Thursday, September 14, 2017

Wabunifu! EAC inahitaji nembo, bendera mpya

 

By Filbert Rweyemamu

Vijana ni nguvukazi muhimu katika kufanikisha mambo ya msingi katika jamii. Umuhimu wao umetambuliwa na Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) lililowapa jukumu la kubuni nembo zitakazoitambulisha.

Baada ya utafiti uliofanywa kati ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na EAC mwaka 2013 katika nchi tano wanachama wake, pamoja na mambo mengine wananchi waliofikiwa walionyesha kutozitambua vyema nembo za jumuiya hiyo.

Wananchi wa wilaya za Monduli na Arumeru za Arusha, Bahi na Mpwapwa za Dodoma, Ilemela na Nyamagana za Mwanza na Tarime iliyopo Mara walitoa maoni yao na kubainisha kutozitambua bendera na nembo ya EAC.

Alama maalumu za utambulisho ni muhimu kwa sababu huibeba taasisi na kuitambulisha katika mawasiliano rasmi ya ndani, nje au kwenye machapisho mbalimbali ya taasisi husika.

Kama taasisi inayokua kimuundo, jumuiya imejipima na kuona kuna sababu ya kubadilika kimwonekano kutokana na mahitaji. Itakumbukwa, jumuiya hii ilianzishwa na nchi tatu pekee ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda hivyo nembo na bendera zilizingatia mahitaji ya wakati huo.

Kwa mujibu wa kanuni za nembo za EAC za mwaka 2004 zilizoanzisha alama za utambulisho huo, zinaonyesha kuwa mwaka 2008 yalifanyika mabadiliko yaliyojumuisha kuongeza mwonekano wa kijiografia wa nchi za Rwanda na Burundi kwenye nembo hiyo.

Mwanachama mpya, Sudan Kusini ambaye katika mkutano wa 17 wa wakuu wa EAC uliofanyika jijini Dar es Salaam alipokelewa na kuwa mwanachama wa sita hatua ambayo imelishawishi baraza la mawaziri la EAC kutoa uamuzi huo.

Vijana kutoka nchi zote sita wamepewa kazi mahsusi ya kuamua nembo na bendera ya EAC ionekane kwa namna ipi. Hii ni heshima ambayo kwa hakika imepatikana kwa busara za viongozi hao ambao wangeweza kutangaza zabuni kwa kampuni yoyote kutoka ndani au nje ya jumuiya.

Kwa muda mrefu vijana wamekuwa wakilalamika kubanwa na wanaowaita ‘wazee’ kwa madai ya kuzuiwa kuonyesha uwezo wao wa maarifa na ubunifu katika nyanja mbalimbali.

Sasa huu ni wakati wa kuonyesha uwezo kupitia ubunifu wa sanaa za uchoraji ambao utaacha alama ya kudumu.

Kwa mujibu wa EAC, kumekuwepo na pengo la utambulisho wa nembo na wakati mwingine kutumika zisizo rasmi na kusababisha mkanganyiko wa mawasiliano hasa mihimili ya jumuiya hiyo ambayo ni bunge (Eala) na mahakama (EACJ).

EAC katika mpango mkakati wa mawasiliano kupitia nembo na bendera imeamua kuiga namna nembo na bendera za taasisi au mashirika mengine kama Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU) na taasisi zake unavyojitambulisha.

Ikumbukwe EAC ina taasisi kadhaa zikiwamo Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC) yenye makao yake Zanzibar, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) na nyingine ambazo zipo katika utaratibu maalumu wa kuwa na utambulisho unaojiungamanisha na nembo ya EAC.

Washindi watatu watakaofanikisha mradi watazawadiwa Dola 35,000 za Maerekani (zaidi ya Sh77 milioni) wakati gharama zote zikiwamo nembo ni zaidi ya Dola 200,000.

Shime wabunifu wa Tanzania onyesheni uwezo kwa kuipa sura mpya jumuiya yetu.

Pamoja na uhamasishaji mwingine unaofanywa kuwahimiza vijana kuchangamkia fursa za biashara zilizopo miongoni mwa nchi wanachama, kuifahamu jumuiya hiyo ni jambo muhimu sana.

Filbert Rweyemamu ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha. Anapatikana kwa simu 0754 945670

-->