UCHAMBUZI: Wamachinga changamkieni vitambulisho hivi

Mara kwa mara, Rais John Magufuli akiwa kwenye ziara za kikazi amekuwa akitoa maagizo ya kutaka wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga na akina mamalishe wasibughudhiwe.

Kwa kutambua umuhimu wa wafanyabiashara hao, hivi karibuni amekwenda mbali zaidi kwa kuandaa mpango wa kuwatambua wafanyabiashara hao kupitia vitambulisho maalumu.

Vitambulisho hivyo vitawahusu wafanyabiashara wale ambao mapato yao hayazidi Sh4 milioni kwa mwaka na ametaka wasibughudhiwe baada ya kulipia Sh20,000 ya kitambulisho kwa kila mmoja. Hatua hiyo imelenga kuwasaidia wafanyabiashara hawa ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakikumbana na adha ya kufukuzwa huku na kule na hivyo kuwasababishia hasara baada ya bidhaa zao kuharibika.

Tumeshuhudia katika sehemu mbalimbali wafanyabiashara hawa wakiiomba Serikali iwatambue na kuwatengea maeneo maalumu kwa ajili ya kufanya shughuli zao.

Ni kama vile Rais Magufuli amesikia kilio chao, lakini safari hii ameamua kuja kwa staili nyingine ya kuwapa vitambulisho vitakavyowafanya watambuliwe na kutosumbuliwa kwenye shughuli zao.

Baada ya Rais kutaja hadharani mpango huo wa vitambulisho, wafanyabiashara wa kada husika walizungumza na vyombo mbalimbali vya habari huku wakionyesha kufurahia hatua hiyo.

Wengine walikwenda mbali zaidi kwa kusema hatua hiyo itakuwa ni mwarobaini wa kero walizokuwa wakizipata miaka kadhaa iliyopita wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

Katika kuonyesha wanawajali wafanyabiashara siku ya pili baada ya Rais kutoa vitambulisho hivyo, baadhi ya wakuu wa mikoa walianza mchakato wa kuwapa wakuu wa wilaya vitambulisho ili wawape wafanyabiashara husika.

Tayari imeshuhudiwa mwamko unaoridhisha kwa baadhi ya wafanyabiashara wa wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakijitokeza kwa wingi kuchukua vitambulisho hivyo ili wafanye shughuli zao kwa ufanisi.

Mwitikio huo unaonyesha namna wafanyabiashara hao walivyo na hamu ya kufanya shughuli zao katika mazingira bora ya kutambuliwa pasipo kubughudhiwa na watendaji wa Serikali.

Nitumie fursa hii kuwashauri wanafanyabiashara kuchangamkia fursa hii adhimu ya kupata kitambulisho ambacho kitakuwa nguzo muhimu kwao kama Rais Magufuli alivyosema kuwa watakaokuwa navyo hawatabughudhiwa.

Najua muda bado upo wa kupata vitambulisho, lakini baadhi ya Watanzania tumekuwa na desturi ya kusubiri siku ya mwisho ya jambo fulani ndipo tujitokeza kwa ajili ya kupata huduma.

Hiki ndicho ninachokiona kwa baadhi ya wafanyabiashara wa wilaya kadhaa hapa Dar es Salaam, ambao licha ya kuwa na uwezo wa kuvipata vitambulisho hivyo, lakini hawako tayari kuvichukua kwa sasa .

Ukifuatilia kwa karibu watu haohao ndio waliokuwa wakilalamika kwa nyakati tofauti wakiiomba Serikali iwatambue na kuwatengea maeneo mazuri ya kufanyia biashara.

Naomba wafanyabiashara tusifike huko au kusubiri kubembelezwa kuchukua vitambulisho hivi, kama uwezo unao ni vyema ukaanza sasa mchakato wa kujaza fomu kupitia kiongozi wako wa biashara au kwenda mamlaka husika

Wale wasiokuwa na uwezo kwa wakati huu ni vyema wakaanza kujipanga taratibu kwa kuweka fedha kidogo kidogo za kuhakikisha wanapata vitambulisho ambavyo ni nyenzo muhimu kwenye shughuli zao.

Tumesikia baadhi ya wilaya zilizoanza kugawa vitambulisho zikisema hata wale ambao hawapo katika mfumo, wana fursa ya kupata kwa utaratibu watakaopewa ambao hauna tofauti na walioutumia wale wengine.

Pia huu ni wakati mwafaka kwa manispaa na halmashauri kupita maeneo mbalimbali ya biashara na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa vitambulisho hivi, jambo litakalosaidia mwamko wa watu kujitokeza na kuvichukua.

Tunaweza kuwalaumu wafanyabiashara wachache kujitokeza kumbe baadhi yao hawana uelewa kuhusu vitambulisho hivyo vilivyotolewa na mkuu wa nchi. Inawezekana kabisa baadhi ya wafanyabiashara hawakuilewa dhamira njema ya Rais Magufuli, ni vyema viongozi na watendaji tutumie fursa hii kuanza kuwapa elimu kuhusu jambo hili.

Suala hili linawezekana hasa kwa kutumia magari yenye vipaza sauti au kuandaa mikutano ya wafanyabiashara kupitia kwa viongozi wao.

Ni wakati wenu sasa wafanyabiashara ndogo. Zamani mlilalamika kuwa hakukuwapo na kiongozi anayewajali. Sasa mmepata ndio maana siku hizi bugudha kwenu zimepungua. Kazi kwenu, itumieni nafasi hii adimu.

Bakari Kiango ni mwandishi wa Mwananchi anapatikana kwa simu namba 0719-999988