Wanafunzi wapewe elimu ya lishe wangali wadogo

Tazania bado inakabiliwa na tatizo sugu la lishe licha ya kuzalisha chakula kwa wingi kila mwaka.

Tatizo hilo ni kubwa zaidi kwa watoto walio chini ya miaka mitano ambapo asilimia 16 wana uzito mdogo huku asilimia 34 wakiathiriwa na utapiamlo.

Ukosefu wa lishe bora kwa watoto umewaathiri wanafunzi shuleni wakishindwa kujifunza darasani kwa kukosa vyakula vinavyoimarisha ubongo na mwili kwa ujumla.

Ukosefu wa lishe bora umeathiri nguvu kazi kwa Taifa na kusababisha umaskini wa kipato katika jamii nyingi.

Juhudi zimekuwa zikifanywa na wadau ili kupambana na tatizo la lishe nchini. Miongoni mwa juhudi hizo ni kuongeza viini lishe kwenye vyakula vinavyoliwa kwa wingi.

Zao la viazi vitamu ndilo limeonekana kuliwa kwa wingi zaidi likitegemewa na asilimia 60 ya Watanzania kama chanzo cha lishe na kipato.

Zaidi ya hekta 760,000 sawa na tani 3.8 milioni huvunwa kila mwaka (tani 5.03 kwa kila hekta).

Wataaamu wa lishe wameviongezea vitamin A na madini mengine viazi vitamu ili vinapoliwa mlaji apate virutubisho muhimu kwa pamoja na hivyo kupambana na utapiamlo.

Kwa kuwa viazi vitamu vimekuwa vikilimwa kwa muda mrefu, juhudi sasa zimeelekezwa kwenye usambazaji wa mbegu zilizoboreshwa (viazi lishe) kwa wakulima wadogo, ikiwa ni pamoja na kushawishi mabadiliko ya mitalaa ya shule, ili kuwawezesha wanafunzi kusambaza, kulima na kujua kupika viazi na jinsi ya kuandaa mlo kamili wakiwa shuleni.

Hata hivyo imeonekana kuna uelewa mdogo wa masuala ya lishe miongoni mwa walimu wa shule za msingi na sekondari.

Kwa mfano, tathmini iliyofanywa na Jukwaa la Kilimo la Asasi Zisizo za Kiraia (Ansaf) kuhusu mtalaa wa elimu ya msingi wa 2005 kama unahusisha masuala ya lishe na jinsia katika silabasi ya mwaka 2016, ilionekana bado kuna upungufu.

Tathmini hiyo ilifanywa katika shule tano kutoka Wilaya ya Mkuraga mkoani Pwani na Wilaya ya Gairo, Mkoa wa Morogoro ikhusisha wanafunzi 30 na walimu 12.

Imeonekana kwamba ufundishwaji unafanyika kwa nadharia badala ya vitendo. Vilevile suala la umiliki wa ardhi, majukumu ya jinsia katika uzalishaji, utayarishaji na uandaaji wa chakula hayakupewa kipaumbele katika silabasi hiyo.

Tathmini hiyo ilibaini kuwepo kwa tofauti ya viwango vya elimu katika ubora, uzoefu na masomo wanayofundisha, japo wameonyesha uelewa mzuri kuhusu lishe na mlo kamili.

Walimu waliohojiwa wakati wa kufanya tahmini hiyo walishauri masomo ya mlo kamili na lishe yawekwe kwenye masomo ya sayansi na ya ukuaji na uzalishaji wa mazao ya chakula na uandaaji pamoja na upikaji wake ndiyo yafundishwe kama stadi za kazi.

Utafiti mwingine uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzaia (Tari) na kuwasilishwa hivi karibuni Dar es Salaam, umeonyesha umuhimu wa kusambaza mazao ya mizizi yaliyoongezewa lishe kwa wakulima wadogo kupitia wanafunzi.

Kwa mfano katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kama vile Mwanza, Tabora na Geita wanafunzi wametumika katika kusambaza mbegu za viazi kwa wazazi na walezi wao kiasi cha kurahisisha upatikanaji wa mbegu za viazi zilizoboreshwa.

Ni wakati sasa kwa Serikali kuiangalia sekta ya elimu kama kichocheo cha kukuza lishe hasa kwa watoto. Wazazi wapatiwe elimu ya kutosha ya lishe ili kuepusha utapiamlo kwa watoto na jamii nzima.

Ukosefu wa elimu ya kutosha ya lishe umesababisha watoto kupata utapiamlo na hatimaye kudumaa.

Imeonekana kuwa watoto wengi huondoka nyumbani kwenda shule bila kupata staftahi na hata wanapofika shule hukaa muda mrefu wakiwa na njaa. Matokeo yake wanashindwa kuelewa masomo darasani na mwishowe kufeli mitihani.

Aidha, shule zinapaswa kuandaa milo kwa wanafunzi ikiwamo uji au chai ya asubuhi na chakula cha mchana. Mlo huo unapaswa kuwa na virutubisho vya kutosha na siyo kujaza matumbo. Watoto washirikishwe katika uandaaji wa chakula ikiwa ni sehemu ya masomo ya stadi za kazi.

Vilevile, suala la lishe lipewe kipaumbele kama moja ya mikakati ya kuimarisha elimu.

Ni aibu kwa Tanzania inayojitosheleza kwa chakula, lakini bado utapiamlo unabaki kuwa tatizo sugu. Tuondokane na hali hii kwa kuweka mikakati kwa wanafunzi wakiwa wadogo.

Haiwezekani Taifa letu ambalo vyakula vinalimwa kwa wingi tukashindwa kuwahudumia watoto wetu shuleni kwa chakula.

Mwanadishi anapatikana kwa baruapepe; [email protected]