Monday, June 19, 2017

Wagombea wajitathmini kabla ya kuomba TFF

 

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuandika, ‘Inawezekana timiza wajibu wako’. Kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere inafaa kutumika hasa wakati huu ambao wadau mbalimbali wa michezo wameanza kuchukua fomu ili kuwania uongozi kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kujitokeza na kuchukua fomu ni kutimiza wajibu ambao kila mdau, mpenzi wa michezo anao katika kuitumikia na kuikuza sekta hiyo ya soka, mchezo tunaoimbiwa siku zote kuwa unapendwa na watu wengi.

Uchaguzi huo unafanyika wakati huu ambao timu zetu za Taifa, zina majukumu makubwa ya kupeperusha bendera ya nchi kuwania nafasi ya kushiriki mashindano mbalimbali, yakiwamo ya Afrika (Afcon), pia yale ya wachezaji wa ndani (Chan), zikiwa kwenye hatua za awali kabisa.

Kutokana na wajibu huo, tunaamini wale wanaojitokeza sasa kuomba ridhaa ya kuongoza TFF watakuwa wakitambua wajibu huo mkubwa, ambao upo mbele yao katika kuhakikisha timu zetu zinafanya vizuri na hivyo kuitangaza nchi yetu kimataifa.

Tunatumia nafasi hii kuwapa angalizo wale wanaochukua fomu kwamba wajitambue kwanza. Wajiuliza kwa nini wanaomba ridhaa hiyo ya kuongoza shirikisho hilo linalosimamia mchezo huo nchini.

Kwa kufanya hivyo, tunaamini, ifikapo Agosti 12, kupitia mchakato ambao tayari umeanza, tutakuwa na wagombea wanaofaa na wenye sifa ya kuongoza soka letu linalopita kwenye kipindi kigumu.

Ni lazima wagombea watambue kuwa wanataka kupewa ridhaa ya kuongoza wakati huu ambao kwa mfano, Zanzibar tayari imepewa uanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), inasaka ule wa Fifa, jambo tunaloamini kuwa ni hatua nzuri kuelekea kuitangaza nchi kimataifa kupitia soka.

Sanjari na hilo, tunawashauri wagombea watakaokuwa wamejipima na kuona wanatosha kuongoza TFF hasa kipindi hiki wajiulize, wana ajenda gani za kuingia nayo kwenye shirikisho, siyo tena mahali pa kujifunzia, tukiamini kwamba kuna vyama shiriki kwa ngazi ya mikoa na wilaya ambako ndiko pa kuanzia hatua za awali za uendeshaji wa michezo.

Tunawataka wagombea waingie kwenye mchakato wa uchaguzi wakijiuliza, wanakwenda kuifanyia nini TFF, siyo shirikisho hilo litawafanyia nini.

Kwa hilo, lazima tuweke msisitizo kuwa kuongoza shirikisho ni jukumu kubwa na zito ambalo si la kufanyia mzaha ambao umekuwa ukionekana kwenye uendeshaji wa shughuli za michezo nchini kwa miaka mingi.

Tunahitaji kuwa na viongozi watakaokuwa tayari kuongoza soka kuelekea kuwa mchezo wa kulipwa, wenye mipango, mikakati endelevu, siyo ubabaishaji au maneno matamu, ambayo utekelezaji wake ni sifuri. Tufike mahali tuwe na viongozi wa soka, ambao wanasema kwa vitendo na dhamira zao zinawatuma kuwatumikia wapenzi wa soka, siyo wale ambao wametumwa na dhamira za kuchumia matumbo yao, kutumikia masilahi ya makundi fulani au ushabiki wa timu au klabu, jambo ambalo linadhoofisha mchezo wa soka Tanzania.

Tunaamini, mchakato wa kupata viongozi wa kuiongoza TFF utakuwa huru na haki ambao unazingatia kanuni, taratibu na ambao hautoi nafasi ya kuwapo kwa rushwa wala maovu mengine ili kuwapata viongozi wa kusimamia chombo hicho.

Lazima tuwe na viongozi wa kweli wa soka, ambao ni wanamichezo kwa vitendo vyao, siyo maneno au ghilba.

-->