bilioni ambazo zilichotwa kifisadi kutoka akaunti hiyo zilikuwemo fedha za serikali

Utamaduni huo ni mbaya na mwingine mbaya zaidi ni wa kuzomea wabunge wanaojadili hoja fulani kwa sababu tu wao ama hawaijui vizuri au hawaitaki. Katika mijadala ya namna hiyo, baadhi ya wabunge kwa sababu ya ushawishi wao huwasema wenzao kwa mambo binafsi kama njia ya kuzima hoja zao.

Katika sakata hilo la Tegeta Escrow, kwa mfano, baadhi ya wabunge waliwashutumu bila ushahidi waliosimamia hoja kwamba walihongwa na Kafulila aliitwa tumbili ndani ya Bunge na nusura apigwe kwa sababu ya msimamo wake.

Miaka minne tangu sakata hilo lilivyojadiliwa wakati mwingine kwa mihemko na maamuzi yake yakatekelezwa nusu, Rais Magufuli amemfuta machozi Kafulila kwa kusema wazi waliomuita mbunge huyo wa zamani kuwa tumbili, wao ndio wamegeuka kuwa tumbili baada ya vyombo vya dola kufuatilia kwa kina na watuhumiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Hatua ya Rais Magufuli kutoa sifa kwa Kafulila iwe fundisho kwa wanasiasa na hasa wabunge kwamba mara zote wazingatie hoja zinazotolewa na siyo sura au itikadi za siasa au mipaka ya kieneo.

Mara zote wajue kwamba maendeleo hayana vyama vya siasa na uhalifu hauna mipaka ya vyama, mafisadi na walarushwa wanaweza kutoka chama tawala au upinzani na Taifa liungane kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria.