Waliomshambulia Lissu wakamatwe, wawajibishwe

Muktasari:

  • Mbunge huyo alishambuliwa juzi mchana mjini Dodoma baada ya kutoka bungeni kwenda nyumbani kwake Area D kwa mapumziko, na kabla hajateremka kwenye gari walijitokea watu wakaanza kulifyatulia gari lake risasi.

Tukio la watu wasiojulikana kumshambulia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu Juzi kwa risasi limewashtua Watanzania na kuzua mijadala miongoni mwao na wapenda haki ndani na nje ya nchi.

Mbunge huyo alishambuliwa juzi mchana mjini Dodoma baada ya kutoka bungeni kwenda nyumbani kwake Area D kwa mapumziko, na kabla hajateremka kwenye gari walijitokea watu wakaanza kulifyatulia gari lake risasi.

Kwa mujibu wa Spika wa Bunge kati ya risasi 32 zilizofyatuliwa, tano zilimpata mbunge huyo, moja kwenye mkono, mbili mguuni na mbili tumboni. Kwa sababu amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

Ni tukio ambalo kama walivyoeleza watu mbalimbali akiwamo Rais John Magufuli linafaa kulaaniwa na kukemewa kwa nguvu zote kwa kuwa linaelekea kutoa kwenye reli ya ustaarabu tuliozoea kwa miaka mingi.

Uzito wa suala hili hauhitaji maelezo ya kutia chumvi, bali unajionyesha wazi kupitia jinsi lenyewe lilivyopokelewa na vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na watu mbalimbali kote duniani, ambako watu wengi wameeleza kulaani na kulikemea.

Zaidi ni kwa jinsi Watanzania wanavyolizungumzia tukio hilo na wanaendelea kulijadili katika makundi, vijiwe, bungeni na mahali pengine wakionyesha kuguswa, kusikitishwa na kukerwa na shambulio hilo.

Ni tukio ambalo limesababisha Tanzania itazamwe kwa jicho tofauti duniani hasa baada ya mataifa makubwa kama Marekani, vyombo vya habari duniani na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu kama Amnesty International.

Pia limelaaniwa na kukemewa na taasisi za wanasheria Tanganyika, Zanzibar na Kenya kwa kutoa matamko ya kulaani shambulizi hilo.

Kama ambavyo taasisi zote hizo na matamko mengine ya yaliyotolewa tangu juzi ndani ya nchi yanashauri, tungependa kuungana nao kulitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wahusika wa shambulio hilo wanasakwa, wanakamatwa na kuchukuliwa hatua zinazoonekana.

Endapo suala hili litachunguzwa kwa kina na wahusika kukamatwa, itaondoa kiwingu kilichopo kinachosababisha taifa letu litazamwe kwa jicho tofauti.

Tunalazimika kuwakumbusha polisi wajibu wao tukikumbuka matukio mengine yaliyopita ambayo pamoja na jeshi hilo kuahidi kuyachunguza na kuchukua hatua, hakuna taarifa zozote zilizoeleza hitimisho lake.

Matukio hayo ni kama shambulio la Dk Stephen Ulimboka, kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane, shambulio la Absalom Kibanda, Kutekwa kwa Roma Mkatoliki, kulipuliwa kwa ofisi za kampuni ya uwakili ya IMMMA, kutishiwa bastola kwa Nape Nnauye na mengine mengi.

Ifike hatua jeshi hilo ambalo mara nyingi limejinasibu kuwa na mafunzo, weledi na vifaa stahiki, lianze kuchukua hatua kulingana heshima lililojijengea, ili kutoa matokeo ambayo, mbali na kulifanya liaminike zaidi, litawafanya wananchi wawe na mwamko wa kulisaidia kutika utoaji wa taarifa za kiuhalifu.

Lakini endapo jeshi hilo litaendelea na mtindo wake wa kufanya uchunguzi wa matukio tata na kuishia katika lindi la ukimya bila kueleza hitimisho, ari na mwamko wa wananchi kutoa taarifa, utaendelea kufifia na pengine hata wanaohusisha katika baadhi ya matukio hawatapata mtu wa kuwasahihisha na kuwaeleza ukweli.

Kila mmoja anatamani kuona wahalifu wanaojihusisha na matukio hayo yanayoichafua nchi, wanakamatwa na sheria kuchukua mkondo wake ili kila mtu apate haki anayostahili kulingana na matendo yake.