Wajasiriamali wasaidiwe kurasimisha kazi zao

Ephraim  Bahemu

Muktasari:

Taifa lolote lenye maendeleo ya kiuchumi, ni dhahiri kwamba watu wake wanafanya shughuli nyingi za kijasiriamali ambazo ni matokeo ya kujituma kwao na uwezeshaji kutoka serikalini.

Ujasiriamali ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi katika jamii.

Taifa lolote lenye maendeleo ya kiuchumi, ni dhahiri kwamba watu wake wanafanya shughuli nyingi za kijasiriamali ambazo ni matokeo ya kujituma kwao na uwezeshaji kutoka serikalini.

Serikali hutoa kipaumbele kwa watu hao, kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya ujenzi wa uchumi wa nchi na hupunguza tabaka la watu tegemezi.

Tanzania kuna idadi kubwa ya watu wanaojishughulisha na ujasiriamali, kwa lengo la kutaka kujikomboa kiuchumi.

Hata hivyo, kuna changamoto hususani kwa wajasiriamali wadogo, kwani wengi hawajarasimisha biashara zao, jambo linalowasababishia kukosa fursa mbalimbali.

Kurasimisha ni kuifanya biashara yako kuwa rasmi kwa kufanya usajili katika mamlaka husika; kuwa na vibali vyote vinavyohitajika katika biashara yako na kuwa na mpango biashara unaoonyesha shughuli unayoifanya.

Kwa mfano, baadhi ya kampuni haziwezi kutoa tenda ya kusambaziwa bidhaa fulani na mjasiriamali ambaye biashara yake haijasajiliwa na mamlaka za kiserikali.

Wengine watataka kuona taarifa ya mwenendo wa biashara yako katika kipindi fulani, ili kujiridhisha kuwa unaweza kufikia matarajio yao sambamba na kuona tathmini ya huduma uliyoitoa kabla.

Taasisi za kifedha ili nazo ziweze kutoa mkopo zitahitaji kuona mpango wa biashara yako na utendaji ulivyokuwa katika kipindi fulani, ili kuwajengea imani kuwa una uwezo wa kukopesheka.

Ikumbukwe kwamba wajisiriamali wadogo wamekuwa wakihangaikia suala la mitaji na mikopo kutoka katika taasisi za fedha, lakini wamekuwa hawaaminiki.

Matatizo yote hayo yanatokana na kutorasimishwa kwa biashara za wajasiriamali. Na hili linasababishwa na wengi wao kukosa elimu au kutoona umuhimu wa kurasimisha shughuli zao.

Katika hili wajasiriamali wadogo wanapaswa kubadili fikra na kuanza kufikiri namna ya kuondoa kikwazo hiki ili watoke walipo na kuelekea daraja jingine lenye manufaa.

Kwa mfano, hakuna haja ya muuza nyanya kuzipanga chini mchangani, wakati angeweza kutafuta meza iliyo safi.

Kwa wauza vyakula, nao wanaweza kuomba vibali kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ili bidhaa zao zithibitishwe na kutambuliwa.

Mapinduzi ya teknolojia sasa yatumike kujipatia taarifa kuhusu nini cha kufanya na nani wa kumuoana.

Mitandao sasa imejaa taarifa tuitumie vizuri na pale itakaposhindikana tuulize kwa watu wanaotuzunguka au maofisa wa Serikali.

Serikali nayo iweze kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka kwa wajasiriamali hawa, inapaswa kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwao hao hususani urahisi wa kufikia huduma za mamlaka tofauti.

Huduma katika mamlaka za utoaji wa vibali na leseni, zinapaswa kuboreshwa na kuharakishwa.

Hapa namaanisha kwamba kila mtu aliye kwenye nafasi ya kumsaidia mjasiriamali atekeleze wajibu wake kwa maendeleo yao.

Aidha, Serikali inapaswa kuwashawishi wananchi na kuwapatia elimu kuhusu ujasiriamali na njia za kupita kuelekea kwenye urasimishaji.

Msisitizo wa ulipaji kodi kama tunavyouona sasa, hautokuwa na maana kama hakuna msukumo wa kuwapo kwa njia bora za kupata kodi hizo.

Ikumbuke kama kila mmoja atatekeleza wajibu wake kati ya Serikali na wajasiriamali, sioni sababu kwa nini makusanyo ya kodi yasiongezeke na hatimaye kukua kwa uchumi wa Taifa..

0756939401